TARATIBU ZA TIBA ZA RAIS ZAKAMILIKA
Taratibu za matibabu ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete (Pichani), zimekamilika leo, Jumatatu, Novemba 24, 2014.
Taratibu hizo za matibabu za
Mheshimiwa Rais Kikwete zimekamilika kiasi cha saa 12 asubuhi ya leo
wakati madaktari bingwa katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko mjini
Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani, walipomfanyia hatua ya mwisho ya
tiba.Hata hivyo, Rais Kikwete ataendelea kupumzika na kuangaliwa kwenye Hoteli Maalum inayohusiana na Hospitali ya Johns Hopkins kwa siku mbili hadi tatu kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani.
Kama kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa na madaktari, Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani Jumamosi, Novemba 29, 2014.
Rais Kikwete aliondoka nchini Alhamisi ya Novemba 6, 2014, kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya yake lakini madaktari katika Hospitali ya Johns Hopkins waliamua kumfanyia upasuaji wa tezi dume Jumamosi ya Novemba 8, 2014.
Rais Kikwete anaendelea kuwashukuru Watanzania kwa sala na maombi yao ya kumtakia heri ya kupona haraka na kurejesha afya njema katika kipindi chote cha ugonjwa wake.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
24 Novemba,2014
Post a Comment