ad

ad

AHADI YA NDOTONI - 13










ILIPOISHIA: “Aliyozunguza ni msamaria mwema anayekufahamu, sikuweza kukubali mara moja mtu aliyekuokota njiani ajue kila kitu kilichokupata kuwa umeunguliwa sijui gari, gari lilionekana kweli limeungua, lakini nyumba na duka lako amejuaje?”
“Kwani aliyenileta alisema anaitwa nani?” SASA ENDELEA...

“Mmh! La...la...shi...Jina lake kweli...sijuiii...”
“Au Lakashi?”
“Sawa sawa kabisa anaitwa Lakashi.”
 “Mungu wangu huyu kiumbe ananitaka nini?”
“Unamfahamu?’

“Ndiye aliyenisababishia yote haya.”
“Mbona ndiye aliyekuokota na kukuleta hapa kisha kukulipia fedha za matibabu.”
“Muongo mkubwa shetani mkubwa yule,” Jeska alisema kwa hasira.
“Siamini usemayo, yule bwana ni mstaarabu kuliko wastaarabu, pamoja na kukufahamu kwa juu juu, huwezi amini jamaa kaondoka alfajiri baada ya hali yako kuwa nzuri, kama angekuwa mtu mbaya asingevumilia kuumwa na mbu pia kuacha usingizi wake,” muuguzi alisema.

“Muuongo mkubwa, tena muuaji asiye na huruma,” Jeska alizidi kubwata kwa sauti ya juu.
“Mbona hatukuelewi?”
“Hamuwezi kunielewa, yule bwana ni mnafiki mkubwa, si tumeachana ananifuatia nini?”
“Jeska uko sawa?” daktari alimuuliza.
“Ni sawa wala sina tatizo lolote katika akili yangu, kama ni kweli alivyonipatia vimeungua aachane na mimi.”

“Kumbe mnajuana?”
“Alikuwa mume wangu tumeachana, lakini nashangaa bado ananifuata.”
“Unataka kusema ndiye aliyefanya uharibifu wote huo?”
“Ndiyo.”
“Kwa nini usipeleke taarifa polisi?”

“Haina haja kama kachoma vitu vyake ya nini kumpeleka polisi?”
“Sasa utaishi vipi?”
“Nitajua mwenyewe.”
“Na kwa nini umebadili jina lako?”
“Jibu mnalo, nashangaa mnaniuliza, huyo huyo mwana haramu aliyenitia umaskini, ndiye aliyenibadili jina na dini ili anifanye mtumwa wake.”
“Mmh! Makubwa.”

“Kutokana na tatizo lililokupata, vipimo hukupata tatizo kubwa zaidi ya mshtuko, kwa hiyo tutakupa ruhusa ya kutoka hospitali leo.”
“Hakuna tatizo.”
Jeska alisema huku akinyanyuka kitandani katika vazi la aibu, alikuwa amevalia gauni lililoacha wazi sehemu kubwa ya mwili wake. Mgongo wote ulikuwa  nje na chini liliishia chini kidogo ya makalio. Vazi lile lilimfanya daktari asimuangalie  mara mbili.
“Una ndugu?” Alimuuliza.

“Ninao, lakini simu nimepoteza.”
“Mmh! Kweli, simu yako aliileta yule kaka aliyekuokota.”
Muuguzi alikwenda ofisini na kurudi na simu ya Jeska pamoja na gauni refu. “Hili gauni la nani?”
“Alisema uvae usitiri  maungo yako.”

Jeska hakubisha kulichukua gauni kutokana na vazi lake la aibu, baada ya kulivaa, alionekana mstaarabu, aliwapigia  simu baba zake wadogo. Baada ya muda walifika hospitali kumchukua na kumpeleka kwao. Alipofika kwa baba zake muda wote alikuwa akilia akikumbuka maisha mazuri aliyokuwa akiishia na kubadilika ghafla kulikosababishwa  na jini alilokuwa akiishi nalo.

Jioni ya siku ile alitoroka na kwenda kuthibitisha mwenyewe kama kweli jumba lake la fahari limeungua moto. Alipofika alishuhudia hasara kubwa  iliyosababishwa na moto wa ajabu. Roho ilimuuma hakuwa na jinsi zaidi ya kurudi nyumbani.
Mwezi mmoja yalianza mazungumzo ya chini chini juu ya kuwepo pale bila msaada wowote. Kila kukicha alikuwa mtu wa mawazo juu ya maisha ya masimango. Akiwa amekaa barazani mkono shavuni, mama yake mdogo alimfuata na kumueleza:

“Jeska unaitwa na baba yako.”
Jeska bila kusema kitu alinyanyuka na kuingia ndani, alimkuta baba yake akiwa amekaa kwenye kochi.
“Kaa hapo,” Jeska bila kusema neno alikaa akiwa amejikunyata.
“Mama tumekuita tuzungumze,” baba yake alimwambia.
“Sawa baba,” alijbu kwa sauti ya chini bila kumuangalia usoni.

“Unafikiri utaendelea na  maisha haya mpaka lini?”
“Hata sijui.”
“Unasema vitu vyako vyote vimeungua?”
“Baba swali gani nimesema au kweli vimeungua!”
“Inawezekana nimekosea kusema, ila nia na madhumuni nilitaka kujua baada ya kupoteza vitu vyote una akiba gani?”

“Baba ni maswali gani hayo ya kuniuliza, kila kitu kimeungua nitabakia na akiba gani?”
“Yaani utajiri uliokuwa nao ukose hata akiba banki?”
“Huwezi kuamini, fedha iliyokuwa benki nilinunulia mzigo wote niliotumwa na wateja  ambao ungenilipa zaidi ya mara nne. Lakini kabla ya kuuza balaa limenitokea.”
“Sasa sisi tutakusaidia nini, wewe ni mtu mzima na nyumba yetu kama unavyoiona inatutosha wenyewe. Huna hata bwana wa pembeni uende ukakae.”
“Sikuwahi kuwanaye.”

“Acha uongo, si ulisema mumeo alikasirika kutokana na kutaka kuolewa na bwana mwingine. Msaada wetu umekaribia mwisho mtafute bwana yako umeombe msamaha.”
“Siwezi kuolewa na Jini.”

“Leo hii ndiyo umemjua ni Jini, kiburi chake ndicho kilichokuponza, tuna nia ya kuendelea kuwa na wewe. Lakini toka uwe hapa maisha yamekuwa magumu kiasi cha kututishia hali yetu. Jana nimeota na nyumba yetu inaungua, ndoto ya jana imenitia wasiwasi huenda na nyumba yetu itaungua kwa hiyo tulikuwa tunaomba uondoke.”

“Jamani niondoke niende wapi?”
“Hiyo haituhusu utajua pakwenda, lakini hapa hutakiwi kukaa utatusababishia matatizo.”
Kauli ile ilikuwa mkuki moyoni mkali mwa Jeska, aliona aliloelezwa na Lakashi la kutengwa na familia yake linatimia.

“Lakini wazazi wangu hamuoni kunifukuza ni kunikumbusha uchungu wa vifo vya wazazi wangu na jinsi mlivyonifukuza na kuchukua mali za wazazi wangu?”
“Sikiliza binti hatupo kukumbushana mambo yaliyopita ukitaka kujikumbusha mambo yaliyopita nenda makumbusho ya taifa.”

“Sasa mnanifukuza nitakwenda wapi?”
“Hiyo haituhusu, tulikuhifadhi kwa muda ili ujipange, lakini siku zinakatika bila kuona dalili zozote za kuondoka zaidi ya kila siku kutufanyia uchimvi wa kulialia. Ona sasa, hata hali zetu zimekuwa mbaya riziki imefunga kwa ajili yako, ndoto za kuunguliwa nyumba haziishi na mchomaji ninaye kuona ni wewe.”

“Lakini baba hizo ni ndoto hazina ukweli wowote.”
“Wewe mtoto mdogo hujui lolote, sisi tuliyewahi kuliona jua tunajua ndoto zina maana gani, hasa ndoto za kujirudia zina dalili mbaya.”
“Hivi mnanifukuza niende wapi?”

“Hiyo haituhusu, nenda kwa rafiki zako.”
“Lakini kumbukeni pamoja na kunidhulumu mali zangu bado maisha yenu yalikuwa mabaya, hata mume wangu alipowalazimisha kulipa hamkuwa na kitu na kuniomba niwaombee msamaha. Nimewaombea na mkasamehewa ikiwa pamoja na kupewa maisha mazuri. Leo nimepata tatizo mnanigeuka?”

“Jeska siku zote tenda wema uende zako usisubiri shukurani.”
“Kwa hiyo umedhamiria kunifukuza?”
“Kwa hali inayojitokeza lazima uondoke tu.”
“Lakini kumbuka maisha haya ni kwa ajili yangu.”

“Unatuchekesha, maisha haya na uliyokuwanayo nani alikuwa na maisha mazuri? Umeshindwa kumheshimu mumeo kwa upumbavu wako matokeo yake unatulaumu tusio husika.”
“Siwalaumu bali nawakumbusha jinsi gani nilivyoonesha ubinaadamu kwenu japo hamkunitendea wema.”

“Nataka nikueleze jambo moja ambalo sikupenda kukueleza mwanzo, njozi zangu za mara kwa mara za nyumba inaungua na mchomaji ni wewe zilinifanya niende kwa mtaalamu mmoja na kumuulizia njozi zile zina maana gani, baada ya kunitia wasiwasi.

“Jibu la mganga ningekuwa na moyo mdogo ningekufukuza muda mrefu, lakini ubinaadamu ndiyo uliyokufanya uwepo mpaka leo.”
“Kwa nini?” Jeska aliuliza akiwa anamtazama baba yake.
“Mganga amesema ndoto ile ni ufunuo uliombele yangu wa juu ya kitu kinachotaka kunitokea.”
“Utokewe na nini?”

“Kuota moto ukiunguza nyumba na wewe ndiye mchomaji inamaanisha nyumba yangu muda wowote itaungua moto na wewe kuonekana ndiye mchomaji inaashiria kuwa chanzo ni wewe baada ya kutoheshimu masharti uliyopewa na mumeo.

Hivyo basi kuendelea kuwepo hapa wakati tumeishajua tatizo ni nini, lazima nyumba yangu itaungua moto na sisi kuwa maskini wa kutupa.”
“Lakini kwa nini muamini njozi, sasa huyo Lakashi kama anaendelea kunifuata basi animalize kabisa,” Jeska alisema huku akilia.

“Jeska hata sisi hapa hatutumii vitu ulivyokuwa ukitumia, tuliacha pombe na nyama ya nguruwe baada ya mumeo kunionya, ili kuendelea kuwa rafiki yetu basi tuhakikishe vitu vyote asivyovipenda tusivitumie.”

“Kwani hata mimi toka nije hapa mmeniona nakunywa au kula nyama ya nguruwe.”
“Kiburi chako ndicho kilichomuudhi, kwa hiyo kwa usalama wa nyumba na mali zetu lazima uondoke si ombi bali amri.”

“Baba kama atakuja zungumza naye basi, mimi nitakwenda wapi?” Jeska alizungumza kwa sauti ya kuomba kuhurumiwa.

ITAENDELEA KESHO

No comments

Powered by Blogger.