AHADI YA NDOTONI - 11

ILIPOISHIA;
Akiwa anajifikiria kufungua mlango alishtushwa na michirizi ya damu, alitaka kukimbia lakini alijipa moyo ili ajue mwisho wa damu ile. Alipaza sauti yake tena kumwita Sadat kwa sauti ya kitetemeshi.
“Sadat upo sawa?”
Vile vile hakupata jibu lolote, kitu kilichozidisha wasiwasi. Wakati huo damu zilizokuwa zikitoka bafuni zilianza kuongezeka. Kabla ya kuusukuma mlango alijiuliza damu ile ni ya nani na Sadat yupo wapi? SASA ENDELEA...
Lakashina kwa ujasiri mkubwa aliusukuma mlango wa bafuni kuangalia kuna nini. Picha aliyoiona ndani kidogo mapigo ya moyo yasimame kwa mshtuko. Sadat alikuwa amekufa kifo kibaya sana, sehemu zake tumboni zilikuwa zimepasuka na utumbo ulining’inia nje. Macho yake na ulimi vilimtoka pima, alijikuta akipiga kelele za woga, akaanguka chini na kupoteza fahamu.
Aliposhtuka alijikuta amelala katikati ya dimbwi la damu, nguo zake zote zililoa. Alijinyanyua chini huku akitetemeka, kilichomshangaza ni muda alioanguka na aliozinduka. Alikumbuka tukio lililotokea asubuhi lakini alizinduka usiku tena wa manane.
Bafuni bado alikuwepo Sadat akiendelea kuvuja damu iliyokuwa ikiongeza dimbwi la damu sehemu aliyokuwa amelala. Alijiuliza Sadat ana damu nyingi kiasi gani ya kumtoka tangu asubuhi mpaka jioni bila kukatika? Akiwa anatetemeka alitoka mbio hadi kwenye gari lake.
Aliliondoa gari kama mwendawazimu hadi nyumbani kwake, alipofika alikimbilia bafuni kuoga. Baada ya kuoga alijiuliza kilichomtokea kama ni kweli au alikuwa akiota. Baada ya muda alipitiwa na usingizi mpaka asubuhi ya siku ya pili.
Siku hiyo ndiyo ya kusafiri kufuata biashara, aliamini kuondoka kule kungemsaidia kupunguza mawazo. Akiwa njiani kwenda uwanja wa ndege alinunua gazeti ambalo lilionesha kifo cha kutisha cha Sadat. Taarifa zilisema kifo kile kimegunduliwa na jamaa wa karibu majira ya saa tano asubuhi na mwili wake umehifadhiwa chumba cha maiti cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ikisubiri uchunguzi baada ya kifo chake kuonekana si cha kawaida.
Taarifa zile zilimchanganya sana Lakashina, alijiuliza kama mwili uligundulika saa tano asubuhi yeye alikuwa wapi, na watu waliokuja kumchukua yeye hawakumwona? Kingine kilichozidi kumchanganya ni taarifa za kuchukuliwa mwili wa marehemu na kupelekwa chumba cha maiti.
Alijiuliza kama mwili ulichukuliwa saa tano asubuhi na kupelekwa kuhifadhiwa chumba cha maiti, ule uliokuwa bafuni ukiendelea kuvuja damu ni wa nani? Muda wa kuingia ndani ya ndege ulipofika alikaa kwenye siti yake kusubiri iondoke.
Mtu mmoja aliingia ndani ya ndege akiwa amechelewa kidogo kabla mlango haujafungwa alimshtua Lakashina. Mtu yule alikuwa akifanana na Lakashi mumewe, hata harufu ndani ya ndege ilibadilika na manukato ya yule mwanaume yalitawala.
Kwake Lakashina hayakuwa mageni kutokana na kutumiwa na mumewe Lakashi, hakuwahi kuyasikia kwa kiumbe yeyote zaidi yake. Hata marashi aliyokuwa akijipaka yeye hakuwahi kuyasikia kwa mtu yeyote, hata rafiki zake walimwomba awatafutie kwa gharama yoyote.
Alimsindikiza kwa macho yule mwanaume ambaye aliamini kabisa ni Lakashi, lakini alikaa siti ya mbele yake. Aliachana na yule mtu kwa kuamini ni kiini macho kinachomtokea, lakini hakuwa na uhakika wowote kwa kile anachokiona. Aliendelea kulisoma lile gazeti kwa kupitia tena maelezo ya kifo cha Sadat, jina lilikuwa lile lile na sura ya marehemu ilikuwa ile ile. Lakini maelezo yake yalikuwa tofauti na yeye alivyoshuhudia mwili wa marehemu mpaka anatoka ndani kwa Sadat.
Taratibu sauti ya Sadat ya kuomba msamaha ilijirudia akilini mwake.
“Samahani... utaniua bure, sijamwita... kaja mwenyewe, nisamehe... nisamehe nimekoma...nakuapia sitarudia tena, kama ukiniona hata namsalimia nifanye lolote, nipo chini ya miguu yako tafadhali usiniue, aaaaaaah!”
Lakashina alijikuta akijiuliza aliyemuua ni nani na kwa nini alipomuuliza Sadat kuhusiana na sauti ya kuomba msamaha alimficha. Bado hakuamini kama kweli Sadat amekufa, aliona kama ni kiini macho cha kumtisha. Alijiuliza anayefanya vile ni nani? Kama ni mumewe anafanya ili iweje? Hakupata jibu.
Alijikuta akiapa kuwa siku akikutana na Lakashi atamweleza ukweli kuwa hataki tena kuolewa naye na alikuwa tayari kuishi maisha ya taabu kuliko maisha ya kutishana. Safari iliendelea, Lakashina akiwa katika kipindi kizito cha mambo ya ajabu yaliyokuwa yakimtokea.
Mpaka mwisho wa safari, ilikuwa tofauti. Yule mwanaume anayefanana na mumewe aliteremka akiwa katika sura ile ile. Lakashina alikuwa na hamu ya kumsogelea ili athibitishe kama kweli ni yeye. Ajabu yule mtu alipotea katika mazingira ya kutatanisha kwani alijichanganya katikati ya watu. Lakashina alikwenda hoteli aliyozoea kufikia kabla ya kuingia kwenye maduka kukusanya mali.
Alipofika kwenye hoteli, alipotaka kulipa pesa alishangaa kuambiwa na mhudumu:
“Samahani dada umelipiwa.”
“Nimelipiwa! Na nani?”
“Kuna kaka mmoja amekuja hapa na kusema utafika na kukulipia kabisa ukifika wee kaa utakavyo hata chakula cha siku utakazokaa.”
“Amejuaje mimi nafikia hoteli hii?”
“Mmh! Kwa kweli dada swali gumu.”
“Anaitwa nani?”
“Amesema anaitwa Lakashi.”
“Lakashi?” Lakashina alishtuka.
“Mbona umeshtuka, kwani humjui?”
“Sijui kama ni yeye.”
“Dada kwani jina hilo hulijui?”
“Nalijua ni la mume wangu.”
“Sasa kipi kilichokushangaza?”
“Sikutegemea kumkuta huku.”
“Kwani yeye ulimwacha wapi?”
“Dada mengine hayakuhusu nioneshe hicho chumba nikapumzike.”
“Kile kile cha siku zote.”
Lakashina alipitia mizigo yake kuelekea chumbani kwake akiwa njia panda asijue nini kipo mbele yake.
Baada ya kuoga na kupata chakula, hakuwa na muda wa kupumzika, aliingia madukani kama alivyotuma oda ya vitu. Alikuta vitu vipo tayari, alilipa pesa na kuchukua mizigo yake. Hakutaka kukaa nchini Dubai kwa muda mrefu kama alivyopanga kupumzika kutokana na mauzauza yaliyomtokea. Uwepo wa Lakashi kule ulimfanya aamue kuondoka haraka.
Akiwa kwenye moja ya maduka makubwa jiji pale, wakati akifanya manunuzi kijana mmoja wa Kiarabu ambaye alionekana si mgeni wa Afrika Mashariki kutokana na kuzungumza Kiswahili safi alimchangamkia sana Lakashina.
Kutokana na uchangamfu wake, mavazi ya heshima aliyoyavaa na jinsi alivyojiweka alimvutia yule kijana ambaye alikuwa mtoto wa tajiri mkubwa pale Dubai.
“Samahani dada umeolewa?”
“Kwa nini unaniuliza swali hilo?”
“Dada nimekuwa nikikufuatilia muda mrefu toka uanze uteja katika duka letu, umekuwa na tofauti kubwa na wanawake wengi wanaotoka Tanzania. Unajiheshimu pia ni mchangamfu, nimejikuta nikivutiwa na wewe. Mimi Naitwa Abdul Diabi ni mtoto wa mzee Diabi Mansul, tajiri wa hapa Dubai. Maduka makubwa hapa Dubai yenye bidhaa za bei nafuu ni yetu. Pia nilikuwa nina shida ya kufungua duka kubwa nchini Tanzania ambalo litakuwa likisambaza bidhaa zetu kwa bei nafuu.”
“Nimekusikia japo jibu ulilotoa halikulingana na swali langu, hebu nipe makusudio ya swali lako lililoambatana na maelezo marefu.”
“Maelezo yangu yote hayo nilitaka kwanza unifahamu kabla ya kueleza kusudio la swali langu kwako.”
“Haya sema.”
“Nimetokea kukupenda na kutaka uwe mke wangu kama hujaolewa, lakini kama umeolewa sitakuwa na jinsi zaidi ya kumsifu mumeo kuwa na mke mzuri.”
“Abdul mbona una Kiswahili kizuri kuliko Waarabu wengi niliokutana nao hapa Dubai?”
“Ni kweli, mimi ni Mswahili nimezaliwa Tanzania na kusomea Tanzania, baba yangu mzee Diabi Mansul alikuwa na wanawake wanne, watatu walikuwa Dubai na mmoja Tanzania ambaye ni mama yangu.”
“Kwa nini hamkufungua maduka Tanzania?”
“Baada ya kifo cha mama yangu, baba alituchukua na kuja kuishi huku mpaka leo, kwa kweli sasa hivi Tanzania ni mgeni kabisa.”
“Mmh! Pole sana kufiwa na mama.”
“Asante.”
“Hata mimi sina baba wala mama.”
“Ooh! Pole sana walikufa kwenye ajali au kila mtu alikufa na wakati wake?”
“Kwa ajali ya moto.”
“Pole sana, sasa nani alikulea?”
“Nimelelewa na wasamaria wema.”
“Kwa hiyo nani kwa sasa ni msimamizi wako?”
“Sina msimamizi, najiongoza mwenyewe kwa uwezo wa Mungu.”
“Inasikitisha sana, je umeolewa?”
“Mmh! Hata nashindwa nikujibu nini, naomba unipe muda nikirudi mara ya pili nitakupa jibu.”
“Subira dhahabu lakini nenda ukijua Abdul ni mgeni wa moyo wako, nipo tayari tuishi sehemu yoyote duniani.”
“Sawa nimekuelewa, nipe muda nitakupa jibu, kuwa na subira.”
“Subira ninayo ndiyo maana nilikufuatilia muda mrefu na leo nimeweza kuufungua moyo wangu kwako. Nina imani jibu langu litakuwa zuri.”
“Nipe muda, ni haraka sana kukujibu.”
“Kwa kukubali kuzungumza na mimi kwa heshima na utulivu nimeamua nusu ya mzigo ulionunua hapa nitalipa mimi,” Abdul alimpa ofa Lakashina ambayo hakuitegemea.
Baada ya makubaliano, Lakashina alirudi hotelini kwake. Alipofika mapokezi alishtuliwa na mhudumu.
“Samahani dada.”
“Bila samahani.”
“Yule kaka aliyekulipia chumba alikusubiri sana lakini alipoona unachelewa aliamua kuondoka na kurudisha funguo,” kauli ile ilimshtua sana Lakashina.
“Alirudisha funguo ina maana alikuwa chumbani kwangu?”
“Si amesema ni mumeo.”
“Sasa kama ni mume wangu kwa nini mumpe funguo bila ruhusa yangu? Meneja wa hoteli hii yuko wapi? Siwezi kufanyiwa vitu kama hivi,” Lakashina alikuja juu.
“Lakini dada si ni wewe ndiye uliyesema ni mumeo.”
“Sijamuona! Mpaka ningemuona ningejua kama mume wangu kweli.”
“Basi dada tusamehe, lakini inaonesha ni mtu mwema tena mwenye pesa, pia aliniachia chupa hii ya manukato akasema ukimaliza kula na kuoga kabla ya kujipumzisha ujipulizie.”
“Mmh! Sawa, hebu nipe.”
Lakashina aliichukua ile chupa na kwenda chumbani kwake, alipofika chumbani alikuwa na mawazo mengi juu ya Lakashi mumewe kuwepo pale huku akishindwa kuonekana mbele yake zaidi ya kuonekana kwa wahudumu wa hoteli.
Baada ya kula, alijipulizia manukato yale. Haikuchukua muda, usingizi mzito ukamchukua.
Lakashina akiwa katikati ya usingizi aliota Lakashi yupo katika merikebu moja nzuri sana ambayo hakuwahi kuiona si katika njozi wala kwenye sinema. Ilikuwa merikebu ambayo katika kumbukumbu zake aliisoma kwenye kitabu cha Alfu lela ulela (siku elfu na moja) katika utawala wa ufalme wa Harun Rashid.
Merikebu ilikuwa ya dhahabu iliyonakshiwa na fito za almasi na mapazia yake yalikuwa ya kitambaa cha hariri.
Aliiiona merikebu ile ikisogea pwani na kutia nanga, wakateremka wanawake wazuri sana wenye mavazi meupe ya kupendeza ambao walitandika zuria jekundu lililokwenda kwenye gari zuri ambalo pia hakuwahi kuliona katika maisha yake.
Alimuona Lakashi akiteremka na kwenda ndani ya lile gari ambalo liliondoka na kuingia mjini. Na mji wenyewe ulikuwa palepale Dubai, aliliona gari likitoka bandarini na kuja moja kwa moja katika hoteli aliyofikia kisha aliteremka peke yake na kuingia ndani ya hoteli. Alipofika mapokezi alimuuliza mhudumu.
“Vipi yupo?”
“Yupo.”
“Ulimpa?”
“Nilimpa, lakini alihoji wewe kuingia ndani mwake bila ruhusa yake.”
“Ndiyo alisema hivyo?”
“Ndiyo.”
“Mmh! Sawa, pole sana,” Lakashi baada ya kusema vile alitoa pochi yake na kumpatia kiasi cha pesa huku akimwambia:
“Pole kwa usumbufu niliokusababishia.”
“Asante kaka mwema,” mhudumu alipokea na kushukuru.
Lakashi aliachana naye na kwenda moja kwa moja chumbani kwake, japo mlango ulikuwa umefungwa aliingia ndani bila kuufungua na kukaa kwenye kiti pembeni ya kitanda akiwa ametulia kwa kukunja nne. Harufu kali na manukato ya Lakashi ilimuuliza pua Lakashina na kumfanya ashtuke usingizini.
Alipoangalia kwenye kochi alimuona Lakashi akiwa amekaa kwenye mavazi yale yale aliyoyaota.
“Asalamu aleykum,” Lakashina alimsalimia huku akipepesa macho na kukaa kitako.
“Waleykum saalam.”
“Karibu.”
“Asante.”
“Za siku?”
“Nzuri.”
“Vipi umerudi rasmi?”
“Bado.”
“Japo nimekuona ndotoni wakati ukija mpaka kuingia ndani, siamini kukuona katika macho makavu kabla ya kurudi rasmi.”
“Nimerudi mara moja kwa ajili yako kisha nitaondoka, nadhani huenda nisirudi tena.”
“Kwa nini mume wangu?”
“Lakashina umeolewa?” Lakashi alimuuliza Lakashina.
“Na nani?”
“Mbona unaniita mimi mumeo wakati humjui aliyekuoa?”
“Sikukuelewa, nimeolewa na wewe.”
“Kweli unakiri toka moyoni mimi ni mumeo?”
“Ndiyo.”
“Si kweli, kilichonileta hapa ni kimoja wala sitahitaji malumbano ila kutimiza dhamira yako iliyokusumbua muda mrefu kiasi cha kukunyima raha.”
“Dhamira gani tena hiyo mume wangu?”
“Lakashina huna fadhila, yote niliyokufanyia imekuwa bure.”
“Lakashi nimefanya kosa gani?”
“Mengi sana, imefikia hatua ya kunipatisha dhambi ili tu ujue mimi nipo lakini nilikuwa natwanga maji kwenye kinu. Leo nimekuja kukufanyia kile ulichokitaka, siwezi kuwa adui wa Mungu kila kukicha.”
“Kweli niliamua kukukana kutokana na kuishi maisha ya vitisho kila kukicha.”
“Ni vitisho gani zaidi ya kukupa muongozo mzuri wa maisha yako?”
“Kwa hiyo unaamua nini?”
Lakashina alimuuliza huku akiwa tayari kwa uamuzi wowote, na alipenda siku ile waachane kabisa, kwani alitamani kuishi maisha ya kidunia. Kabla hajaendelea adhana ya magharibi ilisikika, ikabidi Lakashi asogee pembeni kuswali magharibi, aliswali mpaka kumaliza Lakashina akiwa amekaa kitandani.
Baada ya kumaliza kuswali alirudi kwenye kochi na kumuuliza Lakashina:
“Mbona huswali?”
“Sina udhu,” alijibu kwa mkato.
“Una muda gani hujaswali?”
“Hata sikumbuki.”
“Mmh! Umekuwa mbuzi usiyekumbuka ulipotoka?”
“Wewe fanya kile kilichokuleta, sihitaji vitu vingine visivyonihusu, kwanza dini yenyewe ngumu sina uhuru wa maisha.”
“Mmh! Kweli eeh!”
“Habari ndiyo hiyo, sema tu kila bwana anayenifuata ni Mwislam, bila hivyo ningerudia jina langu la Jeska.”
“Asante, nipe pete yangu,” Lakashina alinyoosha mkono kuomba pete yake.
Lakashina bila kusita aliivua pete ya ndoa na kumkabidhi Lakashi, aliipokea na kusema:
“Asante, kuanzia leo upo huru kuolewa...
Lakashina baada ya kuivua pete nini hatma ya maisha yake? Usikose siku ya kesho!
Like: www.facebook.com/2jiachie
Web: www.2jiachie.com
Post a Comment