ad

ad

She is too young to die (Ni mdogo mno kufa) -1



Jengo refu la ghorofa  tano  lililojengwa kwa vioo tupu lilisimama katikati ya jiji la Dar es Salaam mtaa wa Samora karibu kabisa na mnara wa askari, lilikuwa miongoni mwa majengo mapya yaliyojengwa katika miaka  ya elfu mbili. Chini yake kulikuwa na benki  ya Diamond Trust lakini kwa juu jengo hilo lilikuwa na  maandishi makubwa ya kung’ara yaliyoandikwa WorldCom Tower, yaliyoonyesha kabisa kwamba jengo hilo halikuwa mali ya Diamond Trust bali walikuwa ni wapangaji tu.  Pembeni mwa benki hiyo kulikuwa na  duka kubwa   ambalo kwenye vioo vyake kulipangwa kompyuta nyingi na mlangoni  mwa duka hilo paliandikwa WorldCom computers Ltd, mlinzi aliyevaa magwanda ya  rangi ya kijivu na kofia nyekundu akiwa ameshikilia bunduki mkononi alisimama  kwa ukakamavu akishuhudia gari  aina ya  Rangrover vogue likiegesha taratibu mbele ya jengo hilo.

Kijana mwembamba mrefu  aliyevaa suti nyeusi, shati jeupe lenye mistari na tai nyekundu alishuka akiwa amebeba kisanduku kidogo na kuanza kutembea akielekea kwenye mlango wa duka la WorldCom, askari alizidi kukakamaa kadri kijana huyo alivyousogelea mlango na baadaye kupiga saluti  kuonyesha heshima.

“Shikamoo bosi!” alimwamkia kijana huyo ingawa alikuwa na uhakika kabisa kwamba kwa umri alikuwa mdogo.

“Mambo?”

“Poa”

“Haya kazi njema!” alisema kijana huyo akipokelewa kisanduku chake na msichana mrembo kisha kutembea akipita mlango uliokuwepo mbele yake hadi kwenye lifti,  wote wakapanda na msichana huyo akabonyeza namba tano, lifti ikaanza kupanda taratibu mpaka ghorofa ya  tano,  wote wakashuka na kuingia kwenye mlango wa kung’ara uliondikwa mlangoni WorldCom Computers Ltd,  mlango ulifunguka wenyewe kabla hawajaugusa na wakaingia ndani.

“Shikamoo bosi” msichana nyuma ya kompyuta aliyeonekana kuwa  Katibu Mhutasi wa kijana huyo  alimwamkia.

“Marahaba hujambo Tecla?”

“Sijambo, habari za nyumbani?”

“Salama!”

“Wifi?”

“Bado hajarudi bwana,  halafu nina wasiwasi kweli maana tarehe zake za kujifungua ndio zinakaribia kabisa!”

“Mara ya mwisho mmewasiliana lini?”

“Wiki iliyopita na nikamwambia arejee haraka,  unajua huko kwao ni kijijini sana halafu barabara si nzuri,  masika ikimkuta huko itakuwa ni kazi ngumu sana kutoka! Wala hakuna simu kutoka Mwanza?”

“Kwa kweli sijapokea bosi!”

“Wacha  nijaribu kumtafuta!” aliongea na kuingia ofisini kwake, mlangoni akipishana na Katibu wake binafsi aliyekuwa ametanguliza kisanduku. Kitu cha  kwanza alichokifanya baada ya kuketi ni kujaribu kupiga simu  Mwanza kwa dada yake kuuliza kama  mkewe alikuwa amefika.

“Bado! Halafu mvua zinanyesha  kweli,  nasikia barabara hazipitiki kabisa kwenda huko kwao Kahunda, madaraja yamevunjika!”

“Mungu wangu! Sasa tutafanyaje?”

“Yaani sifahamu na hakuna simu kabisa kule”

“Duh!”

Alikuwa ni Gilbert Mushi, kijana wa Kichaga aliyepata mafanikio makubwa sana kwa biashara ya kompyuta mara baada ya kurejea nchini akitokea Marekani alipokwenda  kusomea digrii ya pili katika masuala hayo na kuanzisha kampuni ya  WorldCom computers. Yeye ndiye alikuwa mtu wa kwanza kusaini mkataba wa kusambaza kompyuta za kampuni ya Microsoft katika nchi za Afrika ya  Mashariki,  akiwa na  ofisi  nchini Uganda,  Kenya lakini makao makuu yakiwa Dar es Salaam kwenye jengo lake la WorldCom Towers.

Miaka miwili tu baada ya kuanzisha kampuni hiyo,  alimuoa  binti aitwaye Salome Mafuru  mwenyeji wa wilaya ya Sengerema,  kijiji cha Kasheka,   kata ya  Mwangika tarafa ya Nyehunge. Wawili hao walikutana wakisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupendana, hivyo Gilbert aliporejea tu kutoka Marekani,  waliamua kuitimiza ndoto yao ya kufunga ndoa  na kuanza kuishi na kufanya kazi pamoja. Kwa muda wa miaka mitatu waliishi bila  kuwa na mtoto,  ndoto waliyotamani sana itokee! Lakini mwaka wa nne Mungu akawabariki,  Salome akawa mjamzito na furaha ikaongezeka katika maisha yao wakimsubiri kwa hamu mtoto  ambaye angezaliwa.

Tangu wafunge ndoa, Salome hakuwahi hata mara moja kupata nafasi ya kwenda kijijini kwao kusalimia lakini Krismasi ya mwaka 1998,  alitamani kula na wazazi wake akamwomba mume wake ruhusa ya kufanya hivyo na Gilbert hakuwa na kizuizi, akamruhusu lakini akimtaka arejee haraka Dar es Salaam kwa ajili ya kujifungua kwani ujauzito wake ulikuwa tayari na miezi minane.

“Hukutakiwa kusafiri lakini nakuruhusu kwa sababu umeng’ang’ania sana,  hali yako kwa hivi sasa ilikuwa inakuhitaji upumzike!”

“Usiwe na wasiwasi G, nitarejea salama  tu,  acha nikamwone mama ili nipate  na baraka zake siku ya kujifungua!” Salome aliongea  akitabasamu.

***

Kazi hazikufanyika siku hiyo, Gilbert alikuwa amebadilika kabisa,  taarifa kuwa madaraja yalikuwa yamevunjika kueleka kijijini kwao na Salome zilimchanganya kabisa hasa kwa sababu hapakuwa na mawasiliano hata kidogo kujua walikuwa wakiendeleaje! Alijaribu kumshawishi dada yake aende kijijini kuangalia lakini alikataa baada ya kusikia kulikuwa na mafuriko,  Gilber akalia.

“Nasubiri mpaka jioni,  ikishindikana  kupata taarifa yoyote nakodisha helkopta itakayonipeleka mpaka huko”

“Bora ufanye hivyo”

“Sawa dada”

Nusu saa baadaye katibu mhutasi wake alipiga simu na kumtaarifu kulikuwa na mtu kutoka kituo cha polisi cha kati aliyetaka kumwona,  Gilbert akakataa kabisa kwamba kwa muda huo hakuhitaji kuonana na mtu yeyote isipokuwa kumfikiria mke wake. Ndipo Katibu wake akamwelewesha kwamba  mtu aliyetaka kumwona alidai kuwa na taarifa za mkewe.

“Kweli? Mwambie aingie haraka” alisema na sekunde chache baadaye mlango ukafunguliwa,  akaingia  askari  mfupi aliyevaa magwanda na kuketi mbele ya meza yake.

“Habari yako bwana Gilbert?” alisalimia askari huyo.

“Sio nzuri!”

“Kweli si nzuri”

“Kwanini?”

“Nina habari za kusikitisha!”

Je, nini kitaendelea?

No comments

Powered by Blogger.