She is too young to die- 5
Mke wa kijana mwenye mafanikio,
Salome ambaye ni mjamzito amekwama kijijini kwao sababu ya mafuriko! Damu nyingi zinamtoka na
amepoteza fahamu, mume wake ameamua
kukodisha helkopta kutoka Dar es Salaam hadi kijijini kwao Kahunda lakini
anamkuta amekwishaondoka kwa Landrover ambayo pia anataarifiwa imeshindwa
kuvuka mto sababu daraja limevunjika. Je, atafanikiwa kumpata na kumwokoa?
SONGA NAYO…
Gilbert hakuweza hata kusubiri mazishi
ya mkwe wake mzee Magoma, alichoomba ni
kuonyeshwa mwili wa marehemu ili atoe
heshima zake za mwisho kwa sababu mzee huyo alipoteza uhai wake kwa ajili ya mke wake, wanakijiji
wakamfanyia kama alivyoomba na baada ya hapo akiongozana na mzee Mchele walitembea tena mpaka kijiji
cha Bupandwamhela shuleni walikoiacha
helkopta, wakakuta wanakijiji wengi zaidi
wamekusanyika kuishangaa! Gilbert akamsimulia Rubani juu ya yote
aliyoyakuta kijijini na kumwomba waruke
mpaka eneo ambalo mke wake alidaiwa
kuwepo, hakuwa na uhakika kama angemkuta hai lakini angalau afanye jambo Fulani, wakati akiongea
machozi yalimtoka Gilbert kama mtoto mdogo, ndani ya moyo alijihukumu kwa
kumruhusu Salome kuja maeneo hayo wakati alikuwa mjamzito.
“Lakini sikujua…hata yeye
aling’ang’ania sana kumbe ndio kifo kilikuwa kinamwita!” Aliwaza moyoni mwake
akipanda ndani ya helkopta pamoja na mzee Mchele aliyejitolea kuwaelekeza
mahali daraja lilipokuwa.
Wakaruka juu kama mita mia
tano hivi na kuanza kuelekea mbele wakipita juu ya vijiji vya Bupandwa, Kafunzo
macho yao yakiwa yameangalia chini,
mzee Mchele akiwaelekeza na hatimaye wakafika kwenye mto wenye daraja lililovunjika, hapo
ndipo wakaiona gari aina ya Landrover
ikiwa imeegesha barabarani hatua chache
tu kutoka kwenye mto uliopita maji mengi. Upande wa pili pia kulikuwa na magari
mengi yaliyokuwa yameshindwa kuvuka mto.
“Nafikiri ni wale!” mwalimu Mchele
aliongea.
“Hapo ndio kwenye daraja?”
“Hapa ndio Bilulumo, daraja limekwenda
na maji!”
“Sasa?” rubani aliuliza.
“Anza kushuka, tutamchukuaje kama kweli hiyo ndiyo gari
yenyewe maana hakuna sehemu ya kutua?”
“Tutatumia kamba, nitakufunga wewe
halafu utashuka hadi chini ambako
utambeba kisha nitakuvuta tena kuja juu kwa kutumia mashine, sawa?”
“Hakuna shida!”
“Haya sogea hapa karibu!” rubanin alisema na Gilbert akatii kisha kumwelekeza mahali
kulikokuwa na kamba, akamwamuru aifunge
kiunoni na kumwelekeza namna ya kushuka
na kuteremka hadi chini, baada ya hapo alianza kuiteremsha helkopta chini mpaka
umbali wa kama mita mia kutoka ardhini.
“Ni mwenyewe, ni mke wangu! Amelala
ndani ya gari, anaonekana amekufa…!”
“Jikaze Gilbert, shuka sasa!” Rubani
alisema baada ya mlango kufunguka na Gilbert akaruka na kuanza kushushwa kwa
kamba hadi chini ambako aliingia ndani ya Landrover na kumkuta mama mkwe wake
amelala kando ya Salome, akamwamsha na kumwamkia huku akimgusa Salome kifuani,
moyo ulikuwa bado unapiga ingawa alikuwa amelala katikati ya mabonge ya damu.
“Pole mama!”
“Ahsante!”
“Tunaondoka naye kwenda hospitali!”
“Hakuna shida baba! Mimi?”
“Wacha kwanza nimpandishe yeye, halafu nikifika juu nitaongea na Rubani!”
Gilbert alichukua mkanda aliopewa na
Rubani, akajifunga kifuani na pia kuufunga kifuani kwa mkewe ukipita chini
ya kwapa zake, alipomaliza alionyesha
ishara juu na mkanda ukaanza kumvuta taratibu mpaka ndani ya helkopta ambako
alifungua mkanda na kumlaza mke wake chini.
“Salome!Salome!Salome!” akaita
mara nyingi bila kuitikiwa.
“Tuondoke?” Rubani aliuliza.
“Mama mke wangu pia anataka kuondoka na
sisi!”
“Haya shusha kamba!”
Gilbert akafanya hivyo kisha kushuka
hadi chini ambako alimkuta mama yake Salome akimsubiri, akauchukua mkanda tayari kujifunga pamoja na
mama mkwe wake, ghafla alimwona mama mkwe akishtuka na kurudi nyuma. Gilbert
akashindwa kuelewa ni kitu gani kilikuwa kimetokea.
“Vipi mama?”
“Baba wewe ni mkwe wangu tukumbatiane?”
“Mama tuko kwenye hali ya hatari!”
“Mh! Ni mwiko!”
Je, nini kiliendelea? Fuatilia

Post a Comment