UKAWA WAMJIBU KIKWETE
SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) warudi bungeni akidai hawana sababu ya kwenda kushitaki kwa wananchi kwa sababu watawacheka na kuwasikitikia, umoja huo umemjibu wakisema wapo tayari kuchekwa.
Akihutubia
vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi, siku moja kabla ya sherehe za
miaka 50 ya muungano, Rais Kikwete alisema kuwa huko nje wanakotaka
kwenda UKAWA siko na siku yake sio sasa, hivyo akawaomba wasipoteze
fursa hiyo muhimu ya kutoa mawazo yao bungeni ili yafanyiwe kazi.
Alisema wananchi hawahusiki wala hawana namna ya kuwasaidia kwani mengi ya hayo yanayowakasirisha ni matatizo waliyoyazusha wao.
Mwenyekiti wa UKAWA, Freeman Mbowe, aliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa
kama Kikwete anafikiri kwamba watarudi bungeni kwenye mijadala ya
dharau, ubaguzi na matusi inayofanywa na wajumbe wa CCM, basi hajui
chimbuko la tatizo.
"Kadiri
anavyoendelea kuliacha Bunge liendelee na mijadala ya kibaguzi na
matusi, taifa linazidi kupasuka na washauri wake hawamwelezi tatizo
hilo," alisema.
Mbowe
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
alisema kuwa Rais Kikwete asipokuwa makini atalitumbukiza taifa kwenye
machafuko ingawa yeye anafanya utani kwa kuipasua nchi na kushangilia
kauli za kibaguzi, kejeli na matusi zinazotolewa na baadhi ya wajumbe wa
CCM.
"Rais na
wasaidizi wake inaelekea hawajasikiliza hata kauli zinazotolewa na
viongozi wa dini kuhusu rasimu ya Warioba, atuache twende kwa wananchi,
wao ndio wataamua. Tumevumilia kwa kiwango fulani, lakini itafika mahali
uvumilivu utaisha, kwani hatuwezi kuendelea kuzuiliwa kufanya mikutano
na jeshi la polisi wakati mikutano ya CCM inafanyika kote nchini
kutuchafua," alisema Mbowe.
CHANZO: TANZANIA DAIMA

Post a Comment