Manji azuia mamilioni ya Okwi
Mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi.
Na Lucy MginaMWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji, ameonyesha ukomavu katika uongozi wa soka baada ya kukataa wachezaji wake kuuzwa katika kipindi timu yao inapambana kutetea ubingwa wa Tanzania Bara.
Manji amekataa kuuzwa kwa Emmanuel Okwi kwa Klabu ya Al Ain ya Abu Dhabi ambayo ilikuwa tayari kutoa kitita cha dola 500,000 (Sh milioni 818) kwa kuwa si wakati mwafaka.
Lakini akasisitiza hata Nadir Haroub ‘Cannavaro’ hawezi kuondoka wakati Yanga ikiwa inapambana katika wakati mgumu.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga kimeeleza, Manji amesisitiza kuwa kama mchezaji anauzwa, lazima kuwe na uhakika wa yule atakayeziba pengo lake kama yuko ndani ya timu au atakayenunuliwa.
“Unajua wale jamaa hawakuwa wamekuja official (kiofisi) kabisa Yanga kumtaka Okwi, lakini taarifa zilishaufikia uongozi na mwisho mwenyekiti alisikia.
“Baada ya hapo akasisitiza hakutakuwa na mchezaji atakayeondoka katika kipindi Yanga inapambana kuwania ubingwa. Badala yake akataka kuwe na utaratibu mzuri wa kuwauza wachezaji na si kuangalia fedha tu,” kilieleza chanzo.
“Lakini kuhusu Cannavaro, pia amesema huu si wakati mzuri na tuna mechi muhimu za kumaliza ligi, hivyo tufanye mambo kitaalamu.”
Al Ain ambayo anachezea Asamoah Gyan, raia wa Ghana, imeonyesha kuvutiwa na Okwi tangu akiwa Etoile du Sahel ya Tunisia, lakini ikawa inachanganywa na mgogoro wake.
Al Ahly yenyewe ilivutiwa na Cannavaro wakati Yanga ilipocheza nayo mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika na nahodha huyo wa Yanga akafunga mechi zote mbili.
Championi Jumamosi lilifanya juhudi za kumsaka Manji na kupata ufafanuzi kuhusiana na suala hilo la kuzuia wachezaji kuuzwa.
“Si kuzuia kwa nia mbaya, lakini Yanga inapouza wachezaji lazima iwe na uhakika kama ina muda wa kuwaongeza na nani anaongezwa. Huwezi kuuza mchezaji halafu wewe ukabaki dhaifu, si sahihi,” alisema kwa ufupi na kusisitiza viongozi wengi, hasa watendaji, wanaweza kulizungumzia.
Msimu uliopita, Simba ilimuuza Okwi ‘bure’ kwa Etoile du Sahel wakati ikiwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, hali iliyosababisha kuzorotesha kikosi hicho ambacho kilitolewa kwa aibu ya kufungwa jumla ya mabao 6-1 baada ya kufunga bao 1-0 jijini Dar na 5-1 ugenini Angola.
CHANZO NI CHAMPIONI JUMAMOSI
Post a Comment