Matajiri wanunua mabao ya Yanga
WANACHAMA wa Yanga Family wameahidi kununua kila bao
litakalofungwa kwenye mechi ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika
dhidi ya Al Ahly itakayopigwa Jumamosi ya wiki hii katika Uwanja wa
Taifa jijini Dar.
Yanga ilifanikiwa kuingia raundi ya kwanza ya michuano hiyo baada ya kuitoa Komorozine ya Comoro kwa jumla ya mabao 12-2.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo kilisema kuwa kundi
la Yanga Family limejipanga kuhakikisha linanunua mabao watakayofunga
katika mchezo huo ili kuongeza ari kwa wachezaji watakapokuwa wakipigana
uwanjani.
Ripoti hizo zinasema zaidi kwamba licha ya kutambua mechi hiyo
itakuwa ngumu kwa upande wao, wameamua kutumia njia hiyo kama sehemu ya
kuwashawishi wachezaji wacheze kwa nguvu na morali kubwa ili wavunje
rekodi ya kuwaondoa Waarabu hao mapema kwenye michuano hiyo mikubwa
Afrika kwa ngazi ya klabu.
Mbali na ahadi kutoka kwa wanachama hao, uongozi umejipanga
kuhakikisha unawapa zawadi kubwa iwapo wataibuka na ushindi kwenye ardhi
ya Tanzania.
“Suala la ahadi hakuna tatizo kwa kuwa kamati husika
zimejipanga na kila kitu kipo sawa, vikao vya kuijadili mechi hiyo
vinaendelea kila siku, lengo ni kutaka kufanya vizuri.
“Tayari Yanga Family wameahidi kununua kila bao watakalofunga,
lakini uongozi wa juu haujataka kusema utakachotoa kwa kuwa wanaona kama
watawaharibu kisaikolojia wachezaji japokuwa zawadi ipo tena kubwa
tu!,” kilisema chanzo hicho.
Post a Comment