ad

ad

NCHAMBI ATAKA MAWAZIRI MIZIGO WATOSWE

MBUNGE wa Kishapu, Suleiman Nchambi, ameungana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, kumtaka Rais Jakaya Kikwete awatimue mawaziri mizigo ambao wameshindwa kutimiza majukumu yao.

Nchambi (CCM), alisema anakusudia kwenda kumuona Rais Jakaya Kikwete kulalamikia uzembe wa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, kwa jinsi alivyoshindwa kutatua kero ya wakulima katika jimbo  la Kishapu.

Mawaziri wengine wanaolalamikiwa na kupendekezwa watimuliwe, wamo Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.

“Mimi naungana na Nape na Kinana kwamba Chiza hafai, hajatembelea maeneo ya kilimo, wizara haitendi haki na kama ni mzalendo anapaswa kujiuzulu mwenyewe maana kama nguo hazikutoshi, vua mwenyewe,” alisema Nchambi.

Alisema amewahi kumuomba Waziri Chiza aende Kishapu akashuhudie na kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya wakulima, lakini hadi leo hajafika.

Alisema katani na pamba inayozalishwa Kishapu ni bora zaidi kuliko sehemu yoyote nchini, lakini wakulima hao hawajafikiwa na wizara katika kuwajengea uwezo wa kuzalisha zaidi ili wanufaike na kilimo chao.

“Baadhi ya kata za jimbo la Kishapu   zina maji ya kutosha na unahitaji utaalamu; huhitaji kuchimba ni kuzuia tu, waziri hayupo! Ni bora mawaziri hao watoke wenyewe,” alisema.

Mbunge huyo alimshambulia Waziri Chiza na Naibu wake kwa tabia zao za kutaka kukaa ofisini Dodoma na Dar es Salaam badala yake waende mikoani kuonana na wakulima.
Mbunge huyo alimpongeza Waziri John Magufuri kwamba anapaswa kuwa mfano wa kuigwa na mawaziri wengine kutokana na staili yake ya uchapaji kazi.
Powered by Blogger.