NCHIMBI ABEBESHWA ZIGO LA PROF KAPUYA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi ameingia lawamani kwa
kudaiwa kumlinda Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM),
anayedaiwa kumbaka na kumtishia kumuua binti wa miaka 16.
Akizungumza kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi wa simu (sms) na
Tanzania Daima jana, binti anayelalamika kutishiwa maisha na Profesa
Kapuya, amemtuhumu Waziri Nchimbi kushindwa kulishughulikia suala hilo
mapema licha ya kuwa na taarifa za tukio hilo muda mrefu.
Binti huyo alisema kuwa Dk. Nchimbi ni miongoni mwa mawaziri na
viongozi wa CCM waliokuwa wakifahamu kila kinachoendelea dhidi ya
malalamiko husika.
Alibainisha kuwa makada hao wa CCM walikuwa wakifanya jitihada za
kuhakikisha manyanyaso na vitisho kutoka kwa Profesa Kapuya haviwekwi
hadharani.
Katika kile kinachoonekana ni kukata tamaa juu ya usalama wake pamoja
na dada yake, binti huyo alisema amewasiliana na Waziri Nchimbi asubuhi
ya jana na kwamba waziri huyo hakuonyesha dalili yoyote ya kujali
madhila yao.
Alisema kutokana na Waziri Nchimbi kutokutilia uzito malalamiko yao,
waliamua kumuandikia ujumbe mfupi wa maandishi wakimshutumu kuendelea
kumlinda Profesa Kapuya.
“Nimemwambia katika ujumbe mfupi wa maneno (sms) kuwa jukumu la
polisi iliyo chini ya wizara yake ni kuhakikisha wananchi wanalindwa
dhidi ya manyanyaso na vitisho vya aina yoyote, na kwamba katika kadhia
hii ya Kapuya Jeshi la Polisi limekuwa kimya.
“Matukio mbalimbali ya kihalifu yenye kutatanisha yametokea nchini,
lakini serikali inasema haiwajui wahusika na kwamba hata hili la
kutishiwa maisha pia serikali inasubiri nife,” alisema binti huyo.
Binti huyo alisema katika ujumbe huo aliomtumia Waziri Nchimbi, pia
amemdokezea kuwa haogopi kitakachompata ilimradi yupo katika msitari wa
kutafuta haki yake.
Amedai kuwa hivi sasa bado kuna jitihada kubwa za watu walio karibu na Kapuya kuwataka waachane na suala hilo.
“Juzi mtu aliye karibu na Kapuya ametuhoji tunataka nini ili tuachane
na jambo hili… sisi tumemjibu tunataka haki si kingine chochote,”
alisema.
Jitihada za Tanzania Daima kumpata Waziri Nchimbi ziligonga mwamba
baada ya simu yake ya mkononi kuita bila majibu na hata alipotumiwa
ujumbe mfupi wa maneno (sms) haukujibiwa.
Wanaharakati walia na polisi
Wakati sakata hilo la Kapuya likiwa kwenye hali ya kutoeleweka,
baadhi ya wanaharakati na watetezi wa masuala ya jinsia wamelitaja Jeshi
la Polisi kwa kuchangia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya
Siku ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwenye viwanja vya Mtandao wa Jinsia
(TGNP).
Joseph Mathias, alisema vitendo hivyo vya ukatili vinaongezeka
kutokana na polisi kuwalea na kuwalinda baadhi ya vigogo wanaovitenda.
Bila kumtaja jina, Mathias alisema hivi karibuni kiongozi mmoja
anahusishwa na ubakaji na kutishia kuua, lakini hadi sasa hajafikishwa
mahakamani.
Mathias, alisema pamoja na dawati la kupinga ukatili wa kijinsia
kupata taarifa hiyo, lakini hadi leo halijamchukulia hatua yoyote ile
kama inavyofanya kwa watu wengine waliofanya makosa kama hayo.
Aliongeza kuwa polisi bado ni tatizo katika mapambano hayo, na kama
hawatabadilika kiutendaji kuna uwezekano tatizo hilo likazidi kushamiri.
“Kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria watu kama hawa, kumekuwa
chanzo cha baadhi ya watu kuyachukulia matendo haya ya ukatili wa
kijinsia kuwa ni haki yao,” alisema Mathias.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TGNP, Anna Sangai, alisema changamoto kubwa inayochangia vitendo hivyo katika jamii ni mila potofu.
“Sisi TGNP tunalichukulia kuwa ni la kirasilimali, hivyo tunaishauri
serikali ijaribu kutenga fedha za kutosha na kuzielekeza kwenye Wizara
za Mambo ya Ndani ya Nchi na Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ili
zifikishe elimu bila vikwazo kwa jamii,” alisema.
Anna alisema endapo jamii itapatiwa elimu kuhusu ukatili huo, anaamini kuwa vitendo hivyo kwa kiasi kikubwa vitapungua.
Aidha, jamii nayo imetakiwa kuondokana na mila potofu kwa kuwaona
wanawake si lolote katika kuchangia masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
Mwakilishi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Judith
Kizenga, alisema serikali imejipanga kukamilisha sheria zote ambazo
zitaweza kupambana na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika
jamii.
Kuruthumu Mikidadi, ambaye ni mwakilishi Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi, alikiri
kuwa dawati la jinsia linakabiliwa na changamoto
mbalimbali, lakini hali hiyo inatokana na uchanga wake.
Awali kwa nyakati tofauti, washiriki zaidi ya wanne kutoka mikoa ya
Mbeya, Morogoro na Dar es Salaam, walilishambulia dawati hilo kuwa
watendaji wake wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na kushindwa
kutoa haki.
Walisema wakati mwingine mhalifu anamfikishwa kwenye dawati hilo,
lakini cha kushangaza kesho unamkuta ameachiwa katika mazingira tata.
CREDIT TANZANIA DAIMA

Post a Comment