Matuta yaizamisha Kili Stars
TIMU ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars imeikosa nafasi ya tatu katika Michuano ya Chalenji iliyomalizika jana nchini Kenya, baada ya kufungwa na Zambia kwa mikwaju ya penalti 6-5.
Katika mchezo huo uliopigwa majira ya saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, dakika 90 zilimalizika kwa timu hizo kufungana bao 1-1, ambapo penalti iliyopigwa na nahodha wa Stars, Kelvin Yondani iliota mbawa na kuipa ushindi Zambia.
Zambia ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 52 kupitia kwa kiungo mshambuliaji, Ronald Kampamba.
Katika dakika ya 60, Kocha Mkuu wa Stars, Kim Poulsen alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Hassani Dilunga na Athumani Idd ‘Chuji’ na kuwaingiza Ramadhani Singano ‘Messi’ na Haruna Chanongo.
Kuingia kwa wachezaji hao kulibadilisha mchezo wa Stars ambao walianza kulishambulia goli la wapinzani wao na dakika 64 mshambuliaji wa kimataifa wa TP Mazembe ya DR Congo, Mbwana Samatta, akaisawazishia Stars.
Waliofunga penalti za Stars ni Samatta, Erasto Nyoni, Himid Mao, Amri Kiemba na Singano huku waliokosa ni Chanongo, Mrisho Ngassa na Yondani.
Mpaka gazeti hili linaelekea mitamboni, mechi ya fainali ilikuwa ikiendelea kati ya Kenya dhidi ya Sudan.

Post a Comment