ad

ad

Kiiza, Kavumbagu wamng’oa Kaseja •Yanga yamnasa Javu wa Mtibwa.

WAKATI wengi wakijiuliza sababu za kuachwa kwa kipa namba moja wa Simba, Juma Kaseja kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, habari kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema kisa ni kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Yanga katika mechi ya kufunga pazia la Ligi Kuu iliyochezwa Mei 18.
Kaseja akiwa langoni katika mechi hiyo iliyochezeshwa na Martin Saanya, mabao ya Yanga yalifungwa na Didier Kavumbagu dakika ya tano na Hamis Kiiza dakika ya 62.

Habari za kuaminika toka ndani ya uongozi wa Simba zinaeleza kuwa kipigo hicho kiliwakera viongozi wa klabu hiyo kukiwa na madai kuwa kilitokana na uzembe au makusudi.

Kiongozi mmoja wa Simba alisema kwamba pamoja na upungufu mwengine ambao kipa huyo amekuwa akihusishwa nao, mazingira ya mabao mawili dhidi ya Yanga, ndiyo yamemwondoa Msimbazi.

“Hivi unavyomfahamu wewe Kaseja anaweza kufungwa mabao kama yale? Kwa kweli hilo limetuacha na maswali mengi kichwani, imetukera sana, mwache aende zake,” alisema.

Akienda mbali zaidi, kiongozi huyo alisema ingekuwa vizuri zaidi kama Kaseja angeweza kuonesha umahiri wake na kuondoa dhana mbovu dhidi yake, lakini kitendo cha kukubali nyavu zake kutikiswa kilitoa jawabu juu ya maswali waliyokuwa nayo.

Siku za karibuni kumekuwa na utata juu ya Kaseja kubaki Msimbazi baada ya mkataba wake kufikia mwisho huku akizua mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Usajili kwa wengine kutaka asajiliwe na wengine wakitaka aachwe.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa klabu hiyo Alhaj Ismail Aden Rage, Kaimu Makamu Joseph Itang’are ‘Kinesi’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zakaria Hanspoppe, kwa nyakati tofauti walisema Kaseja hawezi kuongezewa mkataba.

Viongozi hao walitoa kauli hizo bila ya kueleza wazi sababu za kumuacha kipa huyo namba moja wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambaye ameitumikia klabu hiyo karibu miaka 10.
Hayo yakiendelea, Kaseja mwenyewe ameendelea kuwa kimya kwani katikati ya wiki alitafutwa na mwandishi wa habari hizi na hakuwa tayari kusema lolote, ingawa kuna habari kuwa huenda akatua Coastal Union ya Tanga au Mtibwa Sugar ya Turiani.

Aidha, Yanga imemnasa mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Husssein Javu ambaye pia alikuwa akiwaniwa na Simba.

Habari kutoka Yanga, zinasema nyota huyo amesaini mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuitumikia klabu hiyo.

Aidha, Yanga pia imemnyakua kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ ambaye anafanya timu hiyo kuwa na makipa watatu; Ali Mustafa ‘Barthez’ na Yusuf Abdallah ambaye amepandishwa toka timu ya Vijana ya Yanga.
Imeelezwa kwamba, Yanga imeamua kufuta mpango wa kumuongeza mkataba kipa wa kimataifa, Mghana Yaw Berko baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Ernie Brandts kumkataa
Powered by Blogger.