Dk. Slaa ambana JK • Amtaka aeleze trilioni 1.7/- zilivyotumika, Lema awasha moto.
WAKATI serikali ikishindwa kutoa maelezo ya namna fedha
zilizotolewa na serikali na kuidhinishwa na Bunge kwa ajili ya kuhuisha
uchumi (Stimulus Package) sh trilioni 1.7 zilivyotumika, Katibu Mkuu wa
CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa amefufua kadhia hiyo, sasa akimtaka Rais
Jakaya Kikwete kuwaeleza Watanzania fedha hizo ziko wapi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara jana katika Kiwanja cha Kwaraa,
Babati mjini katika siku ya kwanza ya ziara yake kutembelea maeneo
mbalimbali ya wilaya zote za Mkoa wa Manyara, Dk. Slaa alisema serikali
haijawahi kutoa majibu sahihi juu ya namna fedha hizo za wananchi
zilivyotumika.
Alisema taarifa kutoka ndani ya serikali zinadai kuwa fedha hizo ziliwanufaisha watu wa karibu na Rais Kikwete.
Slaa alisema katika ukaguzi wa fedha za serikali, taarifa muhimu
zilizotakiwa zilifichwa, huku Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG)
akishindwa kupata hesabu za matumizi ya sh bilioni 48 zilivyotumika.
Aliongeza kuwa fedha hizo zingetumika kwa ajili ya manufaa ya
Watanzania hasa kwa kuwekeza katika kilimo, nchi ingeweza kuepukana na
aibu ya kuwa ombaomba hadi wa chakula kutoka nchi ndogo kama Thailand,
Taiwan na Japan.
“Wananchi wa Babati nimezungumzia masuala ya kilimo hapa kwa sababu
najua ninyi ni wakulima na hata matatizo yenu mengi huku ni juu ya ardhi
yenu ambayo imekuwa ikiporwa au kuhodhiwa kinyemela, huku serikali
ikiangalia tu. Wameendelea kutudanganya kama ilivyo kawaida yao kwa muda
mrefu sasa, wanadanganya wananchi waliowapatia dhamana ya kuongoza.
“Tunamtaka Kikwete awaambie Watanzania fedha zetu trilioni 1.7
tulizopitisha pale bungeni serikali yake ikisema kuwa ni kwa ajili ya
kuwainua wakulima waliopata hasara kutokana na anguko la uchumi, hivyo
fedha hizo zilikusudiwa kufufua uchumi, atuambie ziko wapi,
zilitumikaje, akina nani walinufaika? Tunasema hivyo kwa sababu taarifa
za ndani tulizonazo ni kwamba walipewa maswahiba wa Kikwete.
“Mwaka juzi, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali au CAG
kama anavyoitwa na wengi, alibaini kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa katika
fedha hizo, kiasi kwamba serikali ilikataa kumpatia taarifa kamili ya
matumizi ya fedha hizo ili azifanyie ukaguzi. Sasa tunamtaka Rais
Kikwete maana yeye ndiye alipeleka bajeti ile bungeni kupitia kwa Waziri
wa Fedha, atuambie fedha zetu ziko wapi,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kusema kuwa fedha hizo zingewekezwa kwenye kilimo kupitia
mipango mbalimbali yenye nia ya kuwakomboa Watanzania asilimia 74
wanaotegemea sekta hiyo, huku nchi pia ikitegemea kilimo kwa ajili ya
uchumi wake, zingeweza kuwa mkombozi na nchi ingepiga hatua kubwa.
Dk. Slaa ambaye leo anatarajiwa kufanya mikutano ya hadhara katika
maeneo ya Balangida na Gendabi, alisema ni aibu kwa nchi yenye utajiri
kama Tanzania kuwa ombaomba hadi wa chakula kutoka nchi za nje.
“Ndugu zangu uhuru wetu kama nchi uko shakani mno, tunavyozungumza
hapa tumefika mahali tumekuwa ombaomba wa chakula kutoka nje ya nchi,
tena kutoka katika nchi ndogo ambazo hazina rasilimali kama hapa, nchi
kama Japan, Thailand...
“Naambiwa wakubwa serikalini na washirika wao ndio wanaomiliki maduka
makubwa yanayouza chakula kama mchele, ndiyo maana hawataki kuwajali
wakulima wetu hapa nchini, badala yake wanatuletea vyakula kutoka
Thailand ili wakulima wetu wafe, wao wanufaike,” alisema.
Dk. Slaa alidai kuwa kutokana na wakubwa serikalini na watu aliowaita
kuwa ni washirika wao, kumiliki biashara kubwa za uagizaji wa chakula
kama mchele na sukari kutoka nje, yametengenezwa mazingira
yanayowaathiri wakulima wa Tanzania na wananchi kulazimika kulishwa
vyakula visivyokuwa na ubora kutoka nje ya nchi vinavyouzwa madukani.
“Hata sasa kuna chakula kibovu kimeingizwa huko Zanzibar, nasikia
wanataka kukivusha bara ili eti kiteketezwe, si ajabu wanatafuta njia ya
kukiingiza sokoni kama ilivyo kawaida yao, imefikia mahali watu hawa
hawajali chochote kabisa kufanya ufisadi hata unaohatarisha afya za
wananchi,” aliongeza.
Utendaji wa Bunge
Wakati mjadala wa namna Bunge la Tanzania linavyotekeleza utendaji
kazi wake mbele ya macho ya Watanzania, hasa namna ambavyo linadaiwa
kuwa mhuri wa kupitisha kiulaini hoja za serikali ukizidi kupamba moto
katika mijadala mbalimbali nchini, Dk. Slaa amewapongeza wabunge wake,
akisema sasa Bunge limefika patamu.
Akiwapongeza wabunge wake, kwamba wamekuwa wakisimama kidete ndani ya
Bunge kuiwajibisha serikali kwa niaba ya wananchi tofauti na
wanavyofanya wabunge wa CCM walio wengi bungeni, Dk. Slaa alisema kuwa
ni unafiki kuzungumzia nidhamu bungeni, wakati serikali inashindwa
kusimamia nchi kwa niaba ya Watanzania na kuzuia ufisadi.
Dk. Slaa aliwataka wabunge wake kuongeza kasi kwani waliyonayo sasa
bado ni ndogo, kulinganisha na matarajio ya Watanzania wengi aliosema
wanataabika kwa kukosa uongozi.
“Wakati nikiwa bungeni, aliyekuwa Spika wa Bunge la Kenya wakati ule,
nafikiri anaitwa Kapalo... Francis Ole Kapalo kama sijakosea, alikuja
bungeni wakati wa semina moja hivi, akatuambia Tanzania bado haijawa na
Bunge, alituambia kuwa ule ulikuwa ni mkusanyiko tu wa mashehe na
wachungaji wanaopiga mihuri hoja za serikali.
“Akasema hadi siku atakaposikia ngumi zimerushwa bungeni, pale
atakapoona wabunge wanachachamaa dhidi ya serikali kwa niaba ya wananchi
waliowatuma, bila kujali chochote isipokuwa kuwa wawakilishi wa sauti
za wasiokuwa na sauti, ndiyo ataamini tumeanza kuwa na Bunge, nami
nilikubaliana naye,” alisema Dk. Slaa.
CHADEMA wazindua kampeni Arusha
Katika hatua nyingine, CHADEMA imezindua kampeni zake jijini Arusha
kwa ajili ya uchaguzi wa madiwani wa kata nne; Elerai, Kaloleni, Themi
na Kimandolu ambazo madiwani wake walifukuzwa uanachama na chama hicho
huku kikitamba kuwa hakina uchaguzi Arusha ila CCM ndio wenye uchaguzi.
“Arusha CHADEMA hatuna uchaguzi, sisi tuna ushindi ila CCM ndio wana
uchaguzi,” alisema Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini aliyekuwa mgeni
rasmi katika uzinduzi wa kampeni hizo.
Lema alitumia muda mwingi kunadi sera za CHADEMA na kuongeza kuwa
madiwani waliofukuzwa ndani ya chama hicho, walipokea rushwa na katika
kampeni zao kwenye kila kata, watatoa ushahidi jinsi walivyopokea
rushwa.
Huku akishangiliwa na wananchi wa Arusha, Lema alimuonya Mkuu wa Mkoa
wa Arusha na Mkuu wa Wilaya hiyo kujiepusha na kampeni na kutoa
tahadhari kuwa wakibainika wanafanya kampeni itakuwa ni makosa makubwa
kwao.
Katika kampeni hizo, Lema alirudia kauli yake kuwa mwasisi wa siasa za
udini nchini ni Rais Jakaya Kikwete na akaonya siasa zozote za ubaguzi
wa kidini wala ukabila huku akiwaasa watu wa Arusha kuonesha ukomavu na
kuchana na ukabila.
Lema pia alisema anaendelea na msimamo wake wa kutomtambua Meya wa
Jiji hilo, Gaudence Lyimo hivyo anawaomba wana Arusha kumuunga mkono.
Kwa mujibu wa Lema, hayuko tayari kupeleka ushahidi bungeni kuonesha
rais ni mdini na ndiyo maana wanaogopa kumdai ushahidi huo.
“Ushahidi huo ninao tayari, upo mwingi ndiyo maana hawawezi
kunilazimisha kuwasilisha, mimi nataka kuwasilisha kwa uwazi, sipeleki
ushahidi uchochoroni,” alisema Lema huku akishangiliwa.
CHADEMA katika uchaguzi huo imewasimamisha Injinia Jeremiah Mpinga
katika Kata ya Elerai, Emanuel Kessy (Kaloleni), Melansi Kinabo (Themi)
na Rayson Ngowi katika Kata ya Kimandolu.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya kufukuzwa kwa aliyekuwa Naibu Meya
na Diwani wa Kimandolu, Estomih Mallah; Diwani wa Elerai, John Bayo
ambaye kwa sasa amesimama kugombea kwa tiketi ya CUF; aliyekuwa Diwani
wa Themi, Reuben Ngowi; aliyekuwa Diwani wa Kaloleni, Charles Mpanda na
Diwani wa Viti Maalumu, Rehema Mohamed.
CHANZO CHA HABARI HII NI MTANZANIA DAIMA

Post a Comment