ad

ad

ACHA ULIMBUKENI, SI LAZIMA ‘KUDUU’.


Tumshukuru Mungu kwa kutujalia uhai na afya njema, lakini zaidi ya hapo tumshukuru pia kwa kutuumbia kitu mapenzi au siyo?
Siku zote hatutaacha kuzungumza juu ya mapenzi kwani ni ukweli usiopingika kwamba mapenzi ndiyo maisha yetu. Tunafanya kazi usiku na mchana, tunahangaika huku na huko, lakini mwisho wa siku tunafikiria jinsi gani tutaboresha na kufurahia maisha na wapenzi wetu.
 
Tunafikiria pia ni jinsi gani tunaweza tukapata utulivu na amani katika maisha ya kimapenzi na wapenzi, waume au wake zetu katika siku zote za maisha yetu.
Ndugu zangu, mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana kwenye maisha yetu. Ndiyo maana hata vitabu vya dini vinazungumzia namna gani tunatakiwa kuyaendesha maisha yetu ya kimapenzi katika misingi inayokubalika.
 
Kama wewe ni mfuasi wa dini kati ya uislamu au ukristo, utakubaliana na mimi kwamba kuzini hakuruhusiwi. Watu waliotokea kupendana kwa dhati wanatakiwa kufanya haraka kuhakikisha wanaoana na kuishi ndani ya ndoa ili kumfurahisha Mungu.
Kwa maana hiyo ukishaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na mtu ambaye unatarajia katika siku zijazo kuishi naye kama mke na mume, ujue kabisa kwamba hakuna suala la ‘kuduu’ na kama utalazimisha hilo, tambua utakuwa unapata dhambi.
 
Na kwa kuwa hakuna anayetaka kupata dhambi kwa kudhamiria, tuna kila sababu ya kuangalia tuishije na wachumba au wapenzi wetu katika kipindi ambacho tunasubiri kuingia kwenye ndoa. Hilo litafanikiwa tu kama ninyi mliotokea kupendana mnajua misingi ya dini yenu na mko tayari kuishi kwa kuifuata.
Kwa mfano, tunaambiwa hatutakiwi kukutana kimwili kabla ya kufunga ndoa, je, mko tayari kuvumilia katika hilo? Je, mtaweza kuyashinda matamanio yenu wakati mnawaona marafiki zetu wakijiachia kwa raha zao?
 
Kimsingi katika hili kwa kizazi cha sasa kumekuwa na ugumu sana. Vijana wengi hawako tayari kusubiri, wanaona kufanya ngono ni haki yao hasa pale ambapo wameshatamkiana suala la kufunga ndoa. Wanaona kusubiri ni kujinyima raha bila kujua kuwa ni kinyume na maandiko ya dini.
Ndugu zangu, tujue kwamba kufanya mapenzi kupo tu na subira ni lazima ichukue mkondo wake. Tufahamu kwamba hata bila kukutana kimwili bado penzi linaweza kushamiri hasa kama utajua mbinu ambazo wengi wamekuwa wakizitumia kuyapotezea matamanio ya kufanya ngono pale yanapowajia.
 
Sasa tukae tujiulize kwamba, ni nani ambaye yuko tayari kusubiri? Je, wewe unaweza kustahimili katika hilo? Iulize nafsi yako na naamini utapata jibu. Hata hivyo, kwa utafiti usio rasmi nilioufanya nimebaini kuwa, kuna asilimia ndogo sana ya watu wenye mioyo ya kuweza kuvumilia katika hili.
Yaani kufanya ngono inachukuliwa kama kitu cha lazima vile na ikitokea mpenzi wako akataka kuwa na wewe faragha, ukamwambia asubiri mpaka mtakapooana, kwanza anaweza kukuona mshamba lakini pia hilo likipita kuna mambo mawili yanayoweza kutokea.
La kwanza ni kuwepo kwa uwezekano wa mpenzi wako kukusaliti. Atakachokifanya ni kukubaliana na uamuzi wako wa kusubiri lakini kwa siri atatafuta mtu mwingine ambaye anaweza kumtimizia huku ninyi mkiendelea na uhusiano wenu kama kawaida.
Pili, kwa kuwa na msimamo wako kwamba hufanyi mapenzi mpaka utakapoingia kwenye ndoa, unaweza kukufanya ukatoswa na mpenzi wako. Kama hatakutosa waziwazi utaona anaanza kukupotezea kiaina.
Itaendelea wiki ijayo.
Powered by Blogger.