CAG aibua madudu mapya
WIZARA ya Nishati na Madini imekumbwa na kashfa mpya ya
kushindwa kukusanya kiasi cha dola 12,634,354, sawa na sh bilioni 19.7
kama sehemu ya mirabaha kutoka kwenye kampuni zinazochimba madini
nchini.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG
Mbali na kushindwa kukusanya kiasi hicho cha mirabaha, pia imeshindwa
kukusanya kiasi cha sh 1,645,582,899 kutoka vyanzo mbalimbali kama vile
vitalu vya madini na leseni za umeme.
Hayo yamebainika katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ya mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,
2012, iliyowasilishwa bungeni jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Utouh alisema
kuwa maduhuli yaliyoshindwa kukusanywa na wizara hiyo yalitokana na
mabadiliko ya sheria ya madini iliyorekebisha kiwango cha mrabaha kutoka
asilimia 3 hadi 4.
Mbali ya Nishati na Madini, wizara nyingine iliyokumbwa na madudu ni
ya Ujenzi, ambayo kwa mujibu wa ripoti ya CAG, iliamua kutumia sh
milioni 252.9 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo
ya ujenzi wa barabara na badala yake ililipia madeni yanayowakabili.
Upungufu mwingine uliobainishwa katika ripoti hiyo ni pamoja na
kuongezeka kwa fedha za misamaha ya kodi, ambapo katika kipindi hicho,
serikali ilitoa misamaha ya kodi ya sh trilioni 1.9 kutoka trilioni
moja, sawa na ongezeko la asilimia 27 kutoka 18.
Alisema kuanzia mwaka ujao wa fedha, ofisi yake itakagua misamaha
yote ya kodi inayotolewa na serikali na kuwatangaza hadharani makampuni,
mashirika, wafanyabiashara na watu binafsi wanaopata misamaha ya kodi.
Akizungumzia upungufu uliojitokeza kwenye ukaguzi wa Mamlaka ya
Serikali za Mitaa, Utouh alisema kwamba kumekuwa na udhaifu mkubwa
katika kusimamia mapato ya ndani.
Alitaja upungufu huo kuwa ni vitabu 2,990 vya stakabadhi za mapato
kutoka halmashauri 36 kutokutolewa kwa ajili ya ukaguzi wakati
halmashauri 56 zilikuwa na jumla ya sh bilioni 4.4, ikiwa ni mapato
yaliyokusanywa na mawakala ambao hawajawasilisha kwenye halmashauri
hizo.
“Halmashauri 17 hazikukusanya kodi ya majengo kiasi cha sh bilioni 4.3, sawa na asilimia 38,” alisema.
Kama ilivyokuwa katika taarifa yake ya mwaka jana, ukaguzi wa mwaka
huu pia umebaini kuwapo kwa watumishi 17,710 ambao wamekuwa wakipokea
mishahara pungufu, 1/3 ya mishahara yao, kinyume cha sheria kutokana na
watumishi hao kuelemewa na mikopo.
Pia ripoti hiyo imeendelea kubaini kuwa kuna watumishi hewa, wakiwamo
waliostaafu na waliofariki dunia, wameendelea kulipwa mishahara ya sh
milioni 82.3.
Akizungumzia Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali Kuu, CAG
alisema mfuko huo una hali mbaya, kwani hadi sasa una hasara ya sh
trilioni 6.4, hivyo kuwa kwenye hatari ya kufa.
Hata hivyo alisema pamoja na mfuko huo kuwa na hali mbaya kifedha,
amebaini kuwa ulitoa mikopo ya sh bilioni 67 kwa taasisi za umma na
nyingine bila riba na mikopo hiyo ilidhaminiwa na serikali.
Alizitaja taasisi zinazodaiwa na kiasi cha fedha kwenye mabano kuwa ni
pamoja na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) sh bilioni 54.6, PCCB
(sh bilioni 6.6), Tan Power Resources (sh bilioni 5.4) na Kiwanda cha
Madawa Tanzania (sh milioni 485).
Hata hivyo alisema matokeo ya ripoti ya mwaka huu, yameonesha kuboreka
kwa hati zilizotolewa kwa Serikali Kuu na taasisi zake ikilinganishwa
na miaka iliyopita.
Alisema hati za kuridhisha zimeongezeka kutoka 69 mwaka 2011/2011 hadi
108 wakati hati zenye shaka zimepungua kutoka 12 hadi sita mwaka
2011/2012 na hapakuwa na hati isiyoridhisha wala hati mbaya kama
ilivyokuwa mwaka 2010/2011.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(POAC), Zitto Kabwe, alisema pamoja na mabadilko machache, bado ripoti
hiyo ni mbaya, kwani bado kuna matatizo makubwa ya usimamizi wa fedha za
serikali.
Alishangaa Wizara ya Nishati na Madini kushindwa kukusanya mirabaha
kutoka makampuni ya madini na kusisitiza kwamba kuna kazi kubwa ya
kuibana serikali katika kusimamia matumizi ya fedha za umma.
Post a Comment