ad

ad

Barca kukutana na Bayern; Real wapangwa na Dortmund nusu fainali Champions League.

Droo ya nusu fainali ya mashindano ya Klabu Bingwa barani Ulaya imefanyika leo na timu ya Barcelona ya Uhispania imepangwa kupepetana na bingwa wa Bundesliga msimu huu Bayern Munich ya Ujerumani. 

Nusu fainali nyingine itazipambanisha Real Madrid ya Uhispania na timu nzuri ya Borusia Dortmund. Timu ya Barcelona itakuwa msambweni katika mechi ya awali katika uwanja wa Allianz Arena huko Ujerumani kabla ya kuikaribisha Bayern nyumbani katika mechi ya marudiano kwenye uwanja wake wa Camp Nou. 

Kwa mujibu wa droo hiyo, fainali ya klabu bingwa barani Ulaya itakayosakatwa katika uwanja wa Wembley Mei 25 mwaka huu imeweka uwezekano wa kuzikutanisha timu zote kutoka Ujerumani au Uhispania; hiyo ni kama Barca na Real zitazingo'a timu za Ujerumani katika hatua ya nusu fainali au Bayern na Dortmund kuzibwaga timu za Uhispania katika kindumbwendumbwe cha nusu fainali. Real Madrid ambayo imeonekana kuimarika zaidi itaanza mkakati wake wa kuelekea fainali itakapokuwa ugenini. 

Mechi za awali zitachezwa tarehe 23 Aprili na 24 huku zile za marudiano zikifanyika wiki moja baadaye yaani tarehe 30 Aprili na Mei Mosi.
Powered by Blogger.