Polisi wadaiwa kumpora mgeni Sh11 mil
WATU wanaodaiwa kuwa ni polisi kwa kushirikiana na raia
wanaoaminiwa kuwa ni matapeli, wanadaiwa kumpora raia wa Yemen dola za
Marekani 7,000 zinazokadiriwa kufikia Sh11 milioni pamoja na mali
nyingine.
Raia huyo, Saleh Khalfan Abdulah Al Wahaibi
alifika nchini mwishoni mwa mwaka 2011 kwa lengo la kutafuta fursa za
biashara ya madini na baadhi ya kampuni za hapa nchini.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili Al Wahaibi
alisema tukio hilo lilitokea Juni 25, 2012 katika baa ya Masai iliyopo
Kinondoni, jijini Dar es Salaam na kwamba alikwenda kutoa taarifa kituo
cha Polisi Osterbay na hakuna hatua zozote zilizochukiliwa hadi sasa.
Aliongeza kuwa anaamini kuwa polisi wanawafahamu
watu hao lakini kwa sababu ambazo hazifahamu, hakuna hata mmoja
aliyekamatwa na amekuwa akizungushwa mara kwa mara hadi alipoamua kwenda
Kituo Kikuu cha Polisi, makao makuu lakini hata huko anadai bado
anazungushwa.
Kwa mujibu wa Al Wahaibi alipozidi kulalamika katika Kituo cha Polisi Osterbay walichukuwa maelezo yake na kuyahifadhi katika kumbukumbu za kipolisi namba OB/RB/11569/2012.
Anasema alipokwenda makao makuu kupeleka
malalamiko yake, alikabidhiwa kwa mmoja wa maofisa wa polisi ambao
anakumbuka kuwa ni miongoni mwa watuhumiwa wa tukio hilo jambo ambalo
linampa wasiwasi.
“Nilipoambiwa ofisa huyo (jina linahifadhiwa kwa sasa) kuwa ndiye atakeshughulikia kesi yangu, niliogopa kwa kuwa namkumbuka kuwa ni miongoni mwa walioshiriki kunipora fedha zangu,”alisema.
Katika barua yake kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai (DCI) ya Septemba 11, 2012 ambayo Mwananchi Jumapili
imeiona, raia huyo wa Yemen ameomba kusaidiwa kupatiwa haki zake ikiwa
ni pamoja na kuwakamata wahusika wa utapeli huo na kufikishwa kwenye
vyombo vya sheria.
Akielezea mkasa mzima katika barua hiyo kwenda kwa DCI, Al Wahaibi alisema alipigiwa simu na mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Mohamed Bakari akimkaribisha Tanzania na kumtaka wakutane kwa mazungumzo ya kibiashara.
Kwa mujibu wa Al Wahaibi, anahisi Bakari alipata
namba yake kutoka kwa mwanamke ambaye alianzisha mazoea naye alipokuwa
akifika katika baa ya Masai, iliyopo Kinondoni.
“Baada ya kuwasiliana kwa muda mrefu na kukutana naye, siku moja alinipigia simu akiniambia anahitaji kuonana na mimi sababu anajambo muhimu,” anaeleza Al Wahaibi.
“Baada ya kuwasiliana kwa muda mrefu na kukutana naye, siku moja alinipigia simu akiniambia anahitaji kuonana na mimi sababu anajambo muhimu,” anaeleza Al Wahaibi.
Anasema alipofika alikuta Bakari katika nyumba
moja ambayo haikumbuki vizuri lakini ipo maeneo ya Buguruni akiwa na mtu
mwingine ali yemtambulisha kama rafiki yake anayeitwa Sadik Salim
Bakari na kumweleza kuwa mke wa Sadik ana matatizo na anahitaji fedha
dola 5,000 ambazo anadaiwa na bosi wake kazini na kwamba amekuwa
akitembea na mke wake kwa mgongo wa deni hilo.
Aliongeza kuwa watu hao walimwahidi wangemlipa
deni hilo ndani ya siku mbili kwani wanasubiri fedha zao na kwamba
wangemlipa na faida ya dola 5,000 zaidi kama riba.
Raia huyo ambaye kwa sasa anaishi Mbagala Kimbangulile anasema
siku ya makabidhiano ya fedha hizo na kusaini mkataba ambayo
walikubaliana yafanyike Masai baa, Bakari alimpigia simu kuwa anakuja na
muuzaji wa dhahabu aliyemtaja kwa jina la Hamis Ngwamangwa.
“Walipofika niliwataka wanioneshe vitambulisho
vyao na kumtaka Sadik anikabidhi hati yake ya kusafiria (passport),
lakini walisema wamevisahau na hapo niligundua kuwa watu hao ni matapeli
kwani hata dhahabu alizokuja nazo Ngwamangwa zilikuwa feki pia,”
anaeleza.
Anasema Bakari ndiyo aliyemtolea bastola na
kumlazimisha kusaini mkataba wa makubaliano ya kuwapa fedha na
kumrudishia baada ya siku mbili, kisha alimsukuma chini na kuchukua
fedha zake dola 7,000 na simu na kumtishia kuwa wangemuua kama
angejaribu kufanya chochote.
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI

Post a Comment