Tume Ya Uchaguzi (NEC) Yajibu Upotoshwaji Wa CHADEMA Kuhusu Kuhamisha Vituo Jimbo La Kinondoni
Hussein Makame, NEC
Tume
ya Taifa ya Uchaguzi imesema uamuzi wa kuhamisha vituo 46 vya kupigia
kura katika jimbo la Kinondoni umezingatia matakwa ya kanuni za Uchaguzi
kwa kuvishirikisha vyama vyote vya siasa ikiwemo Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema).
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani jijini Dar es
Salaam, kufuatia taarifa za upotoshaji zilizotolewa na baadhi ya
magazeti zinazodai kuwa Chadema hakikushirikishwa katika uamuzi wa
kuhamisha vituo hivyo.
Alisema
kabla ya uamuzi wa kubadilisha vituo hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo
la Kinondoni iliitisha mkutano na vyama vya siasa tarehe 30 Januari,
2018 na wawakilishi 26 walishiriki kwenye mkutano huo wakiwemo
wawakilishi wa Chadema.
“Tume
ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na vyama vya siasa katika kikao
kilichofanyika tarehe 30 mwezi Januari mwaka huu walikubaliana kuhamisha
vituo 46 na katika vituo hivyo vituo 16 viko kata ya Kigogo, vituo 8
viko kwenye kata ya Mwananyamala na vituo 22 viko kwenye kata ya
Kijitonyama” alisema Kailima.
Alifafanua
kuwa kwa mujibu wa kifunga cha 21 (1) cha kanuni za Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, vituo vya kupigia kura havitakiwa kuwa
kwenye maeneo ya watu binafsi, nyumba za mashabiki wa vyama vya siasa
au maeneo ya majeshi na ibada.
“Nimesikitishwa
na kauli ya Chadema eti hawakushirikishwa, nimesikitishwa kwa sababu
kumbukumbu za mikutano zilizopo tarehe 30 Januari mwaka huu, chama cha
Chadema kiliwakilishwa na Mwenyekiti wa Wilaya Bw. Mustafa Muro pamoja
na Katibu wa Wilaya Bw. Shabani Kirita” alibainisha Kailima.
Alifafanua
kuwa wawakilishi hao walihudhuria mkutano wa msimamizi wa Uchaguzi
jimbo la Kinondoni na vyama vya siasa na katika mkutano huo kulikuwa na
ajenda moja tu kuhusu kuhamisha vituo vya kupigia kura na vyama vyote
kwa pamoja vilikubaliana kikiwemo Chadema.
“Unaposema
chama cha Chadema hakikuhusishwa ninapata masikitiko makubwa sana.Tume
ya Taifa ya Uchaguzi haiwezi kuingilia mawasiliana ya ndani ya chama
husika, kwa hiyo kama hakuna mawasiliano kati ya makao makuu na ngazi ya
Wilaya hilo sio tatizo la Tume” alisema Kailima.
Alifafanua
kuwa katika kata ya Kigogo kuna baadhi ya vituo vya kupigia kura
vilikuwa ndani ya msikiti wa Kigogo na vingine vilikuwa ndani ya eneo la
Zahanati eneo ambalo lilikuwa dogo kutosha kwa ajili vituo vya kupigia
kura.
Kailima
aliongeza kuwa, vituo 8 vya Mwananyamala vilikuwa kwenye eneo ambalo
wananchi walikuwa wanalilalamikia, vyama vya siasa vikaridhia kwamba
vituo hivyo vihamishwe na vituo 6 vikapelekwa kwenye kata inayohusika na
vituo 2 vikapelekwa uwanja wa Kopa.
Akizungumzia
vituo 22 kwenye kata ya Kijitonyama, Kailima alisema vyama vyote
vilikubaliana kuvihamisha, hivyo Chadema kikisema havikukubaliana ndipo
inapoleta shida.
Alisema
Maelekezo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi kipengele cha 9 (2) (C) kinasema
kabla vituo vya kupigia kura havijahamishwa ni lazima Tume ishirikiane
na vyama vya siasa na Tume imetimiza takwa hilo la kikanuni na vyama
viliitwa vikakubali.
“Ukisema
huwezi kuhamisha vituo kabla hujafanya Uboreshaji, huwezi kuacha makosa
yakaendelea kuwa makosa.Hatujahamisha kutoa mkoa mmoja kwenda mwingine,
bali tumehamisha kwa ridhaa na vyama vikaridhia.
“Kwa hiyo niwasihi chama cha Chadema kabla hakijaanza kulaumu wawasiliane na wenzao kwenye ngazi husika.” Alisema Kailima.
Katika
hatua nyingine, Kailima amelisihi gazeti la Mwananchi, litoe habari
sahihi kuhusu Tume na kuacha kuandika habari zinazoihusu Tume bila ya
kuwasiliana nayo ‘kubalance’ kuhusu habari husika.
“Nalisihi
gazeti la Mwananchi, tunaliheshimi ni gazeti bora na gazeti
linaloheshimika, lakini nilisihi kabla halijatoa habari lazima lifanye
balance ya habari” alisema Kailima na kuongeza kuwa:
“Wenyewe walipowauliza Chadema wakasema hawakushirikishwa walitatakiwa kuchukua fursa ya kuwauliza Tume kama hawakushirikishwa.
“Kwa
hiyo nilisihi kwa sababu si mara moja wala mara mbili wamekuwa wakitoa
taarifa ambazo si sahihi kuhusu Tume, tunawasihi na kuwaomba wanapotaka
kutoa habari za Tume watoe habari za Tume zikiwa sahihi”
Alifafanua
kuwa kulitaka gazeti hilo kwamba hata linapotaka kukosoa ni lazima
likosoe kwa habari sahihi na sio kwa habari za upotoshaji na za upande
mmoja.
Post a Comment