ad

ad

Bombardier Nyingine na Boeing 787 Kutua Nchini Julai Mwaka Huu

Ndege mbili; moja aina ya Bombardier na nyingine kubwa Boeing 787 yenye uwezo wa kubeba abiria 262 zilizonunuliwa na serikali, zinatarajiwa kuwasili nchini Julai mwaka huu.

Serikali imenunua ndege hizo ikiwa ni mkakati wa kuimarisha Shirika la Ndege (ATCL) ili limudu ushindani kwenye biashara ya kusafirisha abiria na kujiendesha kwa faida.

Akiwasilisha taarifa ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa kipindi cha Januari 2017 hadi, jana, mjini hapa, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Prof. Norman Sigalla, alisema wamejulishwa kuwa pamoja na ndege mbili mpya aina ya Dash 8 Q400, Julai serikali inategemea kupokea ndege zingine mbili ambapo moja ni Dash 8 Q400 na nyingine aina ya Boeing 787 yenye uwezo wa kubeba abiria 262.

Alisema kwa sasa ATCL ina ndege tatu zinazofanya safari ndani na nje ya nchi, lakini akasisitiza kuwa biashara ya ndege inahitaji mikakati mikubwa ya kibiashara kuweza kuingia katika soko la ushindani.

"ATCL iangaliwe kama kampuni ya kibiashara na siyo kutoa huduma na ijitangaze kwenye vyombo rasmi vya kimataifa ambavyo huonyesha safari za ndege duniani," alisema.

"Kampuni ijipange kuingia katika soko kwa kujitangaza kwenye vyombo vya habari, majarida, vipeperushi, kujali wateja, kuwa na bei nafuu ili kuhakikisha abiria wengi wanatumia ndege hizo."

Prof. Sigalla pia alisema Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) inashauriwa kuhakikisha viwanja vya ndege visivyokuwa na hati vinapimwa kisha kupatiwa hati miliki.

Alisema viwanja hivyo pia vinapaswa kuwekewa uzio kuepusha uvamizi wa maeneo jambo ambalo huleta migogoro na wananchi.

"Ili kuongeza udhibiti na ulinzi katika viwanja vya ndege vilivyopo mipakani kama vile Mtwara, Kigoma na Kagera kuepusha viwanja hivyo kupitishwa biashara haramu," alisema.

No comments

Powered by Blogger.