Ajifungua Mtoto Kwenye Korido Hospitalini
JESICA HOGAN, mama wa watoto sita mkazi wa Riley, Kansas, Marekani, amejifungua mtoto pekee wa kiume katika korido ya hospitali ambayo alikuwa anawahishwa kwenda kujifungua.
Mtoto huyo aliyeleta furaha katika familia hiyo ambayo ilikuwa na mabinti mtupu, anaitwa Max, ambaye alizaliwa akiwa salama na mwenye afya njema.
Mwanamke huyo aliyejifungulia katika Hospitali ya Via Christi, ya Manhattan, Kansas, alisema alikuwa hana uhakika wa tarehe ya kujifungua, hivyo hakujua ni lini uchungu ungelianza. Alikuwa nyumbani wakati chupa ilipovunjika kunako saa tisa usiku ambapo mumewe, Travis, alimkimbiza hospitali.
Mara tu baada ya kuingia katika korido ya hospitali hiyo, Jesica alihisi mtoto alikuwa ameanza kutoka, hivyo akaanza kuvua suruali yake wakati kichwa cha mtoto kilianza kujitokeza. Walianza kusaidia na mumewe hapohapo kwenye korido ambapo alilala chini kabla ya manesi kuja na kumsaidia.
“Nilikuwa sifahamu hasa siku halisi ya kujifungua, lakini siku hiyo nilijua imefika, nikamwambia Travis naye akaamua kunikimbiza hospitali.” anasema Jesica ambaye anasema alisahau hata kuvaa viatu kwa ajili ya uharaka.
Post a Comment