Michirizi Ya Damu - 10

“Nani?” aliuliza kwa sauti.
“Fungua mlango!” alisikika mwanaume aliyekuwa nje ya chumba kile.
Akaendelea kuvaa kwa haraka sana, watu waliokuwa nje walipoona hafungui mlango, wakauvunja na kuingia ndani. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumuweka chini ya ulinzi. Hakuwajua watu hao kwani wale walioanza kuingia ndani ya chumba kile walivalia nguo za kiraia.
Alipiga kelele kwa kudai kwamba alivamiwa na majambazi. Akanyamazishwa kwa kuambiwa kwamba wao hawakuwa majambazi kama alivyofikiria bali walikuwa polisi na ili kumridhisha wakamtolea vitambulisho vyao.
“Mwenzako yupo wapi?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Nani?”
“Uliyeondoka naye kwenye mapiramidi!” alijibu mwanaume huyo.
“Sijui! Nimetoka bafuni, simuoni. Kwani kuna nini?” aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Una uhakika!”
“Ndiyo! Kwani kuna nini?’ aliuliza Maria huku akiwaangalia wanaume hao.
Wakamwambia kilichokuwa kimetokea kwamba mwanaume ambaye alikuwa naye alifanya mauaji ya kutisha katika mapiramidi yale, alimuua bilionea Keith ambaye kwa Maria ndiye alikuwa tegemezi lake, ndiye aliyekuwa akimpa pesa nyingi za matumizi, ndiye ambaye alimfanya kujiona mwanamke wa mjini mwenye kila kitu, cheni ya dhahabu, hereni na vito vingine vingi.
“Keith amekufa?” aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Ndiyo! Ameuawa na mtu uliyetoka naye ndani ya piramidi lile. Mfungeni pingu tuondoke naye, huyu atakuwa anafahamu kila kitu,” alisema mwanaume mmoja na hapohapo kufungwa pingu.
Maria alikuwa akilia, hakuamini kilichokuwa kikitokea, hakuamini kama ingetokea siku moja ambayo angefungwa pingu kwa ajili ya kupelekwa katika kituo cha polisi.
Moyo wake ulimuuma, aliumia na hakuacha kulia. Mbali na kufungwa pingu, kilichokuwa kikimuumiza ni kifo cha Bilionea Keith, mwanaume huyo alikuwa mtu pekee aliyemjali, aliyemsaidia kwa kila kitu, maisha yake yangekuwaje baada ya kifo cha mwanaume huyo?
“Haiwezekani! Keith hajafa! Haiwezekani!” alisema Maria huku akilia kama mtoto.
“Twende kituo cha polisi! Mengine utayasikia hukohuko!” alisema polisi mmoja.
Hakujua sababu iliyomfanya Fareed kufanya mauaji hayo, alishangaa, hakuona kama Bilionea Keith aliwahi kuzozana na mwanaume yeyote yule, kwa nini Fareed alimuua? Je, Fareed alijua kwamba polisi walikuwa njiani kufika hotelini hapo mpaka kuamua kumtoroka? Na kwa nini hakumwambia ili watoroke wote? Kila alichokuwa akijiuliza, alikosa majibu.
****
Kila mtu aliyesikia taarifa juu ya kifo cha Bilionea Keith hakuamini, wengi walijua ni tetesi ambazo ziliandikwa kwenye mitandao ya nchini Misri ili kuishtua dunia, kwao, bilionea kama huyo kuuawa kizembe namna hiyo lilionekana kuwa jambo gumu mno.
Watu waliokuwa na ndugu zao nchini Misri waliwapigia simu, walitaka kufahamu kilichokuwa kimetokea, walitaka kujua ukweli juu ya jambo hilo. Waandishi wa habari wa CNN, BBC na wengineo wakawatuma waandishi wao nchini Misri kufuatilia kile kilichokuwa kikiendelea.
Walipofika katika Hospitali ya Sheikh Mazrui iliyokuwa pembezoni kidogo mwa Jiji la Cairo, wakakutana na madaktari ambao waliwathibitishia kwamba mtu aliyekuwa ameuawa alikuwa Bilionea keith.
CNN walipotoa taarifa hiyo ndiyo kila mtu akaamini kwamba kweli mtu huyo alikuwa ameuawa. Lilikuwa pigo kubwa, watu wengi walihuzunika kwani miongoni mwa mabilionea walipokuwa na roho nzuri duniani alikuwa mwanaume huyo, hakukuwa mtu aliyejua ubaya wake kwani kila alipokuwa katika umati wa watu, alijivisha roho ya kondoo na wakati alikuwa mbwa mwitu.
Kila mtu alitaka kujua kuhusu mtu aliyefanya mauaji, kila mmoja masikio yake yalikuwa kwa polisi wa nchini humo wakitaka kujua ni nani hasa alikuwa amehusika katika mauaji hayo na wakati huo muuaji huyo alikuwa wapi.
Polisi wa nchini Marekani, kupitia kitengo cha Interpool walikuwa wakiwasiliana kwa ajili ya kuufahamu ukweli na kujua mahali muuaji huyo alipokuwa. Kulikuwa na kazi kubwa, walipewa picha zake zilizopigwa kwa kutumia kamera za CCTV ambazo hizohizo ndizo walizokuwa wakizitumia.
Polisi walijitahidi kumtafuta kimyakimya, hawakutaka ajue kama tayari walikuwa na picha zake lakini kitendo cha CNN kutoa picha hizo tayari kilionyesha kwamba muuaji alijua kuwa picha zake zilikuwa kila kona, hivyo alitakiwa kujificha.
Wakaacha na suala la kuficha picha zake, walichokifanya ni kuziachia mitaani, zilibandikwa kila kona, kila mmoja alitakiwa kujua kwamba mtu aliyefanya mauaji ya bilionea mkubwa nchini humo alikuwa yeye.
“Jamani! Tuhakikisheni huyu mtu anakamatwa, vinginevyo mambo yatakuwa mabaya kwetu,” alisema kamanda mkuu wa jeshi la polisi nchini humo, alikuwa akiwaambia wenzake.
“Sawa mkuu!”
“Fungeni mipaka yote, bandari, mpaka mfereji wa Suez, asije kutoroka kuelekea Ulaya,” alisema kamanda huyo.
“Sawa mkuu!”
Hilo ndilo walilolifanya, kwa haraka sana mipaka ikafungwa, walitaka kuhakikisha mtu huyo hatoki ndani ya Misri akiwa salama, ilikuwa ni lazima kumtafuta, wampate na kumfanya walichokitaka wao na kuionyeshea dunia kwamba walikuwa na uwezo wa kumtafuta mtu yeyote na kumpata.
Muda ulizidi kwenda mbele, hawakujua mahali alipokuwa Fareed, walishangaa kwani hawakuamini kama mtu huyo alipanda ndege kuondoka nchini hapo kwa kuwa tarayi taarifa zilitolewa kila kona kwamba alikuwa akitafutwa, na uzuri zaidi ni kwamba hata picha tayari ziliwekwa kila kona.
Siku ya kwanza ikapita, siku ya pili nayo ikapita, kwenye kila kona alikuwa akitafutwa, zawadi nono likawekwa la dola laki tano ambazo zilikuwa ni zaidi ya bilioni moja lakini bado mtu huyo hakuonekana kitu kilichowafanya polisi kuchoka, japokuwa walishirikiana na Wamarekani kupitia Interpool lakini bado Fareed hakupatikana.
****
Wakati polisi wakihangaika kumtafuta Fareed, yeye alikuwa akifikiria lake, alitaka kuondoka nchini Misri pasipo kuonekana. Alijua kwamba endapo angeendelea kubaki humo ilikuwa ni lazima kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
Alitakiwa kutoroka haraka iwezekanavyo kitu ambacho kwake hakikuwa na tatizo lolote lile, alichokuwa akihitaji ni kupata usafiri wa haraka wa kuvuka na kuingia Ulaya, sehemu ambayo aliamini ingekuwa nafuu kwake na si kuendelea kubaki Afrika.
“Ni lazima niende Ulaya, siwezi kubaki Afrika kwa sasa,” alisema Fareed.
Hakutaka kutumia ndege, aliamini kwamba katika viwanja vya ndege kulikuwa na ulinzi mkubwa na njia pekee ya kuondoka nchini humo ilikuwa ni moja tu, kwa kutumia ndege, tena si kuelekea katika bandari za Said au Ras el Bar bali alitaka kwenda katika Mji wa Fayed ambapo kulikuwa na ziwa Great Bitter lililounganishwa na mfereji wa Suez, hapo angeomba msaada wa kupanda meli za kwenda Ulaya ambapo angetokomea huko.
Safari hiyo ilitakiwa kufanyika usiku wa siku hiyo, hakutaka kubaki hapo Cairo bali alichokifanya ni kuondoka kuelekea barabarani ambapo akakodi teksi kwa ajili ya kumpeleka Fayed.
“How much?” (kiasi gani?)
“One thousand pound,” (paundi elfu moja) alijibu mwanaume aliyekuwa kwenye taksi.
“Okey!” (sawa)
Si kila mtu aliyekuwa akijua kile kilichokuwa kikiendelea, watu wengine walikuwa bize na kazi zao na si wote walioziona picha za Fareed katika sehemu mbalimbali zilipobandikwa.
Mmoja wa watu ambao hawakuwa wakijua kitu chochote kilichokuwa kikiendelea alikuwa dereva huyo. Ilikuwa ni vigumu kumfahamu Fareed hata kama angeona tangazo na picha zake mara kwa mara kutokana na jinsi alivyovaa.
Alikuwa na kanzu ndefu nyekundu, kichwani alivalia kiremba kikubwa huku akiwa ameshika Juzuu mkononi. Alionekana kama ustadhi ambaye alikuwa akienda sehemu fulani kutoa mawaidha au Imamu fulani aliyekuwa akiwahi sehemu fulani kuswalisha.
Akaingia ndani ya gari hilo, alikuwa na kibegi chake kidogo kilichokuwa na pesa nyingi ambazo alizipata katika kazi yake kubwa aliyokuwa ameifanya kwa kipindi kirefu, kutembea na mabilionea wengi.
Kutoka hapo mpaka Fayad ilikuwa ni zaidi ya kilometa mia moja, hilo halikuwa tatizo, kwa kuwa barabara ilikuwa nzuri, hawakuona kama wangetumia muda mwingi mpaka kufika huko.
Garini, walikuwa wakizungumza kirafiki na Fareed alijitambulisha kama Hamad Al Hamad ambaye alitokea nchini Nigeria na kufika hapo kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Iddi ambayo ilimalizika kwa siku tano zilizopita.
“Kwa hiyo umetokea Nigeria?” aliuliza dereva yule.
“Ndiyo! Ninarudi huko keshokutwa, ninakwenda fayad kutoa mawaidha katika msikiti mkuu wa hapo kisha nitarudi Cairo,” alisema Fareed huku akimwangalia mwanaume huyo.
Walizungumza mambo mengi sana, hakukuwa na siku ambayo Fareed alijifanya kuwa mtu wa dini kama siku hiyo. Kila alipokuwa akizungumza sentensi tano, aliingizia jina la Mtume Muhammad, kila alipokuwa akizungumza sentensi tano, alizungumza kuhusu swala, jinsi Muislamu anavyoweza kuingia motoni kama tu hatokuwa akiswali swala tano kwa siku.
“Na uzninifu! Siku hizi watu wanazini sana. Wewe una wanawake wa nje wangapi?” aliuliza Fareed huku akimwangalia dereva huyo aliyeonekana kuwa mtu mzima kidogo.
“Mimi ni mwenye dhambi! Nina mahawala watatu. Allah anisamehe,” alisema dereva huyo, aliumia moyoni mwake, kwa jinsi Fareed alivyokuwa akizungumza, alionekana kuwa mtu wa swala tano.
Safari iliendelea, walikuwa wakizungumza mambo mengi njiani. Magari ya polisi yalikuwa yakiwapita kwa sana kiasi kwamba dereva yule alikuwa akishangaa tu. Muda wote Fareed alipokuwa akiyaona magari hayo, alikuwa akishangaa, aliamini kwamba hao walikuwa wakimtafuta yeye, alipokuwa akiangalia saa yake, ilikuwa ni saa 11:30 alfajiri.
Hawakuchukua muda mrefu wakaanza kuingia katika Mji wa Ismailia. Walipofika hapo, wakakutana na magari kama kumi yaliyokuwa yakikaguliwa na askari waliokuwa mahali hapo. Dereva yule hakuogopa hata kidogo, hakujua kama msako ule ulikuwa ni kwa ajili ya abaria aliyekuwa ndani ya gari lake.
“Kuna nini?” aliuliza Fareed huku akimwangalia dereva.
“Sijui! Nashangaa! Huwa hakuna kitu kama hiki huku,” alijibu dereva yule, alipokuwa akiwaangalia polisi wale, walishikilia karatasi mikononi mwao iliyokuwa na picha ya Fareed.
Hakutaka kujiuliza, alikuwa na jibu kichwani mwake kwamba polisi wale walikuwa mahali hapo kwa ajili yake hivyo ilikuwa ni lazima afanye kila linalowezekana aweze kuondoka mahali hapo.
“Ngoja nisogeze gari wakague wanachokitaka, wakimaliza tuondoke zetu,” alisema dereva huyo, alitamani kumwambia alirudishe gari nyuma, alichoshindwa ni kwamba kwa nyuma kulikuwa na gari jingine, na alipokuwa akiendelea kuwaangalia polisi hao, walikuwa wakizidi kusogea kule walipokuwa. Walibakiza gari moja kabla ya kuwafikia, mbaya zaidi mikononi mwao walikuwa na picha yake.
“Mungu wangu! Nimekwisha,” alisema Fareed huku mapigo yake ya moyo yakiwa juu. Yalidunda mara mia moja kwa dakika.
****
Fareed hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya mahali hapo, polisi wale waliendelea kusogea kule gari lao lilipokuwa kwa ajili ya kulichunguza ili kuona kama mwanaume aliyekuwa akitafutwa alikuwa ndani ya gari hilo au la.
Wakati wakiwa wamebakiza hatua kama kumi kulifikia, ghafla adhana ikaanza kusikika ikiadhiniwa. Kwa haraka sana Fareed akamwambia dereva kwamba lilikuwa kosa kubwa sana kupita siku pasipo kuswali hivyo akateremka kutoka garini na kwenda pembeni kidogo.
Akasimama na kuangalia kibla, dereva yule alishangaa, ni kweli alikuwa na abiria wengi waliokuwa wakipanda ndani ya gari lake lakini huyo abiria wa siku hiyo alikuwa kiboko, aliijua dini, alipenda kuswali utadhani alikuwa ndugu yake mtume.
Polisi walipofika, wakachungulia ndani, wakamwangalia dereva ambaye aliwaambia alikuwa na safari ya kuelekea Fayed na alikuwa amempandisha ustaadhi mwenye kujua misingi ya dini na alitoka nje kwenda kuswali.
“Ndiye yule?” aliuliza polisi mmoja.
“Ndiyo! Anakwenda kwenye sherehe ya Iddi na yeye ndiye anasubiriwa,” alisema dereva yule, kitendo kile alichokifanya Fareed kikawatoa hofu polisi na kuona kwamba walikuwa wakipoteza muda kulipekua gari hilo, hivyo wakasogea mbele kwenye magari mengine.
Fareed alijifanya kuswali, watu wengine walikuwa wakimshangaa, walijua kwamba alikuwa mtu wa dini sana kumbe upande wa pili kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea. Alichukua dakika saba, alipomaliza, akarudi garini huku uso wake ukiwa umefunikwa kwa kiasi fulani.
“Twende!” alisema Fareed, dereva akawasha gari na kuondoka mahali hapo huku polisi wale wakiwa kwenye magari mengine, hawakujua kama mtu waliyeamini kwamba alikuwa ni wa dini sana, aliyependwa kuswali kumbe ndiye alikuwa mtu waliyekuwa wakimtafuta kwa udi na uvumba.
Hawakuchukua muda mwingi wakafika Fayed, Fareed alimshukuru Mungu kwa kuona kwamba sasa ilikuwa ni nafasi yake ya kutoroka nchini Misri na kwenda katika nchi yoyote ya Ulaya.
Aliamini kwamba kama angepanda ndege ndani ya nchi hiyo ilikuwa ni lazima kukamatwa, hakutaka kuona hilo likitokea na ndiyo maana aliamua kupanda meli, tena iliyokuwa ikielekea Ulaya kwa kupitia katika Mfereji wa Suez ambayo ingempeleka mpaka Cyprus na kuunganisha mpaka nchini Uturuki.
Alipofika Fayed, akateremka na kumlipa dereva kiasi cha fedha alichokihitaji na kuondoka mahali hapo. Hakutaka kuelekea hotelini, bado aliona kwamba alikuwa kwenye hatari kubwa hivyo kama angediriki kwenda huko ingekuwa ni rahisi kwake kukamatwa.
Alichokifanya ni kwenda katika ufukwe wa Ziwa Great Bitter ambapo kwa mbali aliziona meli zikiwa zimepaki huku nyingine zikipakiza mizigo ambayo ilitakiwa kupelekwa katika nchi mbalimbali barani Ulaya. Huku akiwa mahali hapo, macho yake yakatua kwa vijana wanne waliokuwa wamekaa pembeni kabisa huku macho yao yakiangalia kule meli zilipokuwa.
Kwa ufahamu wa harakaharaka akahisi kwamba hao walikuwa Beach Boys ambao kazi zao zilikuwa ni kuwafanyia mipango watu waliokuwa wakitaka kuzamia kwenda barani Ulaya. Akawafuata, aliposimama mbele yao, kila mmoja akayainua macho yake na kumwangalia mwanaume huyo.
Hawakujua mwanaume huyo alikuwa akifanya nini mahali hapo kwani haikuwa rahisi kumuona mtu mweusi akiwa katika ufukwe huo. Wakamuuliza alichokuwa akikihitaji, hakuwaficha, akawaambia kwamba alitaka kuzamia kuelekea barani Ulaya, alikuwa amesafiri kwa umbali mrefu, lengo kubwa likiwa ni kufika huko.
“Umetokea nchi gani?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Nigeria!”
“Ooh! Sawa. Kwenda Ulaya si tatizo. Ila una pesa?” aliuliza kijana mmoja.
“Kiasi gani?”
ITAENDELEA KESHO HAPA HAPA
Post a Comment