Serikali Yamwaga Ajira 400 TRA
Benny Mwaipaja, Shinyanga
Serikali
inatarajia kuajiri wafanyakazi 400 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
katika kipindi kifupi kijacho ili kukabiliana na changamoto ya upungufu
wa watumishi katika Mamlaka hayo, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi
na makusanyo ya kodi.
Ahadi
hiyo imetolewa Mjini Shinyanga na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua
utendaji wa Mamlaka hayo mkoani humo.
Dkt.
Kijaji amesema kuwa taratibu zote zimekamilika na wakati wowote nafasi
za ajira zitatangazwa na kwamba nafasi hizo zimelenga kuiwezesha TRA
kuwafikia watu wengi zaidi na kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi.
“Tunatambua
changamoto ya uchache wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA
ndio maana tumeamua kuajiri wafanyakazi hao 400 ambao ni wengi kuliko
kada nyingine ili tuweze kuimarisha utendajikazi wa Mamlaka na hivyo
kuongeza makusanyo ya kodi zinazotakiwa kwa shughuli za maendeleo
nchini” alisema Dkt. Kijaji
Alisema
kuwa pamoja na uhaba wa watumishi, anaamini kuwa lengo la mwaka huu la
kukusanya shilingi trilioni 17 ambazo Mamlaka hayo imepangiwa yatafikiwa
na ikiwezekana kuzidi kwa kutumia wafanyakazi waliopo.
Dkt.
Kijaji alitoa rai kwa wafanyakazi wa TRA kuwa waadilifu na kwamba
atakayebainika kukiuka maadili yake ya kazi atachukuliwa hatua kali za
kinidhamu na kisheria.
Awali
Meneja wa Mamlaka ya Mapato mkoa wa Shinyanga Bw. Jumbe Samson,
alieleza kuwa mkoa wake umepangiwa lengo la kukusanya Shilingi bilioni
18 na kwamba wanauhakika wa kufikia lengo hilo kutokana na mikakati
mbalimbali waliyojipangia ikiwemo kusimamia ukusanyaji kodi kikamilifu
katika sekta ya madini.
Kwa
upande wake, Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA Bw.
Beatus Nchota alisema kuwa Mamlaka yake imejiwekea mipango ya kufungua
ofisi zake kila wilaya hapa nchini ili kusogeza huduma karibu na
wananchi na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali ili lengo
walilopewa la kukusanya shilingi trilioni 17 liweze kufikiwa.
Mkuu
wa Wilaya ya Shinyanga, Bi. Josephine Matiro, akizungumza kwa niaba ya
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, alisema kuwa Serikali mkoani humo
itahakikisha kuwa TRA inatimiza malengo yake ya kukusanya kodi na
kumhakikishia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji kwamba
watasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Post a Comment