Msajili wa vyama vya siasa aibua utata sheria mpya ya vyama
Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa imeibua utata kuhusu mchakato wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa, huku wadau wakitaka iweke hadharani rasimu ya mabadiliko ya sheria hiyo.
Mchakato
huo umeanza kunyooshewa vidole na vyama vya siasa na hasa vya upinzani
vikidai una lengo la kutaka kuvikandamiza na kuirudisha nchi kwenye enzi
cha mfumo wa chama kimoja.
Utata huo unajitokeza
katika taarifa kwa umma ya msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis
Mutungi aliyoitoa Oktoba 13 akielezea mchakato huo na rejea ya barua
yake ya Agosti 28 yenye kumbukumbu namba KA.231/322/01/174 kwenda kwa
makatibu wakuu wa vyama kutofautiana.
Katika barua ya Agosti 28, msajili aliwataka wadau kutoa maoni ndani ya wiki mbili baada ya kupokea barua hiyo.
Hata hivyo, katika taarifa ya Oktoba 13, msajili amewataka kuendelea kutoa maoni licha ya muda uliotengwa kupita.
Akizungumzia
suala hilo jana, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa
Chadema, John Mrema alihoji, “Msajili anawezaje kutueleza tupeleke maoni
wakati muda aliotupa kwa mujibu wa barua yake ya Agosti 28 umekwisha
tangu Septemba 10 na hajaitengua kuwa ameongeza muda.”
Katika
barua ya Agosti 28 iliyosainiwa na naibu msajili wa vyama vya siasa,
Sisty Nyahoza kwa niaba ya Jaji Mutungi iliyokuwa na kichwa cha habari
‘Maombi ya kupatiwa maoni kuhusu kutungwa kwa sheria mpya ya vyama vya
siasa’ ilitoa siku 14 kwa wadau kuwasilisha maoni yao.
Jaji
Mutungi alitoa ufafanuzi kwa umma Oktoba 13 baada ya gazeti hili
kuripoti kuhusu rasimu ya muswada wa sheria inayopendekezwa kuwa na
vifungu vinavyoelezwa na wadau wa siasa kwamba ni kandamizi na unalenga
kuviua vyama visivyo na wabunge, madiwani au wawakilishi.
Katika ufafanuzi wake, Jaji Mutungi ambaye hakukana moja kwa moja maudhui yaliyomo kwenye rasimu hiyo ambayo Mwananchi iliiona.
Alisema kilichofanyika kwa ofisi yake ni kuwataka wadau wa siasa kuwasilisha maoni yao kwa ajili ya kutungwa kwa sheria hiyo.
“Ofisi
ya msajili wa vyama vya siasa inaelewa kuwa kwa asilimia nyingi sheria
inatengenezwa na wadau, hivyo maoni yao ni muhimu katika kutungwa kwa
sheria,” alisema Jaji Mutungi akifafanua taarifa iliyoandikwa na gazeti
hili kisha akaongeza kuwa;
“Hivyo, kabla ya kuandaa
bango kitita la mapendekezo ya kutungwa kwa sheria mpya vya vyama vya
siasa, tuliona ni vyema kupata maoni kutoka kwa wadau ili mapendekezo ya
sheria yatokane na maoni ya wadau.”
Taarifa yake
ilifafanua, “Napenda kutumia fursa hii pia kuwaomba wadau wawasilishe
maoni yao kama tulivyowaomba katika barua yenye kumbukumbu namba
KA.231/322/01/174. Pia, nawaasa wajiepushe kuzua mijadala na propaganda
kwenye vyombo vya habari na mitandao isiyo na tija.”
Mwenyekiti
wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda alisema jana kuwa, “Ile
rasimu ilishatoka hata kabla ya maoni kuombwa tupeleke lakini
ninachoweza kusisitiza mimi mwenyekiti wa baraza sijui lolote na
najiuliza watu wameipata wapi na tena inasambaa mitandaoni.”
Shibuda
ambaye ni katibu mkuu wa Chama cha Tadea alisema, “Mawazo au fikra
zisizo na malumbano au kusigana hujenga Taifa imara. Mimi ni mwenyekiti
na sekretarieti na ofisi ya msajili sasa kama inaandaa kisiri siri
wanataka kupanda mbegu gani Tanzania.”
Barua yenye
kumbukumbu namba KA.231/322/01/174 aliyoielezea Jaji Mutungi iliyokwenda
kwa wadau kuwataka wawasilishe maoni yao ilitoa kipindi cha wiki mbili
ambazo ni siku 14 na kwa kuwa iliandikwa Agosti 28, muda wa mwisho
kuwasilishwa ilikuwa Septemba 10.
Barua hiyo ilieleza
wazo la kutungwa kwa sheria mpya ya vyama vya siasa linatokana na maoni
kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya sasa yaliyowasilishwa na
wadau kuwa mengi.
Pia, ilieleza kuwa endapo sheria
itarekebishwa bila kuandikwa upya, marekebisho yatakuwa mengi kuliko
sheria ya sasa na mtazamo wa sheria ya sasa utabadilika kabisa.
“Aidha,
pamoja na ukweli kwamba zoezi la kukusanya maoni ya wadau kuhusu
marekebisho ya sheria hii lilianza muda mrefu tangu mwaka 2013, ofisi ya
msajili wa vyama vya siasa inaomba maoni yenu yawasilishwe ndani ya
wiki mbili kuanzia tarehe ya barua hii ili kuhakikisha mchakato wa
kutunga sheria mpya ya vyama vya siasa unakamilika kabla ya kuanza kwa
msimu wa Uchaguzi Mkuu unaofuata,” ilieleza barua hiyo.
Zitto atoa ushauri
Kiongozi
wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alitoa ushauri kwa ofisi ya
msajili kuitisha kikao cha baraza la vyama ili kujadili aina gani ya
sheria wanaitaka, lakini hilo halikufanyika.
“Kama
msajili anasema si ya kwake basi atoe ya kwake tuone nani mkweli, mimi
nimezungumza na viongozi kadhaa wakiwamo wa Chadema na kuelezwa ndiyo
yenyewe na mimi nikashiriki kuichambua kidogo, sasa anaposema si ya
kwake atueleze yake ni ipi,” alihoji Zitto ambaye pia ni mbunge wa
Kigoma Mjini.
“Naendelea kusisitiza kuitishwa kwa kikao
cha Baraza la Vyama vya Siasa ili tujadiliane ni aina gani ya sheria
tunaitaka, je hii iliyopo imepitwa na wakati au kipi kipungue na kipi
kiongezeke.”
Akizungumzia kuvuja kwa rasimu hiyo,
mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya mje wa Chadema, Mrema
alisema inaweza kuwa imetolewa na watumishi wa ofisi ya msajili baada ya
kuona ni mbaya ili izue mjadala mapema.
“Lakini
anaposema tupeleke maoni, mbona barua yake ya Agosti 28 ilitoa wiki
mbili tu, tukipeleka maoni sasa anayapokeaje wakati muda ulishapita?”
alisema Mrema.
“Hiki kilichotokea kimemweka katika
wakati mgumu tunasubiri kuona hiyo rasimu atakayoitoa, je itafanana na
hii au itatofautiana?”
By Ibrahim Yamola, Mwananchi iyamola
By Ibrahim Yamola, Mwananchi iyamola
Post a Comment