ad

ad

YANGA YAIKAMATA SIMBA, YAIPIGA NJOMBE NYUMBANI KWAO



MASHABIKI wa Simba walikuwa wanaibeza sana Yanga, kwanza kwa sababu ya straika wao mpya, Ibrahim Ajibu kuonekana kama hana jipya, pili ni imani kwamba Wekundu hao wana timu bora zaidi msimu huu, lakini mambo yameshageuka. 

Kama ukizungumzia ubora, hadi sasa zimeshachezwa mechi mbili na tayari mabingwa watetezi, Yanga, wameshaikamata Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, ingawa Simba ipo juu kutokana na mabao yake 7-0 iliyofunga dhidi ya Ruvu Shooting. Lakini kama ukimzungumzia Ajibu, basi naye ameshaanza kuonyesha uwezo wake, kwani jana ndiye aliyeiokoa Yanga kwa kufunga bao safi la faulo ya moja kwa moja wakati mabingwa hao walipoanza kazi ya kutetea ubingwa wao kwa kuinyuka Njombe Mji bao 1-0 kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe. 

 
Ajibu alifunga bao hilo dakika ya 16 na kuonyesha kuwa bado kuna mengi mazuri yanaweza kutokea kwake. Njombe hawakuwa wapinzani rahisi kama wengi wanavyoweza kudhani na huenda timu nyingine kubwa zikaangukia pua kwenye uwanja ule, hasa ukizingatia hali ya hewa ni tofauti na sehemu nyingi nchini, kule kuna baridi kali. Tusubiri.
 
 Jana Mcongo ambaye amegeuka kipenzi kikubwa cha mashabiki wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi, alikuwa kama haonekani sana uwanjani lakini alifanya kazi kubwa mno. Kazi ya Tshishimbi katika mchezo wa jana ilikuwa ni kukaba na kutibua mipango ya wapinzani, tofauti na alivyozoeleka kupiga pasi na kushambulia. Hii inaonyesha kwamba huyu ni kiungo aliyekamilika. Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, baada ya mchezo aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana kupata ushindi.

 “Wametumia uzoefu wao kuweza kushinda licha ya kwamba hali ya hewa (baridi) ilikuwa ni tatizo kubwa. Tunashukuru tumepata pointi tatu na sasa tunajiandaa na mchezo unaofuata,” alisema Nsajigwa. Kwa upande wake, Kocha wa Njombe Mji, Hassan Banyai ambaye ni mzoefu kwenye Ligi Kuu Bara akiwahi kuzifundisha timu kama Moro United na Majimaji, alisema: “Nimesikitishwa na matokeo haya, vijana wangu walipambana vya kutoshakupata ushindi nyumbani.

 Tulifanya kosa moja ambalo lilitugharimu. Beki wangu alicheza faulo ambayo haikuwa na ulazima, na Yanga wakaitumia kupata bao.” Ushindi huo unawafanya Yanga kufikisha pointi nne katika michezo miwili, sawa na Simba. Njombe Mji yenyewe imebaki bila pointi yoyote katika michezo miwili iliyocheza, ilianza ligi kwa kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Prisons katika uwanja huohuo.  Yanga walipata kona tano, wakati Njombe walipata mbili.

 Lakini Yanga walichezewa faulo 24, wakati Njombe walichezewa faulo 23. Njombe Mji: David Kisu, Agathon Mapunda, Remy Mbuligwe/Innocent Jackson dk 62, Raban Kambole, Peter Mwangosi, Hassan Kapalata/Behewa Sembwana dk 80, Awadhi Salum, David Napa/Raphael Siame dk 47, Joshua John, Ditram Nchimbi na Noti Carry Masasi. 

Yanga: Youthe Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Kelvin Yondani, Andrew Vincent, Papy Kabamba Tshishimbi, Juma Mahadhi, Thaban Kamusoko/Raphael Daud dk 49, Donald Ngoma/ Obrey Chirwa dk 56, Ibrahim Ajibu na Emmanuel Martin.

No comments

Powered by Blogger.