ad

ad

TAMKO LA GLOBAL KUHUSU HABARI YA WEMA NA BWANA MPYA


WAPENZI wasomaji wetu, mara kadhaa Kampuni ya Global Publishers, wachapishaji wa Magazeti ya Ijumaa Wikienda, Uwazi, Risasi Mchanganyiko, Risasi Jumamosi, Amani, Ijumaa na Championi, tumekuwa tukieleza namna ambavyo habari zetu siku zote husimamia ukweli tupu. 

Kuandika uongo au habari za kumuonea mtu kwa uzushi wa jambo lisilo na ukweli, kwetu ni mwiko. Kama kinavyojieleza kichwa cha tamko hili, tunalazimika kufafanua habari kubwa iliyoibuliwa na Gazeti la Ijumaa linaloingia mitaani kila Ijumaa lililotoka Ijumaa iliyopita ya Septemba 22 hadi 28, 2017, juu ya staa Wema Sepetu kubambwa faragha na anayedaiwa ndiye mwanaume wake mpya wa sasa.
Baada ya kutoka kwa habari hiyo, kumeibuka makundi ya aina mbili; -moja linadai kuwa habari hiyo ilitokana na picha za sinema mpya ya Wema na siyo kama ambavyo Gazeti la Ijumaa lilivyoripoti kama habari ya kiuchunguzi.
Pili, kuna kundi la watu ambao wameanza kujitokeza na kusema kuwa habari hiyo ni ya uongo tu bila hata kueleza sababu zao za kwa nini wanasema kuwa habari hiyo ni ya uongo.
Jambo hili la kuambiwa kuwa habari zetu ni za uongo bila mtu kueleza kwa nini anaamini kuwa habari hiyo ni ya uongo, limekuwa likitukwaza mno na hasa pale tunapokuwa na ushahidi wote juu ya habari husika na kuuanika kwa kuambatanisha na habari hiyo.
Lakini wale wanaojifanya wataalam wa kutoa maoni mitandaoni huishia kusema tu ni habari ya uongo kwa kuwa wana vidole vya kuandika maoni na Mungu amewajalia kujua kusoma na kuandika. Inaudhi na kukera sana!
Tukirudi kwenye habari ya Wema na bwana mpya, kwanza; -habari hiyo haina uhusiano wa hata chembe na sinema mpya ya Wema kwani tunao ushahidi wa kutosha wa matukio tuliyoyanasa ya ndani na nje ya nchi ambayo hayawezi hata kuwekwa behind the scene, achilia mbali ndani ya sinema yenyewe.
Global haichapishi habari yoyote pasipokuwa na ushahidi. Tunatambua kwamba mbali na kulipishwa fidia baada ya mhusika kutushtaki na kushinda mahakamani, tunaweza kuchukuliwa hatua nyingine kali za kisheria zikiwemo hata za kufungiwa gazeti.
Hivyo kila habari tunayoipata lazima tujiridhishe kwa kina kabla ya kuichapisha. Habari ya Wema tulijiridhisha na kuwa na uhakika wa asilimia mia kwamba si habari ya uongo, si filamu na Bakari ndiyo mwandani wa Wema ambaye wengi walikuwa hawamjui.
Mwanaume huyo hana uhusiano wowote na sinema na kwamba asingependa kuhusiashwa na masuala hayo hata kidogo- ni mfanyabishara.

Wema Anaswa Live Kwenye Sofa Kochi na Kidume Kipya -Video

Pili; kwa wanaosema habari hiyo ni ya uongo, kwa nini wasilichukulie hatua stahiki Gazeti la Ijumaa ikiwemo kulifikisha mahakamani au mamlaka nyingine zinazostahili?
Tunayo mifano mingi ya habari ambazo mara nyingi tukishaziandika na kwa kuwa anayeandikwa ana wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii, basi huishia kudai kuwa ni habari za uongo, lakini wanapotakiwa kwenda kwenye vyombo vya kisheria ili kupata haki zao, huingia mitini au kuomba yaishe kwa maelezo kuwa walikanusha ili ‘kuua soo’ lakini habari ni ya ukweli mtupu.
Hivyo kwa maelezo hayo, katika habari ya Wema na bwana mpya ya Gazeti la Ijumaa, kwa yeyote anayedai kuwa ilikuwa ni sinema au mwenye ushahidi kuwa ni habari ya uongo, basi amwage ushahidi au aende mahakamani, nasi tupo tayari kumlipa fidia. Lakini ukweli ni kwamba tumechoshwa na watu ambao mara zote husema kuwa habari zetu ni za uongo bila kuwa na ushahidi wowote ilimradi tu kutuaribia sifa njema ya kuwahabarisha watu wetu tuliyojijengea. Tuache roho chafu za namna hiyo!
Kwa kuongezea, wale wote wanaochonga mitandaoni, wajiulize kwa nini Wema mwenyewe hakanushi mitandaoni? Ana wafusi wengi wanaomfuatilia na amekuwa akikanusha kama ameandikwa habari isiyokuwa na ukweli, kwa nini hii hakanushi? (Jibu nadhani sasa mnalo).
Kwa kuwa sisi tunaamini tulichoandika ni sahihi na hakina hata chembe ya uongo, tupo tayari kumwaga ‘silaha’ zetu zote tulizonazo pale itakapobidi.
Mungu ibariki Tanzania!
Nawasilisha,
Sifael Paul –Mhariri
Gazeti la Ijumaa.

No comments

Powered by Blogger.