Spika aeleza jinsi Lissu alivyojeruhiwa kwa risasi tano
Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi kati ya 28 hadi 32, huku tano zikimpata mwilini.
Lissu alishambuliwa jana Alhamisi kabla hajashuka kwenye gari baada ya kumaliza kikao cha Bunge na alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kusafirishwa saa sita usiku, kuelekea Hospitali ya Aga Khan ya Nairobi, Kenya.
Akitoa taarifa ya tukio hilo kwenye kikao cha Bunge leo Ijumaa, Ndugai amesema risasi mbili zilimpata Lissu kwenye miguu, mbili tumboni na moja kwenye mkono.
Amesema watu wasiofahamika wakiwa kwenye gari aina ya Nissan ambalo halijajulikana walimpiga risasi kisha kutoweka.
“Baada ya tukio hilo watu hao walikimbia,” amesema Ndugai. Alisema Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa kutumia gari la familia ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kwa kuwa wanaishi jirani.
“Alipofika hospitali aliingizwa kwenye chumba cha upasuaji na kufanyiwa upasuaji ili kuzuia damu kuendelea kutoka katika majeraha aliyokuwa ameyapata,” amesema Ndugai.
Amesema upasuaji huo uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya akishirikiana na madaktari wengine.
“Baada ya upasuaji tulielezwa kuwa hali yake iliendelea kutengemaa na anaweza kusafirishwa kwa matibabu zaidi,” amesema.
Ndugai amesema ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ilishaandaa ndege saa 10:30 jioni kwa ajili ya kumchukua mgonjwa na kumpeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
Hata hivyo, amesema baada ya kushauriana na familia na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe waliona ni vyema mgonjwa huo apelekwe katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi.
“Hivyo kwa kushirikiana na ofisi ya Bunge ilipatikana ndege nyingine ya Flying Doctors na kuondoka na mgonjwa saa sita usiku, kuelekea Nairobi,” amesema.
Amesema tukio hilo liliripotiwa polisi ambako waliahidi kufanya msako kuwatafuta wahalifu hao na Serikali itatoa taarifa kamili kwa kuzingatia utaratibu wa kibunge.
Spika Ndugai amesema tukio hilo ni la kwanza la aina yake tangu Bunge lilipohamia Dodoma na kwamba, haijawahi kutokea mbunge akashambuliwa kwa risasi.
Amesema pia haijawahi kutokea tukio la aina hiyo wakati Bunge likiendelea na vikao, hivyo amewaomba Watanzania kuwa na subira wakati vyombo vya dola vikiendelea na kazi.
“Utaratibu wetu wa kibunge wa matibabu ambao ndiyo utaratibu wa Watanzania wote, baada ya mwenzetu kupata tatizo hili tulikuwa tumeshaagiza ndege kumpeleka Muhimbili,” amesema.
Amesema ingekuwa anatakiwa kusafirishwa nje, Serikali ina mkataba na Hospitali ya Apollo ya India na kwamba, Lissu amepelekwa Nairobi kwa sababu familia imeomba.
“Lakini kwa nini mwenzetu alipelekwa Nairobi, ni kwa sababu familia iliomba. Nimnukuu Mheshimiwa Mbowe kwa niaba yake si kwamba wana shaka na umahiri na uwezo wa madaktari wetu,” amesema.
Amewataka Watanzania kuendelea kumuombea kiongozi huyo katika kipindi hiki kigumu.
Amewashauri wabunge walioanza kutuma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kutumia maneno ya hekima badala ya kuendelea kuchonganisha pande mbili.
Post a Comment