Serikali Kulikarabati Jengo Alilolazwa Lissu
Lissu alipigwa risasi Septemba 7 mwaka huu na kupelekwa hospitalini hapo kwa ajili ya huduma ya utengemavu kabla ya kupelekwa Nairobi nchini Kenya ambapo hadi sasa anaendelea matibabu.
Akizungumza wakati alipoitembelea hospitali hiyo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Seleman Jafo amesema kuwa ukarabati huo unalenga katika kukarabati miundombinu ili kuendana na mahitaji ya mji wa Dodoma kwa sasa.
“Hatuwezi kuvumilia hili tunataka tulete fedha tuikarabati ili iendane na hali halisi ya mahitaji ukizingatia sasa hivi Dodoma ni mji mkuu.
Tunataka viongozi na wananchi waweze kutibiwa katika hali nzuri na ya kisasa zaidi ya hapa,”amesema.
Hatua hiyo ilifuatia Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Caroline Damian jengo hilo limekuwa likitumika kufanya upasuaji kwa wastani wa watu 500 kwa wiki.
“Kwa siku tumekuwa tukifanya upasuaji kwa watu kati ya 15 na 20, ili kukidhi mahitaji imebidi kubalisha vyumba vingine ambavyo havikuwa vya upasuaji kuwa vya upasuaji,”amesema.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Kiologwe amesema kwamba awali wakati jengo hilo linajengwa kuna aina ya upasuaji ambazo zilikuwa hazifanyiki mkoani hapa lakini sasa zinafanyika.
“Zamani kuna aina ya upasuaji ulikuwa haufanyiki lakini sasa unafanyika. Tuna madaktari wazuri wanaojituma lakini changamoto ipo katika miundombinu,”amesema.
Kuhusu ujenzi wa jengo la wakinamama na watoto, Jafo amesema ameridhika na kazi inayoendelea bali amemtaka mkandarasi kuhakikisha kazi hiyo inakamilika Oktoba 20 ili lianze kutumika.
“Nimewapa maelekezo wahakikishe kuwa jengo hilo linakuwa na mfumo wa gesi ya oksijeni ili kuepuka wahudumu ama wauguzi kukimbizana na mitungi mara kunapokuwa na mahitaji ya kuokoa maisha ya mama na mtoto,”amesema.
Meneja Msaidizi wa Mradi huo, Mhandisi Frank Mabubu amesema jengo hilo limekamilika kwa asilimia 85 na kwamba ujenzi utakamilika Oktoba 20.
Post a Comment