ad

ad

Ni Vigumu Kumuacha Umpendaye Lakini Ikibidi, Muache!



PENZI linapoota mizizi, ni vigumu kulivunja. Kila mmoja anafikiria mahali walipotoka, anaumizwa na upendo aliouwekeza. Hakubaliani hata kidogo na sababu yoyote inayotaka kuwafanya waachane.

Anafikiria mipango waliyopanga, ahadi waliyoiweka katika uhusiano wao, akili haitaki kuachana. Mawazo yake anayapeleka katika mapito magumu waliyoyapitia, anakumbuka na vile vipindi vizuri (good time) walivyopitia, moyo unakuwa mzito kukubali kuachana.


Ndiyo maana katika maisha ya uhusiano, wengi hujikuta wakifanya jaribio la kutaka kuachana lakini hujikuta wakishindwa. Wapendanao wanateswa na historia ya mapito yao. Kila mmoja anaguswa na mazuri aliyotendewa na mwenzake. 


Anayefanya uamuzi wa kumuacha mwenzake, anakuwa na hoja zake za msingi lakini zote zinayeyuka pale tu mwenzi wake atakapomwomba msamaha. Wakati mwingine anaweza kuwaza kufanya hivyo lakini akajikuta ametengua uamuzi wake pindi tu atakapojipa muda wa kutafakari safari ya uhusiano wao.


Akili inataka lakini moyo unakataa. Yawezekana anayempenda akawa anamtesa penzini lakini kwa sababu moyo wake umependa, anapambana na hali ya moyo wake. Mwenzi wake yawezekana akawa na tabia sugu ambayo miaka nenda rudi ameshindwa kubadilika lakini kwa sababu anampenda, anaumia tu. 


Bahati mbaya sana, yule anayependwa naye anapojua anapendwa kiasi hicho huongeza kiburi. Anaamini anapendwa, anazidisha vituko kila kukicha. Anaamini hawezi kuachwa kwa sababu anapendwa.


Marafiki zangu, kuna umuhimu wa kufanya maamuzi magumu katika uhusiano ili uweze kufikia kwenye kilele cha mafanikio. Ni kweli mapenzi ni hisia, yanaponzwa na moyo unaohifadhi hisia hizo lakini kama mwanadamu ni vizuri ukachagua kuwa huru. 


Sina maana kila unapokutana na tatizo katika uhusiano basi umuache mpenzi wako lakini kuna nyakati inabidi suala hilo litokee. Unapojiridhisha kwamba wewe na mwenzi wako mnashindwa kuendana tabia, hampikiki chungu kimoja, ni bora msitishe safari. 


Maisha ya uhusiano yanahitaji upendo wa dhati. Kila mmoja aguswe na uhusiano husika. Asiwepo mmoja wenu ambaye anaona ni kama anamsaidia mwenzake kuwa naye katika uhusiano. Mnajenga mwamba wa upendo kati yenu, kila mmoja aguswe na uwekezaji huo. 


Unapofika kwenye kipindi ambacho uhusiano wenu unabaki kuwa tu jina kwamba fulani mpenzi wake ni fulani, hakuna mwenye hamu wala upendo na mwenzake na mnapitia kwenye hali hiyo mara kwa mara, unapaswa kuanza kutafakari namna ya kumuacha yule umpendaye. 


Mkiwa mnapitia kwenye vipindi vya ugomvi mara kwa mara, mmepoteza kabisa hamu ya mapenzi kuna sababu gani ya kuendelea? Hata kama uhusiano wenu umedumu kwa muda mrefu, mna mipango ya kufika mbali, kuna kila sababu ya mmoja wenu kufanya uamuzi sahihi. 


Unapoona mnaishi kwenye mazingira ya kutoelewana kwa muda mrefu, kila mnapojaribu kutafuta suluhu mnashindwa, bora muachane. Kama mnashindwa kupata suluhu kwa kila mmoja wenu kujiona yupo sahihi, mwenzake ndiyo mkosaji hatma yenu itakuwa ni nini? 


Pima uzito wa tabia mnazotofautiana, linganisha na historia ya majanga mnayopitia mara kwa mara na huoni uwezekano wowote wa kurekebisha hali hiyo, kiroho safi tu unashauriwa kumuacha yule umpendaye. 


Utapata maumivu kwa muda lakini mbeleni utapata faraja. Unapowekeza upendo na mtu ambaye unaona mbeleni kuna tatizo ambalo miaka nenda rudi umekosa majibu ya tatizo hilo, chagua kuwa huru. Kaa peke yako na utampata mwingine ambaye atakuwa sahihi kwako.

No comments

Powered by Blogger.