Mbowe Afunguka Sakata la Tundu Lissu Kushambuliwa kwa Risasi
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, ameongea na wanahabari nje ya Hospitali ya Mkoa wa Dodoma juu ya maendeleo ya shambulio lililofanywa leo dhidi ya Tundu Lissu, ambapo amesema tukio hilo lilimtokea mbunge huyo alipokuwa anarudi nyumbani kwake kwa ajili ya chakula cha mchana baada ya kumalizika kwa kikao cha bunge cha asubuhi.
Aliendelea kusema kwamba wakati akirudi nyumbani kulikuwa na gari linamfuata kwa nyuma na ghafla mtu asiyefahamika akiwa ndani ya gari hilo alitoa bunduki aina ya SMG na kuanza kulishambulia gari hilo la Lissu.
Kuhusu hali ya Lissu, kiongozi huyo wa Chadema alisema, yuko chumba cha upasuaji (theatre) kwa ajili ya kumtoa risasi zilizoingia tumboni na sehemu nyingine za mwili.
Kutokana na tukio hilo, Chadema hakiwezi kumnyooshea mtu yeyote kidole cha mashitaka au tuhuma ila kimelipokea kwa huzuni baada ya kuona kiongozi akishambuliwa kwa risasi mchana kweupe.
Mbowe amewaomba wabunge, viongozi mbalimbali na Watanzania wote kumwombea Lissu atoke salama chumba cha upasuaji.
Kiongozi huyo pia aliwaomba wananchi wasubiri ripoti za madaktari na polisi kwa taarifa zaidi.
Post a Comment