Chelsea, Arsenal Sare, Man United Spidi 100 Yaipiga Everton Bao 4-0
DAVID Luiz jana alipewa kadi nyekundu wakati timu yake ya Chelsea ilipotoka suluhu na Arsenal, huku Man United wakiichapa Everton bao 4-0. Katika mchezo wa kwanza, Arsenal walikuwa ugenini kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, lakini wakaonyesha kiwango cha hali ya juu sana huku wakikosa nafasi kadhaa za wazi kipindi cha kwanza. Hata hivyo, timu zote mbili haziwezi kufurahia sare hiyo kutokana na upinzani mkali uliopo kwenye Ligi Kuu England kwa sasa.
Arsenal ambao waliifunga Chelsea kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la FA mwaka jana na kuwachapa tena kwenye Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimu huu, walionekana kumiliki mchezo huo kwa asilimia kubwa sana mwanzoni. Lakini Chelsea nao waliibuka kipindi cha pili na kukosa nafasi kibao. Hii ni sare ya kwanza kwa timu hizo mbili kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, baada ya kupita miaka 12. Awali, Arsenal ilikuwa ikikumbana na kichapo uwanjani hapo.
Zikiwa zimebaki dakika chache kabla mchezo huo haujamalizika, Luiz alipewa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu mbaya beki wa Arsenal, Sead Kolasinac, ambaye alionyesha uwezo wa hali ya juu sana kwenye mchezo wa jana. Matokeo haya yamewafanya Chelsea kukaa nafasi ya tatu kwenye ligi hiyo wakiwa na pointi 10 sita nyuma ya vinara Man United, huku Arsenal wakiwa nafasi ya 12 na pointi saba.
Katika mchezo wa pili, Man United walionyesha kuwa wanaweza kufanya vizuri msimu huu baada ya dakika ya nne tu Antonio Valencia kufunga bao safi kwa mashine kali. Hili ni bao la kwanza kwa beki huyo kufunga kwenye Uwanja wa Old Trafford kwa kipindi kirefu.
Everton ambao hawana msimu mzuri walianza kubadilika baada ya kufungwa bao hilo, lakini uwezo wa mastaa wao akiwemo Wayne Rooney walishindwa kufurukuta na kumruhusu Jese Lingard kufunga bao la pili katika dakika ya 84 baada ya kupata pasi ya Romelu Lukaku.
Lukaku alikuwa akicheza dhidi ya timu yake ya zamani, huku Rooney naye akirejea Old Trafford kwa mara ya kwanza tangu alipoondoka na kujiunga na Everton. Romelu Lukaku na Anthony Martial (penalti) walifunga mabao ya haraharaka dakika ya 89 na 92. United kwa sasa wapo kileleni na pointi 13, sawa na Man City huku Everton wakiwa katika nafasi ya 17
Post a Comment