ad

ad

Uchaguzi Kenya: Matokeo Ya Urais Yasubiriwa - LIVE


 

Habari za hivi pundeIEBC: Twasubiri fomu za maeneo bunge mawili




Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Uchaguzi Ezra Chiloba amesema tume hiyo sasa imefanikiwa kupata fomu za matokeo kutoka maeneo bunge 288.
Amesema Fomu 34B za maeneo mawili bado haziko tayari. Hata hivyo amesema wameziona fomu hizo na wamewasiliana na wasimamizi wa uchaguzi maeneo hayo mawili.
Hata hivyo, kulikuwa na mambo yaliyofaa kufafanuliwa kwenye fomu hizo.
Bw Chiloba amewaomba Wakenya kuwa na subira.
"Ni muhimu zaidi tuwe sahihi kuliko kuharakisha," amesema.
Ameeleza kuwa tume itafanya kikao baadaye kikiongozwa na mwenyekiti Wafula Chebukati kutoa maelezo zaidi.


Taarifa ya IEBC yasubiriwa, Jubilee wajiandaa KICC

 

Tume ya uchaguzi ilikuwa imeahidi kutoa taarifa zaidi kuhusu fomu za matokeo ya uchaguzi kutoka maeneo bunge ambazo zilikuwa bado hazijapokelewa kufikia sasa.
Hayo yakijiri, chama cha Jubilee kimeendelea kuandaa ukumbi wa mikutano wa KICC.
Wafuasi wa Jubilee wanaendelea kufika, na wengine wanatumia fursa hiyo kuuza bendera.


Habari za hivi pundeNaibu Rais William Ruto awasili Bomas

Naibu Rais William Ruto, ambaye ni mgombea mwenza wa Rais Uhuru Kenyatta amewasili katika ukumbi wa Bomas.

Kalonzo Musyoka awasili Bomas

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Kenya (IEBC) inatarajia kupokea fomu zote za matokeo kutoka vituo vya kupigia kura kufikia leo saa sita mchana. Tangazo la mshindi wa urais linatarajiwa kutolewa baada ya tume hiyo kuhakiki fomu hizo.

Mgombea mwenza wa urais wa Bw Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, amewasili katika ukumbi wa Bomas of Kenya unaotumiwa kujumlishia matokeo.Taarifa zinasema pia kwamba Bw Odinga yuko Bomas ingawa hajaonekana.

Upinzani wasisitiza hawakubali matokeo ya IEBC


Viongozi wa muungano wa upinzani Nasa, wakiwemo kakake mgombea urais Raila Odinga, Oburu Oginga, wamewahutubia wanahabari na kusisitiza kwamba hawayakubali matokeo ya awali yanayotangazwa na IEBC katika mtandao wake.

Habari za hivi pundeChebukati: Bado hatujatokea fomu kutoka maeneo 17

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Wafula Chebukati amesema tume hiyo kufikia sasa imepokea Fomu 34B, fomu za matokeo kutoka maeneo bunge kutoka maeneo 273.
Tume hiyo ilikuwa imetarajia kupokea fomu hizo kufikia saa sita leo mchana.
Matokeo kutoka kwa maeneo 17 bado yanasubiriwa, amesema akihutubia wanahabari Bomas.
Miongoni mwa maeneo ambayo matokeo hayajafika kwa tume ni Nyali, Mvita, Lagdera, Wajir Mashariki, Mandera Magharibi, Imenti Kaskazini, Kiminini, Kitui Mashariki, Ndaragwa, Mathira, Turkana Kaskazini, Kasipul, Ndhiwa, Mogirango Kaskazini na Embakasi Mashariki.
"Tutawapasha kuhusu hatua tulizopiga saa nane unusu adhuhuri.
Kwa sasa, tutarudi faraghani na kushauriana na maajenti waangalizi na maafisa wengine,” amesema.
"Nawaomba Wakenya kuwa na subira, tafadhali rejeeni kazini tukiendelea kukamilisha kazi hii.”

'Wanawake walifanya vyema sana uchaguzini

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Jinsia Wilfred Lichuma amesema tume hiyo imefurahishwa sana na idadi ya wanawake walioshinda nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi uliofanyika Jumanne.
Kwa mara ya kwanza kuna magavana watatu waliochaguliwa ikilinganishwa na mwaka 2013 ambapo hakuna mwanamke hata mmoja aliyechaguliwa gavana.
Wanwake 3 pia wamechaguliwa kuwa maseneta na 23 kama wabunge.
Kuna wanawake 97 waliochaguliwa kuwa wawakilishi wa wadi.
Soma zaidi: Wanawake washinda nyadhfa za Ugavana Kenya

Hali ukumbi wa Bomas yabadilika matokeo yakisubiriwa

Maafisa wakuu wa serikali pamoja na mabalozi wameanza kuwasili ukumbi wa Bomas ambako kuna kituo cha taifa cha kujumlishia na kutangazia matokeo ya urais, ishara kwamba tangazo muhimu linasubiriwa.
Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Amina Mohammed na washirika wengine wakuu wa Rais Uhuru Kenyatta wamewasili Bomas.
Mabalozi wa Marekani na Uingereza pia wamewasili.
Kunashuhudiwa shughuli nyingi na usalama umeimarishwa pamoja na hali kuonekana kubadilika katika ukumbi huo.
Tume ya uchaguzi IEBC ilikuwa imetangaza kwamba inatarajia kupokea matokeo yote kutoka vituo vya kupigia kura kufikia leo saa sita mchana.
Mwenyekiti wa tume hiyo anatarajiwa kutangaza matokeo baadaye baada ya kuhakikiwa kwa fomu za matokeo.
Matokeo ya awali kwenye tovuti ya tume hiyo yanaonesha Rais Kenyatta akiongoza kwa takriban asilimia 10 ya kura zilizohesabiwa dhidi ya Bw Odinga.
Tume ya uchaguzi ina siku saba kisheria kutangaza matokeo ya urais.


Hali ilivyo KICC ukumbi wa mkutano wa Jubilee

Hivi ndivyo hali ilivyo ukumbi wa Jumba la Kimataifa la Mikutano la Jomo Kenyatta (KICC) ambako chama cha Jubilee kinatarajiwa kuwa na mkutano baadaye leo.

CHANZO: BBC SWAHILI

No comments

Powered by Blogger.