Taarifa kwa Wote Walioomba na Watakaoomba Kazi Serikalini
Mtakumbuka Serikali katika mwaka wa fedha uliomalizika 2016/2017 iliahidi kutoa Ajira serikalini zaidi ya 52,000 kwa
Watanzania, ambapo katika siku za hivi karibuni Serikali imekuwa ikitoa
vibali vya kuajiriwa watumishi wa kada mbalimbali ikiwemo Waalimu wa
Sayansi, Kada za Afya na maeneo mengine kulingana na mahitaji.
Kama mnavyofahamu mojawapo ya jukumu
la msingi la kuanzishwa kwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa
Umma ni pamoja na kuendesha mchakato wa ajira kwa niaba ya waajiri
mbalimbali na hatimae kuwapangia vituo vya kazi waombaji kazi wanaofaulu
usaili, ambapo tangu Serikali ilipoanza kutoa vibali baada ya
kusitishwa tumeshapokea jumla ya vibali kwa ajili ya mamlaka za Ajira 239, kati ya hivyo vipo ambavyo vimeshafanyiwa kazi na vingine mchakato wake unaendelea katika hatua mbalimbali.
Aidha, baadhi ya vibali ambavyo mchakato wake umeshakamilika ni pamoja na kibali cha Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambayo tulipokea jumla ya maombi ya kazi 6,852 na walioitwa kwenye usaili kutokana na kukidhi vigezo walikuwa 2,949, kwa upande wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) maombi yaliyopokelewa ni 9,022 na walioitwa kwenye usaili ni 1,550.
Aidha, miongoni mwa taasisi ambazo mchakato wake bado unaendelea ni pamoja na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) ambapo jumla ya maombi ya kazi 2,273 yamepokelewa na waliokidhi vigezo vya kuitwa kwenye usaili ni 144, maombi yaliyopokelewa kwa ajili ya Wakala wa Serikali Mtandao (e-GA),yalikuwa 5,732 na walioitwa kwenye usaili ni 4,054.
Taasisi nyingine ambayo mchakato wake unaendelea ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo ina nafasi wazi za kazi 400 na jumla ya maombi ya kazi 56,815 yamepokelewa
kupitia mfumo wa uwasilishaji wa maombi ya kazi kwa njia ya
kielektroniki “Recruitment Portal’ na baada ya kufanyiwa kazi waliokidhi
vigezo kwa mujibu wa sifa zilizokuwa zimeainishwa katika tangazo la
kazi husika na kuitwa kwenye usaili ni 29,674.
Pamoja na nia ya Serikali ya awamu ya
tano kuendelea kuhakikisha Watanzania wanaohitimu katika fani
mbalimbali ndani na nje ya nchi wanapata kazi, zipo changamoto kadhaa
ambazo zimekuwa zikijitokeza wakati wa utekelezaji wa mchakato wa ajira
ambazo hupelekea baadhi ya waombaji kazi kutoitwa kwenye usaili. Kama
mlivyoona katika takwimu zilizoainishwa hapo juu katika baadhi ya
taasisi ambazo mchakato wake umeshafanyiwa kazi kupitia Sekretarieti ya
Ajira.
Aidha, tungependa mzifahamu
changamoto hizo ili mtusaidie kuendelea kuelimisha wadau wetu tukitambua
mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kuelimisha na kuhabarisha
jamii ili nao waweze kuzifahamu, kuzielewa na kuzifanyia kazi ili
nafasi nyingine za kazi zitapotangazwa waweze kuziepuka na kuwa katika
nafasi nzuri na uhakika wa kuweza kuitwa kwenye usaili na hatimae kupata
kazi wanazoomba.
Changamoto hizo ni pamoja na Waombaji
wengi kutokufahamu namna ya kuandika barua za maombi ya kazi,
kutoainisha nafasi wanazoomba, kutokusaini barua za maombi ya kazi
wanazoziwasilisha, kutokuthibitisha nyaraka zao (certify) katika
wanavyotakiwa kufanya hivyo, hususan kwa waombaji waliosoma nje ya nchi
kutowasilisha vyeti vyao vya elimu kwa ajili ya uthibitisho wa
kutambulika elimu walizozipata katika mamlaka husika kama NECTA, NACTE
na TCU kabla ya kuzituma Sekretarieti ya Ajira.
Sambamba na hizo, ni baadhi ya
waombaji kutokuambatisha nyaraka za elimu hususani cheti cha kidato cha
nne na sita au astashahada, stashahada, shahada, shahada ya uzamili na
kuendelea kulingana na elimu waliyonayo.
Baadhi yao kutozingatia vigezo vya
nafasi iliyotangazwa, ikiwemo kudanganya sifa wakidai wamemaliza shahada
ya fani fulani ilihali hawajasoma shahada ya aina hiyo, au mwombaji
mwenye elimu ya astashahada kuomba kazi ya shahada, kuandika barua moja
ya kuombea kazi kwa nafasi tofauti, kutojua namna ya kuandika wasifu
binafsi (CV), waombaji wengi kuandika wadhamini wachache ambao ni ndugu
zao badala ya idadi ya wadhamini inayotakiwa ambao wanauwezo wa kutoa
taarifa zao za kitaaluma na kikazi kwa uhuru pindi wanapotakiwa kufanya
hivyo.
Changamoto nyingine ni baadhi ya
waombaji kazi wanapoelekezwa kuwasilisha picha za utambulisho wao
“Pasportsize” wao wanapakia kwenye mfumo picha tofauti bila kujali
mavazi wanayovaa, mandhari iliyotumika na aina za picha wanazotuma.
Changamoto nyingine ni ya baadhi ya
waombaji kazi ambao ni Waajiriwa katika Utumishi wa Umma kutokupitisha
barua za maombi yao kwa Waajiri wao kabla ya kuziwasilisha Sekretarieti
ya Ajira, pamoja na baadhi ya waombaji kuja kwenye usaili wa mchujo au
mahojiano bila ya vyeti vyao halisi kama inavyoelekezwa.
Nyingine ni waombaji wengi
kutozingatia masharti ya jumla ikiwemo, kuwasilisha nyaraka pungufu
mfano kutokuwasilisha barua ya maombi ya kazi, kutokuambatisha baadhi ya
vyeti vya taaluma, kuwasilisha maombi, kwa njia tofauti na ile
iliyoelekezwa kwenye tangazo la kazi, kuwasilisha taarifa za uongo
mfano, wasifu binafsi usio wa ukweli, kutopakia taarifa sahihi (upload)
katika maeneo husika ya mfumo wa kuombea kazi pamoja na kupakia vyeti
visivyokamilika mfano “result slips, partial transcript, provisional
result, progress report, statement of result”.
Tumeainisha baadhi ya mapungufu hayo
hapo juu ili wahitimu ambao ni waajiriwa watarajiwa wafahamu hivi sasa
soko la ajira ni la ushindani mkubwa na linahitaji mwombaji aliyejiandaa
vizuri.
Tunaamini endapo muombaji yeyote wa
kazi mwenye sifa na ambaye anazingatia maelekezo yanayotolewa na
Serikali kwenye maombi ya kazi anayowasilisha ataitwa kwenye usaili.
Kwakuwa wale ambao wahazingatii kikamilifu mara nyingi hukosa fursa ya
kuitwa katika usaili na kuikosa nafasi anayotarajia na hatimae
kusababisha malalamiko.
Aidha, ni vizuri wakafahamu Serikali
inatumia gharama kubwa katika kuendesha mchakato wa Ajira hadi
kukamilika, na ni nia ya Serikali kuona kila nafasi inayotangazwa
inapata mwombaji makini mwenye sifa, ujuzi na weledi wa kutosha kuweza
kutumikia Taifa lake.
Mwisho, nimalizie kwa kutoa rai kwa
waombaji kazi wote wanaomba kazi serikalini kujiandaa kikamilifu pamoja
na kuzingatia masharti ya matangazo husika kwa kuhakikisha
wanaambatanisha nyaraka zinazotakiwa na kuomba nafasi za kazi ambazo
wana sifa stahiki.
Niwaahidi kuwa Sekretarieti ya Ajira
itaendelea kutoa elimu zaidi na kuwataka wale wenye changamoto ambazo
wanaona wanahitaji msaada wasisite kuwasiliana na taasisi kwa kufika
katika Ofisi za Sekretarieti ya Ajira au kupitia mawasiliano yetu katika
mitandao ya kijamii kama facebook.com/sekretarietiajira,
twitter.com/psrsajira, instagram:psrsajira au kwa simu za kiganjani
kupitia namba 0784398259/0687624975.
Imetolewa na; Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, tarehe 24 AGOSTI, 2017.
Post a Comment