JPM: Tumebaini Mengi ya Hovyo, TAKUKURU Msiwe na Kigugumizi

Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amewataka viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) kutokuwa na kigugumizi cha kuchukua hatua pale wanapokuwa na
ushahidi dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo tarehe 28 Agosti, 2017 alipotembelea
na kuzungumza na wafanyakazi wa TAKUKURU katika ofisi za makao makuu ya
taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam.
“Kuna
mambo mengi ya hovyo yanafanyika, tumehakiki pembejeo za ruzuku na
kubaini madai ya Shilingi Bilioni 48 ni hewa, tumebaini wafanyakazi hewa
zaidi ya 19,500, tumebaini kaya masikini hewa 56,000 zilizopaswa kupata
fedha TASAF, tumebaini wanafunzi hewa 5,850 waliotakiwa kupata mkopo,
kuna vichwa vya treni 11 vimeletwa bila kuwepo mkataba na mengine mengi,
haya yote yanafanyika kwa rushwa, nataka kuwaona mnachukua hatua
stahiki” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli amesema ana imani na TAKUKURU na amewataka wafanyakazi wa
taasisi hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uzalendo na uadilifu
mkubwa na kwamba Serikali itafanyia kazi changamoto zinazowakabili.
Katika
mkutano huo Mhe. Rais Magufuli amepokea masuala mbalimbali kutoka kwa
wafanyakazi wa TAKUKURU na amewaahidi kuwa Serikali itayafanyia kazi ili
kuboresha maslahi yao na mazingira ya kazi.
Mkutano
huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Anjellah Kairuki, Katibu Mkuu Dkt.
Laurian Ndumbaro na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw. Valentino Mlowola.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi
na wataalamu wanaosimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ujenzi
wa mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge
Hydropower Project), ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa
(Standard Gauge) na ujenzi wa barabara mbalimbali nchini, Ikulu Jijini
Dar es Salaam.
Katika
Mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Matogolo
Kalemani ametoa taarifa ya maandalizi ya awali ya kuanza kwa ujenzi wa
mradi wa umeme wa Stiegler’ Gorge na kwamba zabuni ya kuanza kwa ujenzi
huo itatangazwa tarehe 30 Agosti, 2017.
Mhe.
Rais Magufuli amesema fedha za kuanza kwa ujenzi wa mradi huo mkubwa
utakaozalisha Megawatts 2,100 zitakazoingizwa katika gridi ya Taifa
zipo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Agosti, 2017

Post a Comment