Vanessa Mdee Video Yako ya Kisela Ft. Mr. P umekopi kutoka kwa Keri Hilson - Energy
NYIMBO nyingi za Bongo Fleva kwa sasa zinabebwa na ubora wa video ambayo msanii anaifanya. Hapa unaweza kukuta wimbo wa kawaida ambao hata haueleweki lakini inatumika gharama kubwa kuhakikisha video yake inakuwa ya kiwango kikubwa. Suala hilo limewafanya wasanii wengi Bongo kufukuzana na hali hiyo, jambo ambalo limesababisha baadhi yao kuchukua mawazo ya video za wasanii wenzao na kuyaingiza kwenye video zao, yaani kukopi na kupesti. Awali, suala hilo lilianza kama utani hivi lakini kwa sasa limejichimbia mizizi na kukomaa. Idadi ya wasanii ambao wanapesti mawazo ya wenzao katika video zao ni kubwa kuliko kipindi cha nyuma. Mwanzoni kabisa gazeti hilihili la Championi, liliibua na kuonyesha jinsi msanii Diamond alivyorudia mawazo ya wasanii wengine hasa wale wa Ulaya kwenye video ya nyimbo zake. Alianza na Make Me Sing kisha Kidogo na sasa kamalizia na Fire ambayo video yake inafanana na ile ya Jason Derulo iitwayo Swalla. Baada ya msanii huyo kuyafanya hayo, hivi karibuni mwanadada anayekimbiza kwenye game ya muziki huo, Vanessa Mdee ‘Vee Money’ naye kaamua kupita mulemule yaani kakopi kisha kupesti katika mkwaju wake mpya wa Kisela ambao amempa shavu pacha wa Kundi la P-Square, Paul Okoye. Kisela ya Vee Money inafanana na ile ya Energy iliyofanywa na Keri Hilson wa Marekani, lakini tofauti ni miaka, wakati Kisela haina hata wiki mbili tangu iachiwe yaani Julai 10, mwaka huu, Energy ya Keri sasa inagota mwaka wa nane tangu iachiwe kwake Desemba 13, 2009. Championi Jumatatu linakuletea baadhi ya maeneo ambayo Vee Money aliyesikika kisanii kupitia Ngoma ya Closer, ameiga kutoka kwenye video ya Energy.
Keri Hilson - Energy
MAZINGIRA YA VIDEO NZIMA
Hapa ndipo tatizo la kukopi na kupesti alilofanya Vee Money linapoanza, haihitaji elimu ya chuo kikuu kutambua kwamba mazingira ya video zote mbili yanafanana yaani ile ya Kisela na Energy.
Vee Money ametembelea mawazo ya Keri Hilson ya kutengeneza video katika mazingira ya ‘gym’ (sehemu ya kufanyia mazoezi kwa wanamasumbwi) ambapo mwanzo mwisho video hiyo imeshutiwa eneo hilo kama ilivyo ya Energy.
UWANJA WA NGUMI Hili pia ni eneo lingine ambalo Vee Money ‘dizaini f’lan amelipestisha’ kwenye video yake ambapo mwanzoni tu mwa video yake anaonekana yuko kwenye ulingo wa ngumi jambo ambalo hata Keri amelifanya katika video yake na hata kukaa kwenye viti vinavyowekwa kwenye kona ya mabondia. Ukifuatilia kwenye video zote mbili ya Keri na Vee Money, utabaini kuwa wasanii wote wametumia eneo la ulingo kwa asilimia kubwa katika kushutia video zao. Msanii wa Kimataifa, Keri Hilson.
KUPIGA PUNCHING BAG Vee Money ameendelea kuonyesha kuwa hakutumia nguvu kubwa kuwaza kuitengeneza video yake hiyo hata kama atakuwa ametumia fedha nyingi kuitengeneza. Eneo lingine ambalo linamuonyesha Vee Money amekopi na kupesti ni kwenye kipengele hiki ambapo kule kwa Keri anaonekana kupiga ‘punching bag’ kwa ajili ya kujiandaa na pambano lake jambo hilohilo linafanywa na Vee Money kwenye video yake ya Kisela. Hapo utaona kabisa kuwa amekopi tu tukio la mwenzake kisha kulihamishia kwake.
Staa wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee 'Vee Money'.
KUPIGA SPEED BAG Kukopi kamwe hakutamuacha salama Vee Money kwani vipengele alivyovitumia kwenye wimbo wake ndivyo vinamhukumu mwenyewe, ukiitazama vizuri Video ya Energy kuna sehemu inamuonyesha Keri akipiga ‘speed bag’ na ukirudi kwa Vee Money naye mwanzoni alikuwa akifanya hivyo kabla ya baadaye kuja kufundishwa na Paul Okoye jinsi ya kukitumia kifaa hicho.
Post a Comment