ad

ad

Waraka huu mzito uwafikie Bongo Muvi wote!

HUU ni waraka mzito kwa Bongo Muvi wote kutoka kwa mdau kama kweli wanataka kuinusuru tasnia hiyo na kifo ni vyema kuzingatia haya; MAPENZI: Mapenzi ni moja kati ya sababu kubwa za mtu hasa wanawake kuingia kwenye tasnia. Kama mdada ana makalio makubwa, nido za kueleweka na mambo mengine yenye kuamsha tamaa za mwili, basi huyo amefuzu kuwa mwigizaji hata kama hana kipaji chochote.

Unapotumia mapenzi kama chujio kwenye usahili, unakusanya makapi na wenye vipaji wanachujwa, kisa muonekano tu.

UBINAFSI: Unakuta muvi moja, mtu mmoja ndiye staa, mwongozaji mhariri, mzalishaji, mwandishi wa mswada na mengineyo. Yaani akili ya mtu mmoja inaongoza nafasi zaidi ya tano. Siku ikitokea mtu huyo akapatwa na tatizo, karibu kampuni yote inatikisika au kufa (kisa cha Steven Kanumba kinaakisi hili). Kwa nini wasitafutwe watu tofauti kwenye nafasi mbalimbali ili kuingiza akili nyingi na mawazo ya watu wengi kwenye utengenezaji?

ELIMU: Kubali au kataa lakini asilimia kubwa ya waigizaji wa Bongo Muvi ni wale wenye uwezo mdogo kielimu, ambao walijishawishi kuwa hawakupewa akili za darasani ila vipaji vya sanaa, wasijue akili ndiyo mzizi wa kila kitu. Matokeo yake ni kukosa kazi bora, ubunifu na mengine muhimu katika sanaa. Mbadala wake wameishia kukopiana kazi zao, ku-reflect matukio ya kwenye jamii kama vile mauaji ya maalbino na vikongwe, ndoa na usaliti na mapenzi kwa jumla. Vitu ambavyo haviisisimui hadhira maana walishavizoea.

MADAWA YA KULEVYA: Madawa ya kulevya ni sababu nyingine ya wao kuvurunda na ndiyo matokeo ya kufa kwa Bongo Muvi. Ni sababu kwa maana wakishatumia madawa uwezo wa kazi unapungua. Wanakuwa wamesizi kwa muda mrefu zaidi ambao walitakiwa wafanye kazi, pia wanatumia fedha nyingi kununulia unga. Ni matokeo kwa maana wakishafulia kwenye uigizaji wanabakiwa na jina bila fedha. Ili kuendelea kushikilia majina yao wanakubali kuwa punda wa kubebea unga ili wapate namna ya kuishi mjini.

KUTUMIKA KISIASA: Kama nilivyosema, hawa watu uwezo wao kielimu ni mdogo. Wanajiingiza kwenye chama cha siasa bila kujali mashabiki wao ni vyama tofauti na wengine hawana vyama. Hawajui kwamba kama tasnia kujiingiza kwenye chama wanaonekana kama vile ni kitengo cha chama fulani. Ikiwa mashabiki wana chuki na chama walichojiunga, basi ile chuki inasambaa hadi kwao na mwishowe hakutakuwepo wa kununua kazi zao. Waraka wa mdau kutoka mtandaoni.

No comments

Powered by Blogger.