SI KITU BILA PENZI LAKO-10

NYEMO CHILONGANI
Maria hakujisikia vizuri moyoni, mvulana ambaye alikuwa amemuona katika kipindi kichache kilichopita alionekana kumchanganya. Ni kweli alikuwa amewaona wavulana wengi na kutongozwa na wavulana wengi lakini mvulana ambaye alikuwa amemuona katika kipindi kichache kilichopita alionekana kumchanganya.
Akajilaza kitandani na kuanza kumfikiria. Akili yake haikutulia kabisa, moyo wake ulionekana kuhisi kitu fulani ambacho kilikuwa kigeni sana maishani mwake. Akaanza kujisikia kupenda na kuitaji. Mapenzi makubwa aliyokuwa nayo moyoni, alitaka kumpatia Hidifonce ambaye alikuwa amemuona nje.
Hakuwa akimfahamu kwa jina na hiyo ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kumuona machoni mwake. Bado aliendelea kukihisi kile kitu kizito moyoni mwake. Hakutaka tena kuendelea kubaki ndani, akatoka nje ili kwenda kumwangalia Hidifonce kwa mara nyingine.
Hidifonce hakuwa pamoja na vijana wale, alikuwa ameondoka na kuelekea chumbani mwake. Maria akaonekan kuwa mpweke, moyo wake ukaanza kummisi mvulana ambaye ilikuwa mara yake ya kwanza kumuona machoni mwake.
Akaanza kurudi nyumbani kwao ambako akaingia getini na kuelekea chumbani kwake. Maria hakulala, muda wote alikuwa akimfikiria Hidifonce. Kitandani hakukulaloka, alibaki akijigeuza huku na kule. Maria akasahau kabisa kama alikuwa mtoto wa mchungaji wala hakufahamu kama alikuwa katika kikundi cha Uimbaji kanisani, kwa kipindi hicho kitu alichokijali ni kuwa pamoja na Hidifonce tu.
Wiki moja ilipita, Hidifonce hakuonekana machoni mwake, siku zote hizo Maria alikuwa akionekana kuwa na mawazo juu ya Hidifonce. Muda mwingi Maria alikuwa akimfikira Hidifonce kiasi ambacho alishindwa kabisa kujisomea nyumbani.
Maria akaonekana kutokukubali kabisa kuuacha moyo wake uwe na mawazo juu ya Hidifonce. Kitu alichokifanya ni kwenda katika sehemu ile ambay alimuona Hidifonce akiwa amekaa paoja na vijana wengine. Maria akaamuulizia Hidifonce mahali pale.
Kila kijana ambaye alikuwa mahali pale alibaki akishangaa, hawakujua Maria na Hidifonce walikuwa wamefahamiana vipi kwani Maria aliuliza kana kwamba alikuwa akimfahamu Hidifonce. Akaelekezwa nyumba ambayo Hidifonce alikuwa akiishi na moja kwa moja kuanza kwenda huko.
“Ni vigumu kumpata mchana. Muda mwingi huwa anashinda ofisini” Msichana mmoja aliyekuwa akikaa katika nyumba ile, Shania alimwambia Maria.
Maria akaonekana kuchoka, maneno ambayo aliambiwa yalionekana kumuumiza, alihitaji sana kuonana na Hidifonce kwa wakati huo, maneno ambayo aliambiwa kuwa usiku ndio ulikuwa muda wa kuonana nae ulionekana kumuumiza.
Hakuwa na uhakika kama angeruhusiwa kwenda sehemu yoyote usiku. Alijiona kuwa na bahati mbaya, akamwangalia Shania huku akioekana kuhuzunika, alionekana kukosa raha kabisa.
“Akirudi mwambie namtafuta” Maria alimwambia Shania na kuondoka.
Shania akabaki akiwa na mshangao, hakuamini msichana mrembo kama Maria angefika nyumbani hapo na kumuulizia Hidifonce. Alimuona Maria kama msichana ambaye alitakiwa kukaa nyumbai na kumsubiri mvulana na si yeye kwenda kumuulizia mvulana.
********
Mitumbwi zaidi ya mia moja ilikuwa ikiingia katika ziwa Viktoria kila siku usiku. Wavuvi walikuwa wakivua samaki usiku mpaka alfajiri muda ambao walikuwa wakirudi katika makazi yao na kuwauza.
Biashara ile ilionekana kubadilisha maisha ya wakazi wengi kwa wananchi ambao walikuwa wakizunguka ziwa la Viktroria, yaani kuanzia Uganda, Kenya mpaka Tanzania. Samaki halikuonekana kuwa tatizo kwa upande wa sehemu hizo tatu, kila siku samaki wengi walikuwa wakivuliwa, hasa katika usiku ambao hakukuwa na mwezi.
Kati ya wavuvi ambao walikuwa wakifanya kazi ya uvuvi alikuwepo mzee Mshana ambaye mara kwa mara alikuwa akiingia ziwani pamoja na vijana wake kufanya kazi hiyo ya uvuvi. Kila siku walikuwa wakiingia ziwani usiku pamoja na chemri zao.
Kazi kubwa ya chemri zao ilikuwa ni mwanga. Ziwani hakukuwa na mwanga hali ambayo mara samaki walipokuwa wakiuona mwanga wa Chemri, walikuwa wakija juu hali iliyofanya kuvuliwa kwa urahisi zaidi. Kutokana na hali hii, kazi ya uvuvi ilionekana kuwa ngumu katika kipindi ambacho kulikuwa na mbaramwezi, katika kipindi hicho, samaki hawakuwa wakija juu kwani mwanga wa mbaramwezi ulikuwa ukiwatosha.
Mzee Mshana pamoja na vijana wake walikuwa wakiendelea na kazi zao za uvuvi kama kawaida. Walikuwa katikati ya ziwa huku wakijaribu kushusha nyavu zao kujaribu kama wangeweza kupata samaki wowote. Kipindi hicho kilionekana kuwa kipindi kigumu kutokana na mwezi kuangaza angani.
Walijaribu kushusha nyavu zao katika kila kona lakini hawakupata samaki wengi, kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa. Mara kwa mara walikuwa wakiuangalia mwezi kwa nyuso zilizojaa hasira. Hawakuupenda mwezi katika maisha yao kwani upatikanaji wake ulikuwa ukiyafanya maisha yao kuwa magumu.
“Kuna boti ile inaondoka...ilikuwa imesimama mahali pale. Kwa nini tusiende pale na sisi tukajaribu?” Fikiri aliwaambia wavuvi wenzake akiwepo mzee Mshana .
“Hakuna kitu pale. Hivi kama kungekuwa na kitu wale wangeondoka na mtumbwi wao?” Mzee Mshana alimwambia Fikiri.
Mvutano ukaanzia mahali hapo. Fikiri alikuwa wakitaka kuelekea katika eneo lile kwa ajili ya kuhakikisha kama kweli hakukuwa na samaki. Tayari Fikiri akaonekana kuwa na wasiwasi na mtumbwi ule ambao ulikuwa umeondoka kwa kasi mahali pale.
Kila alipotaka kulipotezea jambo hilo, moyoni alisikia sauti ambayo ilimwambia kuwa ni lazima waende mahali pale. Fikiri alijaibu kubishana na sauti ile lakini sauti ile ikaonekana kuwa kero moyoni mwake. Hakujua kama sauti ile ilikuwa ni mawazo yake mwenyewe, sauti ya Malaika au sauti ya Roho chafu iliyokuwa ikimtaka awashawishi wenzake waende pale ili wazame na kupotea.
Akaupiga moyo wake konde na moja kwa moja kuwang’ang’aniza wavuvi wenzake waende mahali pale. Fikiri alionekana kuwa mbishi hali ambayo iliwafanya kukubaliana nae kwa shingo upande. Wakaanza kupiga kasia mpaka katika eneo lile ambapo wakachukua nyavu na kushusha majini.
Wala hawakuchukua muda mrefu, mara wakasikia kitu kizito kikiwa kinaivuta vuta nyavu yao. Wakajitahidi kuvuta nyavu zao lakini wala hawakufanikiwa kitu ambacho kiliwapelekea kumwambia Fikiri kuingia chini ya Ziwa kwa ajili ya kumtoa samaki huyo mkubwa ambaye alikuwa amenasa katika nyavu zao.
Fikiri hakuwa na la kujifikiria mara mbili mbili, moja kwa moja akajitosa majini huku akiwa na kisu chake mkononi pamoja na tochi ambayo ilikuwa na uwezo wa kutokupitisha maji. Alikuwa akielekea chini kabisa ambako kulikuwa na kina kirefu zaidi ya maghorofa kumi na mbili.
Baada ya kufika chini ya maji, akaanza kumulika mulika katika kila kona majini mule hasa katika nyavu yao ambayo walikuwa wameishusha. Aliendelea kuangalia zaidi na zaidi, ni samaki wachache ndio ambao walikuwa wamenasa katika nyavu zao.
Fikiri akajaribu kuivuta tena nyavu ile, ilionekana kuwa nzito kuja juu hali iliyomfanya kugundua kuwa kulikuwa na kitu majini, hasa kule chini kabisa. Kwa sababu bado alikuwa amebakisha pumzi za kutosha, akaendelea kwenda chini huku akimulika mulika.
Fikiri hakuamini macho yake, alibaki akitetemeka huku akiuhisi mwili wake ukifa ganzi majini. Kitu alichokiona hakuwa akiamini kama ndicho kilikuwa kile alichokuwa akikiona au kilikuwa tofauti na kile. Alitamani apige mbizi kwenda juu, lakini akaupiga moyo wake kondo na kuelekea kule alipomuona binadamu huku akikiweka vizuri kisu chake.
Ulikuwa ni mwili wa binadamu ambao uilikuwa umelegea kupita kiasi. Akaushika mkono na kuanza kurudi kwa juu. Wavuvi mbao walikuwa mtumbwini walikuwa wakimsubiria Fikiri kwa furaha zote kwani waliamini kuwa ni lazima angerudi mtumbwini hapo akiwa na samaki mkubwa ambaye allikuwa amenasa katika nyavu yao.
Fikiri akaibuka na kuomba msaada wa kumvuta kutoka majini. Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akiamini kile ambacho alikuwa akikiona mahali pale. Fikiri alikuwa amekuja na kitu kingine ambacho kilikuwa na tofauti na matarajio yao.
“Binadamu....!” Mzee Mshana alisema huku akionekana kuogopa.
“Hebu muwekeni hapo kwanza” Fikiri aliwaambia wavuvi wenzake na kumvuta Patrick na kumuweka katika mtumbwi wao.
Kila mmoja alikuwa akimwangalia Patrick kwa mshangao, kila walipojaribu kumuuliza Fikiri kwa kile ambacho kilikuwa kimetokea ziwani mule, hakuongea kitu, alikuwa amekaa pembeni akihema kwa nguvu kutokana na kutokuvuta pumzi muda mrefu majini.
“Hivi anapumua?” Mzee Mshana aliuliza hali iliyompelekea mvuvi mmoja kusikiliza mapigo ya moyo.
“Mhhh!! Kwa mbali sana....yaani sana” Kijana yule mvuvi alimjibu.
Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa na hamu ya kuendelea na uvuvi, walichokifanya ni kuanza safri ya kuelekea katika kisiwa cha Ukerewe ambacho walikuwa wakiishi. Muda wote walikuwa wakijitahidi kumtoa maji Patrick tumboni, hakuwa akijitambua kabisa pale alipokuwa na wala hakujua ni kitu gani kilikuwa kinaendelea.
Walichukua masaa mawili mpaka katika kisiwa cha Ukerewe ambako wakauweka mtumbwi wao na kisha kuanza kuelekea katika nyumba yao huku saa ikiwaonyesha kuwa saa kumi na robo alfajiri.
Patrick akawekwa katika chumba ambacho hakikuwa na kitu chochote kile kwa ajili ya kupata hewa safi. Masaa yaliendelea kukatika, ilipofika saa nne asubuhi, Patrick akafumbua macho. Akaanza kuangalia huku na kule, uso wake ulijawa na mshangao kupita kiasi.
Akainuka kutoka pale kitandani na kuanza kuelekea nje, maeneo ya eneo lile yalionekana kumchanganya kupita kiasi. Akaanza kuvuta kumbukumbu zake, alikumbuka mara ya mwisho alikuwa katika mtumbwi pamoja na wavuvi wengine na kisha kutoswa majini. Alikumbuka kila kitu, alipoanza kutapatapa mpaka kuona giza mbele yake.
Akaangalia vizuri sehemu ile, wavuvi wanne wakaonekana wakiwa katika mtumbwi uliokuwa karibu na ufukwe wakichambua samaki. Patrick akaanza kupiga hatua kuwafuata mtumbwini mule. Kila mtu akaanza kumwangalia Patrick huku nyuso zao zikionekana kujawa na tabasamu.
“Unaendelea vipi?” Fikiri alimuuliza Patrick.
‘Naendelea vizuri. Hivi ni nini kilitokea?” Patrick aliuliza hali iliyowafanya wavuvi wale kuanza kumuelezea kila kitu ambacho kilitokea.
Katika kisiwa hicho cha Ukerewe ndipo ambapo Patrick alipoanza maisha mapya. Kila siku alikuwa akibaki nyumbani pamoja na Fikiri huku wavuvi wakiendelea na kazi zao za uvuvi. Patrick alionekana mpweke, baridi lililokuwa kisiwani kule lilionekana kumsumbua kupita kiasi.
Muda mwingi alikuwa akimfikiria Azizi, hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea kwa Azizi, kila siku maisha yake yalikuwa na huzuni, akili yake ilijua fika kwamba Azizi alikuwa ametoswa majini kama vile ambavyo ilitokea kwake.
Hakujua kama Azizi alikuwa amenusurika kama ambavyo alinusurika yeye. Kila siku mawazo juu ya Azizi yalikuwa yakimsumbua, wakati mwingine alikuwa akitoa machozi, alijiona kumpoteza tu muhimu maishani mwake ambaye aliamini kuwa angekuwa pamoja nae hadi pale ambapo maisha yake yangekuwa salama.
Kila siku Patrick alikuwa na wazo moja tu, la kuondoka kisiwani hapo na kuelekea Mwanza mjini ambako huko angejua ni wapi ambapo angetakiwa kwenda. Hakutaka kabisa kuishi kisiwani hapo, kila siku alikuwa akipanga namna yya kutoroka kisiwani hapo.
Mwezi ulikatika, bado Patrick alikuwa kisiwani hapo huku akiwa amezoeana na watu wengi ambao walikuwa wakiishi kisiwani hapo. Patrick alikuwa akisaidiana nao kazi japokuwa akili yake ilikuwa ikitafuta namna ya kutoroka mahali hapo.
Siku ziliendelea kukatika, kila njia ambayo alikuwa akiifikiria aliiona kutokufaa kabisa. Kitu alichokifanya kwa wakati huo ni kujenga urafiki mkubwa na Fikiri ambaye wakatokea kuzoeana kama ambavyo alizoeana na Azizi ambaye hadi wakati huo hakujua alikuwa mahali gani.
“Nataka kujifunza kuvua samaki” Patrick alimwambia Fikiri asubuhi moja ambapo hakukuwa na watu wengi kisiwani hapo.
“Mbona asubuhi namna hiyo, wewe unafikiri utapata samaki kweli?” Fikiri aliuliza.
“Nitapata tu. Kama ambavyo Petro alivyopata wakati walipokwenda kuvua” Patrick alimwambia Fikiri.
Fikiri hakuwa na jinsi, kwa kuwa alikuwa amemzoea sana Patrick, akaona kuwa kusingekuwa na tatizo kama ambavyo alivyofikiria. Akamkabidhi Patick mtumbwi mmoja na kisha kuingia nao majini. Akili ya Patrick ilikuwa ikifikiria kuondoka kisiwani hapo ambapo aliyaona maisha kuwa magumu kwake.
Akaanza kupiga kasi kwa kasi, hakuttaka kuchelewa sana kufika Mwanza mjini. Aliendelea kupiga kasia zaidi na zaidi, alikuwa akipishana na mitumbwi kadhalika ziwani mule. Mikono yake ilikuwa imechoka kupita kiasi lakini hakutaka kusimama njiani, bado alitaka kufika Mwanza mapema.
Alichukua masaa matatu mpaka kufika Mwanza mjini. Mitumbwi ilikuwa mingi ziwani na wala hakukuwa na mtu aliyehofia kwa mtu mwenye umri kama wake kutumia mtumbwi ziwani. Mara baada ya kufika karibu na nchi kavu, akauegesha mtumwi pembeni na kisha kuteremka.
Akaanza kupiga hatua kuelekea mjini huku akiangalia huku na kule. Njaa kali ilikuwa imemkamata kiasi ambacho wakati mwingine alikuwa akijihisi kusikia kizunguzungu. Patric alitembea kwa haraka sana, maghorofa yalikuwa yakionekana machoni mwake, akaanza kuangalia huku na kule, macho yake yakamuona dereva Taksi ambaye alikuwa amesimama nje ya gari lake.
“Naomba unisaidie” Patrick alimwambia dereva yule.
“Nikusaidie nini?”
“Mia tano. Nasikia njaa kaka yangu” Patric alimwambia dereva yule kwa sauti ya chini ambayo ilionyesha ni kwa kiasi gani alikuwa na njaa kwa wakati ule.
“Umeniona mimi ni benki? Au kituo cha kutoa msaada kwa watoto wa mitaani?” Dereva yule aliuliza huku akinekana kukasirika kutokana na kuwa mahali hapo kwa masaa manne pasipo kupata abiria yeyote.
“Naomba unisaidie kaka yangu” Patrick alimwambia dereva yule.
“Sikiliza. Unaliona gari lile, wafuate na uwaombe msaada, watakusaidia. Wao wanawajali watoto lakini si mimi” Dereva yule alimwambia Patrick.
Patrick akaliangalia gari lile ambalo alikuwa ameambiwa. Maneno makubwa yaliyosomeka Thomas Lyaruu Tourism Company yalikuwa yakionekana katika gari moja aina ya Harrier. Patrick akaanza kupiga htua za haraka haraka kuelekea katika gari lile.
Alipofika nyuma ya gari lile, akaanza kuangalia nyuma ya gari lile. Kreti tano za soda pamoja na mikate ilikuwa ikionekana vizuri machoni mwake. Akajaribu kuufungua mlango ule wa nyuma kabisa, mlango ukafungua na kisha kuingia. Kutokana na njaa kali aliyokuwa nayo, akaanza kunywa soda zile na kula mikate ile kwa kasi kubwa.
Alikula na kunywa, ghafla akasikia mlango wa mbele ya gari ukifunguliwa. Kwa kasi akajifunika shuka kubwa lililokuwa nyuma ya gari lile sehemu ya kubebea mzigo na kujifunika. Patrick akasikia gari lile likiwashwa na kisha kuondoka mahali pale huku akiwa garini.
“Ni lazima tuwahi. Tunajua kuwa kule tutakutana na wazungu wengi ambao tutawachukua na kuwapeleka wanapopataka” Sauti ya kijana mmoja ilisikika.
“Ila si kuna magari mengine ya kampuni hii yataelekea kule?”
“Ndio”
Gari lile la watalii lilikuwa likiendelea na safari ya kuelekea Musoma katika kijiji cha Butiama kwa ajili ya kukumbukwa kwa Hayati Mwalimu Nyerere. Wazungu wengi walikuwa wakitarajiwa kukusanyika mahali kule kwa ajili ya kuangalia kaburi la kiongozi huyo ambaye alikuwa ameipa Tanganyika uhuru.
Siku hiyo ilionekana kuwa maalumu kwa Watanzania, wafanyaazi hawakwenda kazini na wala wanafunzi hawakwenda shuleni. Idadi ya watu zaidi ya elfu tano iltarajiwa kukusanyika katika kijiji hicho, kila mtu alitamani kuliona kaburi hilo ambalo lilikuwa likitangazwa sana katika vyombo vya habari hasa mara baada ya kufanyiwa matengenezo na kuwa tofauti na jinsi lilivyokuwa kabla.
Patrick hakujua alikuwa akipelekwa wapi ila kitu ambacho alikuwa akikitaka ni kuondoka na kuelekea sehemu yoyote ile ili tu akaanze maisha mapya. Vumbi lilikuwa likiingia katika shuka lile lakini Patrick hakuonekana kujali, bado alikuwa akitaka kufika mwisho wa safari ile ambayo hakujua ingekuwa mahali gani.
Patrick alionekana kuchoka na maisha, alijitolea aishi sehemu yoyote ambayo aliiona kuwa na utulivu na salama katika maisha yake. Kila siku alikuwa akijifikiria ni kwa jinsi gani angefanikiwa katika maisha yake na kurudi kijijini Itilima kwa ajili ya kumuoa Victoria ambaye bado alikuwa akimpenda kuliko msichana yeyote.
Gari lile lilitembea kwa masaa matatu, Patrick alilihisi likisimama, akafungua shuka na kuanza kuchungulia kwa nje. Milango ya gari lile ikafunguliwa na wale watu ambao walikuwa katika gari lile kuteremka. Sauti za watu zilikuwa zikisikika mahali pale.
“Kachukue vinywaji kule nyuma ya gari” Sauti ya kijana mmoja ilisikika.
Patrick akaonekana kushtuka, hakujua ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya kwa wakati ule. Alisikia vishindo vya mtu akija kule ambako alikuwepo. Patrick akaanza kutetemeka kwa hofu, wasiwasi ulikuwa umemjaa kupita kiasi, tayari alijiona kukamatwa na mtu yule ambaye alikuwa akija kule kuchukua vinywaji.
*****
Hidifonce alijikuta akichanganyikiwa kupita kiasi. Kitendo cha Maria kuja nyumbani na kumuulizia kilionekana kumchanganya sana. Akaanza kumfikiria msichana huyo, uzuri wake na hadi kila kitu ambacho alikuwa nacho.
Hakujiona kujiamini kabisa, Maria kwake alionekana kuwa msichana mzuri ambaye wala hakutakiwa kuwa na mwanamume kama yeye. Mwanaume ambaye alihitajika kuwa na Maria ni yule ambaye alikuwa na usafiri utakaomfanya Maria kutokutembea kwa miguu kwa ajili ya kuuchosha mwili wake.
Alimwangalia Shania mara mbili mbili, hakuonekana kutokuamini kile ambacho alikuwa amemwambia. Kitendo cha Maria kuja nyumbani pale kilionekana kumfanya kutokuamini kabisa. Akaingia chumbani kwake na kujipumzisha kitandani mwake.
Akili yake ikaanza kumfikiria Maria toka siku ile ambayo alikuwa amemuona na kuangaliana kupita kiasi. Hidifonce akaanza kujiona mtu mwenye bahati sana, kitendo cha kuuliziwa na Maria, msichana ambaye alikuwa na uzuri wa kipekee, kilionekana kuwa kitendo kilichokuwa na bahati kubwa.
Hidifonce hakutaka kabisa kuonana na Maria kitendo ambacho kilimfanya kuchelewa kurudi nyumbani. Kila sik alipokuwa akirudi nyumbani alikutana na malalamiko kadhaa kutoka kwa Maria ambayo alikuwa ameyaacha kwa Shania.
Maria alionekana kumuhitaji Hidifonce ambaye wala hakuonekana kujali kutokana na woga ambao alikuwa nao. Malalamiko yaliendelea kuzidi kila siku lakini wala hakukuwa na mabadiliko ambayo yalikuwa yametokea, bado Hidifonce hakutaka kuonana na Maria.
“Ameleta bahasha” Shania alimwambia Hidifonce huku akimkabidhi bahasha ile.
Hidifonce akaichukua bahasha ile kubwa ya kaki na kuingia ndani. Akaanza kuifngua, macho yake yakakutana na maua kadhaa pamoja na kadi. Tabasamu kubwa likautawala uso wake. Akaendelea kuangalia zaidi, macho yake yakakutana na albamu ndogo ambayo akaichukua na kuanza kuangalia picha zilizokuwa katika albamu ile.
Hidifonce akaonekana kushtuka, mapigo ya moyo yakaanza kumdunda kwa kasi, hakuamini kile ambacho alikua akikiona katika albamu ile. Picha kadhaa za Maria ambazo alikuwa amezipiga nusu uchi zilikuwa zikionekana vizuri machoni mwake.
Hidifonce akajiona kuhisi hali ya tofauti mwiini mwake. Hamu ya kufanya mapenzi ikaanza kumkumba. Kila alipozidi kuziangala picha zile na ndivyo ambavyo alizidi kuchanganyikiwa na hali ile kumshika zaidi. Alipomaliza kuzingalia picha zile, akajilaza kitandani huku albamu ikiwa pembeni yake.
Tayari akaona ni kwa jinsi gani Maria aikuwa akimpenda, moyo wake akauhisi kuanza kuingia katika uhitaji wa kuwa pamoja na Maria. Mpaka kufikia hatua ile, hakuona sababu ya kumpotezea Maria, alijua ni kwa jinsi gani moyo wa msichana yule ulikuwa ukimuuma kila alipokuwa akija nyumbani na kumkosa.
“Ni lazima niongee nae kesho” Hidifonce alisema.
Siku iliyofuata ilikuwa jumamosi ambayo wala Hidifonce hakuwa akielekea kazini. Alibaki nyumbani huku akiiona siku hiyo kuwa maalumu ya yeye kuwa pamoja na Maria na kuongea. Alianza kufanya kazi zake kama kawaida na alipomaliza, akaandaa chakula na kuanza kula.
Alitaka kupata maandalizi makubwa zaidi kwa ajili ya kuongea na msichana yule ambaye kila siku sifa za uzuri wake zilikuwa zikizidi kusikika kutoka kwa watu mbalimbali mtaani pale. Hidifonce alifanya kila kitu, alipomaliza, akamfuata Shania.
“Unaweza kwenda kumuita?”
“Nani?”
“Maria”
Shania akachomoka mahali pale na kuelekea nyumbani kwa mchungaji Christopher kwa ajili ya kumuita Shania. Shania hakuonekana kuamini kama kweli Hidfonce ndiye ambaye alikuwa akimuita kwa wakati huo. Kwa kuwa alikuwa amekwishaoga, akaanza kujiandaa kwa kujipulizia pafyumu kadhaa na kisha kuanza kwenda kumuona Hidifonce. Kadri alivyozidi kupiga hatua kuelekea katika nyumba aliyokuwa akiishi Hidifonce na ndivyo ambavyo mapigo yake ya moyo yalivyozidi kumdunda.
“Naomba unisindikize Shania” Maria alimwambia Shania huku akionekana kuogopa kuingia peke yake.
“Inga tu. Kama unaogopa basi rudi” Shania alimwambia Maria ambaye akaingia ndani.
Hidifonce alikuwa ametulia kitini huku akionekana kuukunja uso wake kama mtu ambaye alikuwa amekasirika. Maria akaonekana kuogopa, akamwangalia Hidifonce mara mbili mbili huku kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo hofu ilivyompata zaidi.
Kwa sababu hakukuwa na viti chumbani pale, Maria akakaa kitandani, macho yake yalikuwa yakiangalia chini huku kwa mbali akionekana kutetemeka. Hidifonce alibaki akimwangalia Maria, tayari alikwishauona woga ambao alikuwa nao Maria, akaanza kumsogelea kwa karibu.
“Mbona umefanya ujinga huu Maria?” Hidifonce aliuliza huku akimwangalia Maria. Maria hakujibu kitu.
“Yaani unanitumia picha ulizopiga nusu uchi. Unafikiri nikiziangalia ndio nitakuona wewe mzuri? Sikiliza Maria, kama mbaya ni mbaya tu, hata ungeniletea picha za utupu kabisa, ungeendelea kubaki hivyo hivyo, yaani wala usingenisisimua” Hidifonce alimwambia Maria.
Ghafla Maria akaanza kubadilika. Kwikwi ikaanza na hatimae machozi kuanza kumtoka. Maneno aliyoyaongea Hidifonce yalionekana kumuumiza kupita kiasi. Akasimama na kuanza kuufuata mlango. Hakutaka kumwangalia Hidifonce usoni, tayari machozi yake yalikuwa yameloanisha mashavu yake. Akatoka ndani ya chumba kile na kuufunga mlango kwa kuubamiza hali iliyoonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa na hasira.
Je, nini kitaendelea?
Post a Comment