Maradona na PES17 hapakaliki, kuwaburuza tena mahakamani
Mcheza ndinga wa zamani mkongwe katika soka Diego Maradona yuko mbioni kuipeleka mahakamani kampuni ya Konami ambao ni watengenezaji wa video game maarufu ya PES.
Maradona ameishutumu Konami kwa kutumia muonekano wake bila ruhusa yake, sura hiyo ya Mradona imeonekana katika game yao mpya ya mwaka 2017.
Maradona aliyeonekana mwenye jazba na hasira sana alitumia ukurasa wake wa Facebook kuwajia juu Konami kwa game yao hiyo, na amewahakikishia lazima wapande juu ya kizimba kutokana na suala hilo.
Maradona aliipiga picha yake anavyoonekana katika game hiyo wakati alipokuwa kijana huku akionekana na nywele ndefu nyeusi, nywele zilizokuwa zikionekana kama wigi.
Konami ambao ni Wajapani wanaweza kukumbana na rungu kali la sheria kwani inasemekana waliitumia picha ya Maradona na kuipa jina lingine la Malgini.
Katika kesi ya kwanza ya Maradona baada ya jina lake kubadilishwa, Maradona alishinda kesi hiyo ya mwanzo. Lakini safari hii Konami wanaweza kuwa katika matatizo zaidi kwa kutumia image ya Maradona bila ruhusa yake.
Kesi hii ya Maradona inaweza kuwafaidisha wapinzani wakubwa wa PES17 ambao ni FIFA17, ambao wao wameruhusiwa na Maradona kutumia sura yake baada ya makubaliano yao kuafikiwa.
Lakini kesi ya Maradona na Konami inaweza kuwa na jambo la utetezi kwa Konami kwani inasemekana mwaka 2016 walisaini mkataba na Barcelona ambao uliwapa haki ya kuwatumia wachezaji wote waliopitia Barcelona vivyo hivyo na Napoli.
Post a Comment