SIMULIZI: SI KITU BILA PENZI LAKO -02
Bado Patrick alimkazia macho msichana yule aliyesimama mbele yake akimuomba kucheza naye. Alikuwa akimshangaa, hakuelewa kwa nini msichana yule hakuwa akimuogopa kutokana na sifa kubwa ya uchawi aliyokuwa nayo.
Patrick akasimama, bado mapigo yake ya moyo yalikuwa yakiendelea kumdunda kupita kawaida, hakuelewa msichana yule alikuwa na lengo gani kwake. Wanafunzi wengine waliokuwa wamesoma naye shule moja, wakamshangaa msichana yule ambaye wala hakuonekana kuogopa kitu chochote kile.
“Naitwa Victoria. Victoria Carlos,” msichana huyo alijitambulisha kwa Patrick huku akijaribu kuupeleka mkono wake katika mkono wa Patrick.
“Naomba tukacheze muziki,” Victoria aliendelea kumwambia Patrick.
Patrick hakutaka kubaki mahali hapo, akaanza kupiga hatua kurudi nyuma kama njia moja ya kumkwepa Victoria na baada ya kufika umbali fulani, akaanza kukimbia kuelekea porini.
Victoria hakutaka kubaki mahali hapo, naye akaanza kukimbia kuelekea kule ambapo Patrick alikuwa amekimbilia. Kutokana na kasi kubwa aliyokuwa akiitumia Patrick, Victoria hakuweza kumuona.
Tayari giza lilikuwa limeingia. alizidi kukimbia. Moyo wake ulikuwa na wasiwasi mkubwa kwamba wazazi wake walikuwa wakimsubiri kwani haikuwa kawaida yake kuchelewa kufika nyumbani. Hakutaka kuyasubiri magari yaliyokuwa yakiwachukua wanafunzi kuwapeleka katika vijiji mbalimbali kwani aliamini kuwa asingechukuliwa kama alivyofanyiwa kipindi cha kwenda mahali pale.
Giza lilikuwa limekwishaingia na bado alikuwa akikimbia kwa mwendo wa kasi kuelekea kijijini kwao, Chibe. Ingawa kulikuwa na giza lakini hakuogopa kitu chochote kile, alichokitaka kwa wakati huo ni kuingia kijijini na kuelekea nyumbani kwao.
Kwa mbali Patick akaanza kuuona mwanga wa moto uliokuwa ukiwaka, akasogea zaidi na zaidi kuelekea kule kulipokuwa na eneo la nyumba yao. Akashtuka baada ya kugundua kuwa nyumba iliyokuwa ikiteketea ilikuwa nyumba yao.
Akajificha katika kichaka kimoja na kuanza kuangalia kule kulipokuwa na nyumba yao. Vijana zaidi ya ishirini walikuwa nje huku wakishangilia kwa shangwe. Mara akamuona baba yake, mzee Innocent akitoka nje na wale watu kumvamia.
Kila kitu kilichotokea, Patrick alikuwa akikiangalia, hakujua afanye nini, alimuona baba yake akishambuliwa na vijana wale. Moyo wake ulimuuma mno, akaanza kulia kwa uchungu kichakani pale. Mara baada ya wale vijana kumshambulia baba yake, moja kwa moja wote wakaingia ndani ya nyumba ile.
Patrick hakutaka kuendelea kubaki mahali pale, tayari alikwishaona sehemu ile kuwa na hatari, alichokifanya ni kuanza kukimbia kuelekea porini huku akilia kupita kawaida. Alishuhudia baba yake akiuawa mbele ya macho yake, hakujua kuhusu mama yake, ila moyo wake ulimwambia kuwa mama yake naye aliuawa na vijana wale na kubaki peke yake.
“Wamemuua baba, najua watakuwa wamemuua na mama pia, nitaishi vipi mimi?” alijiuliza huku akiendelea kukimbia kwa kasi kubwa katika pori lililokuwa na giza.
Alikimbia mpaka alipochoka, hakuweza kuendelea na safari yake, ilikuwa ni lazima apumzike, akatulia chini ya mti. Moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, alilia sana, baada ya saa moja akapitiwa na usingizi.
Kilichomuamsha asubuhi zilikuwa sauti za watu waliokuwa wakiongea kwa sauti kubwa. Patrick akashtuka kutoka katika usingizi mzito, macho yake yakatua kwa watu hao, walikuwa wanaume kadhaa walioshika mapanga na marungu mikononi mwake. Hakutaka kujiuliza, akajua kwamba watu hao ndiyo walikuwa wale vijana waliowaua wazazi wake, akaanza kulia kuomba msamaha.
“Naombeni mnisamehe...naombeni mnisamehe, naomba msiniue,” alisema Patrick huku akilia kwa sauti kubwa. Ndiyo kwanza vijana wale wakaziweka sawa silaha zao.
*****
Bi Anna alibaki akitetemeka ndani ya nyumba, hofu kubwa ilimuingia na kuona kwamba muda wake wa kuishi ulikuwa umefika. Ilibidi aondoke ndani ya nyumba ile kukiepuka kifo, akili yake ikafanya kazi ya ziada kwamba kama kukimbia, hakuwa na budi kupitia nyuma ya nyumba ile.
Bahati kubwa kwake ni kwamba vijana wote waliokuwa nyuma ya nyumba walikuwa mbele ya nyumba hiyo kwa ajili ya kumshambulia mumewe hivyo hata alipotoa nyasi upande wa nyuma, ikawa nafuu kwake, akatoka ndani ya nyumba ile bila kuonekana na kuanza kukimbia kwa mwendo wa kasi.
Hakutaka kusimama, katika kipindi hicho kukimbia ndiyo ilikuwa salama yake, porini huko, alichoka lakini hakusimama hata kidogo. Alikimbia kwa dakika zaidi ya thelathini ndipo mbele yake akaanza kuziona nyumba kadhaa zikiwa zimewashwa taa, kidogo moyo wake ukapata ahueni kwa kuona kwamba alikuwa amefika sehemu sahihi, tabasamu la uchungu likaanza kuonekana usoni mwake.
“Asante Mungu kwa kunifikisha huku, naomba unilinde nisiuawe,” alijisema Bi Anna huku akiendelea kupiga hatua kukifuata kijiji kilichokuwa mbele yake.
*****
Patrick alikuwa akilia, moyo wake ulimwambia kwamba watu waliokuwa mbele yake ambao walishika silaha mbalimbali za jadi walikuwa vijana walewale walioiteketeza familia yake. Alikuwa akiomba msamaha pasipo kujua kosa alilolifanya.
Watu hao waliosimama mbele yake hawakuwa maadui, walikuwa wawindaji kutoka katika Kijiji cha Wami kilichokuwa mbali kidogo na mahali hapo walipokuwa. Walibaki wakimwangalia Patrick, hawakuelewa sababu iliyomfanya kulia namna ile.
Mmoja wa vijana wale akamfuata Patrick pale chini alipokuwa na kisha kumuinua. Kitendo hicho kikamfanya Patrick kuhisi kwamba watu hao hawakuwa hatari kwake kama alivyokuwa amehisi kabla.
“Usilie...wewe ni nani na unafanya nini mahali hapa?” aliuliza kijana huyo huku akimwangalia Patrick usoni.
Patrick akaanza kuelezea kila kitu kilichotokea mpaka kuwa mahali hapo. Kila alipokuwa akielezea, alikuwa akilia. Moyo wake ulimuuma mno. Kila mmoja akaonekana kumuonea huruma Patrick aliyeonekana kuhitaji msaada mkubwa.
“Ni lazima tuondoke naye,” alisema kijana mwingine kitu ambacho kilikubaliwa na kila mtu kwani maisha ya Patrick hayakuonekana kuwa salama kabisa.
Safari ya kurudi kijijini ikaanza huku wakiwa pamoja na Patrick. Japokuwa wakati mwingine hakuwaamini vijana hao lakini hakuwa na jinsi, alikuwa kwenye matatizo makubwa, watu haohao ndiyo walionekana kuwa msaada wake, hakuwa na jinsi, akakubali kuondoka nao.
Walitumia dakika hamsini hadi kufika kijijini Wami. Kila mwanakijiji alikuwa akiwaangalia wawindaji wale na Patrick waliyekukuja naye pale kijijini. Safari ikaishia katika eneo la nyumba ya mwenyekiti wa kijiji, mzee Carlos na kumpa taarifa juu ya kila kilichotokea juu ya Patrick.
“Hatuna budi kumsaidia, tutamsaidia mpaka mwisho wa maisha yake,” alisema mzee Carlos, kwa kumwangalia tu isingekupa ugumu kugundua kwamba mzee huyo alikuwa miongoni mwa watu wakarimu sana.
Huku maisha yake yakiendelea katika kijiji hicho ndipo alipogundua kwamba alikuwa na kipaji kikubwa cha kuchora. Uwezo mkubwa aliokuwa nao ulimshangaza mpaka yeye mwenyewe. Alipokuwa akichukua karatasi na kuanza kuchora, picha hizo zilionekana kama kupigwa na kamera.
Wanakijiji walikishangaa kipaji chake, si kwamba hawakuwahi kuwaona watu wengine waliokuwa na uwezo mkubwa wa kuchora, waliwaona ila kipaji alichokuwa nacho Patrick kilikuwa kikubwa sana.
“Unajua sana kuchora,” alisema kijana mmoja huku akiangalia picha ambayo Patrick aliichora kwa ajili yake.
“Asante,” alijibu Patrick ambaye mara nyingi hakuwa muongeaji sana.
Mwezi wa kwanza ukakatika na wa pili kuingia. Wanakijiji walipenda sana kuziangalia picha alizokuwa akizichora kiasi kwamba wengi wao wakatamani kuwa na ukaribu na Patrick. Kila siku aliongeza marafiki waliokuwa wakitamani kuwa karibu naye, katika marafiki haohao ndipo akatokea msichana Victoria.
“Unanikumbuka?” aliuliza msichana huyo.
“Hapana!”
“Mimi ni yule msichana uliyekutana nami jana tulipokuwa kwenye mahafali, kwa nini ulinikimbia?” aliuliza Victoria huku akimwangalia Patrick usoni.
“Niliamua tu!”
“Kwa nini?”
“Basi tu! Niliamua.”
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa urafiki wao, kila alipokuwa Patrick, Victoria alikuwa pembeni yake. Tayari penzi zito likaanza kuingia moyoni mwa Victoria, kila siku hakutaka kukaa na wasichana wenzake, mtu aliyetamani kukaa naye alikuwa Patrick tu.
Moyo wake ukatekwa na penzi zito, alimpenda sana Patrick kiasi kwamba akahisi hawezi kula wala kunywa kwa ajili yake. Ukaribu wake na kijana huyo ndiyo ukawafanya wanakijiji wengine kuhisi kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea kwa watu hao.
Victoria alijua fika kwamba alizaliwa katika familia inayomjua Mungu lakini hilo halikuweza kumzuia kwani kwake, mapenzi yalikuwa na nguvu kubwa kuliko kitu chochote kile. Hakutaka kumuona Patrick akipita katika maisha yake, alitaka awe naye na hivyo kuwa mwanaume wa kwanza kumpa penzi lake.
Alimheshimu sana baba yake ambaye alikwa amemlea katika maisha ya kidini, hakutaka kuzielezea hisia kali za mapenzi ambazo alikuwa nazo juu ya Patrick kwa kuogopa kuuchafua moyo wake kwa kuukaribisha uzinzi moyoni mwake. Akaamua kunyamaza kimya ingawa kila siku moyo wake ulikuwa ukijisikia kumwambia ukweli Patrick.
Victoria alikuwa ameamua, Patrick ndiye alikuwa mwanaume ambaye alikuwa akimtaka katika maisha yake. Alikuwa tayari kukosa kitu chochote katika maisha yake lakini si kumkosa Patrick. Alikuwa tayari kugombana na mtu yeyote yule, hata wazazi wake lakini ili mladi awe pamoja na Patrick.
Kila siku mdomo wake ulikuwa na kigugumizi kila alipotaka kuongea na Patrick juu ya kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea moyoni mwake. Hakujua ni kwa jinsi gani alitakiwa kuufikisha ujumbe huo kwa mvulana mwenye sura nzuri kama Patrick. Siku zilivyozidi kwenda mbele, hatimaye akaamua kujipanga na kumfuata kijana huyo kwani hakutaka kuona akiteseka kila siku katika maisha yake.
“Unaonekana kuwa na kitu unataka kuniambia,” Patrick alimwambia Victoria ambaye alikuwa akimwangalia kwa jicho lilimaanisha kile ambacho kilikuwa moyoni mwake.
“Nani? Mimi?” aliuliza Victoria huku akijifanya kushangaa.
“Ndiyo. Niambie ni kitu gani kinakutatiza moyoni. Au unataka nikuchore na wewe pia?” aliuliza Patrick.
“Nafikiri uko sahihi ila ningependa unisaidie kufanya kitu kimoja. ”
“Kitu gani?”
“Nataka unisindikize sehemu fulani.”
“Wapi?”
“Sehemu fulani.”
“Lakini giza linaingia Victoria.”
“Hata kama. Ninaomba unisindikize Patrick. Nakuombaaaa,” alisema Victoria kwa sauti ya kumtoa nyoka pangoni.
Patrick alimwangalia Victoria mara mbilimbili. Hakuelewa kile Victoria alichokiongea. Kumsindikiza sehemu fulani kwa wakati huo kulionekana kumtatiza mno. Giza lilikuwa likiingia kadri muda ulivyozidi kwenda mbele, hakuelewa ni sehemu gani aliyotakiwa kumsindikiza Victoria.
Kwa kuogopa kumkasirisha, Patrick akainuka. Victoria naye akainuka na kuanza kupiga hatua kuelekea katika sehemu iliyokuwa na kichaka huku wakihakikisha hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akiwaona.
Tayari giza lilikuwa limeanza kuingia, Patrick alionekana kuwa na hofu lakini Victoria hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote ule. Wakaingia porini na kuelekea mbele zaidi, Victoria aliifahamu kila kona japokuwa kulikuwa na giza kubwa.
Walitembea kwa muda mchache, Victoria akaingia katika kichaka, akamtaka Patrick kumfuata. Victoria akakaa vizuri chini na kukifungua kilemba alichokuwa nacho kichwani. Akaichukua khanga ambayo alikuwa ameivaa na kuitandika chini.
“Nakuhitaji Patrick,” alisema Victoria huku akimwangalia Patrick kwa jicho lililojaa utata. Hakutaka kusubiri, alichokifanya ni kumshika na kuanza kumvutia kwake.
“Victoria. Unafanya nini?” aliuliza Patrick.
“Inamaana huelewi kitu Patrick? Naomba unielewe...nakuhitaji..naomba tufanye....nakuomba Patrick...nimezidiwa kwa ajili yako,” alisema Victoria kwa kulalamika.
Patrick akabaki akitetemeka, hakujua afanye nini. Victoria alizidiwa, alionekana kuwa na uhitaji mkubwa wa kupewa kile alichokitaka. Hakujua kitu gani alichotakiwa kufanya kwa. Bado Victoria aliendelea kulalamika kwa sauti iliyojaa mahaba, akili yake ikachanganyikiwa mno.
Japokuwa Patrick alijitahidi kujizuia ili asiweze kufanya kitu chochote kile na Victoria lakini mwisho wa siku akashindwa kabisa, akajikuta akivutwa na msichana huyo na kujikuta akiwa amemlalia juu yake na kilichoendelea baada ya hapo ni kushikana hapa na pale na ndani ya sekunde chache nyasi kuanza kulalamika.
Victoria alilia kwa maumivu makali, hakuwahi kufanya mapenzi na mwanaume yeyote maishani mwake, siku hiyo ndiyo ilikuwa ya kwanza na Patrick ndiye alikuwa mwanaume wa kwanza katika maisha yake kufanya naye mapenzi.
Alilia lakini kitu cha ajabu Patrick hakuondoka juu yake, aliendelea kufanya mchezo ule ambao ulimpa maumivu makali chini ya kitovu. Baada ya dakika kadhaa, wakamaliza, Patrick akaanza kumwangalia Victoria kwa macho yaliyojaa hasira kali.
“Ndiyo tumefanya nini Victoria?” aliuliza Patrick huku akionekana kuwa na hasira kali.
“Unasemaje?”
“Ndiyo tumefanya nini? Angalia Victoria, nimemtenda Mungu wangu dhambi!” Patrick alimwambia Victoria huku akivaa harakaharaka.
“Nilizidiwa Patrick...naomba unisamehe mpenzi.”
“Nani mpenzi wako. Naomba uniache Victoria....nimemtenda Mungu wangu dhambi,” alisema Patrick kwa kulalamika.
Victoria akaanza kuvaa nguo zake, wakati wakiwa wanavaa, ghafla wakasikia minong’ono ya watu ambao hawakuwa mbali sana kutoka pale walipokuwa. Mianga ya tochi ikawamulika usoni hali ambayo ilimpekea Patrick kumuinua Victoria na kuanza kukimbia naye kuelekea mbele zaidi. Watu hao nao wakatoka kichakani na kuanza kuwakimbiza.
Je, nini kitaendelea?
Post a Comment