ad

ad

SI KITU BILA PENZI LAKO-03

 
Bi Anna akazidi kuisogelea nyumba ile huku akiwa na matumaini makubwa moyoni mwake. Akazidi kupiga hatua kuifuata nyumba ile. Mlango ulikuwa umefungwa, Bi Anna akaanza kuugonga huku akionekana kuwa na hofu kubwa. Wala hazikupita sekunde nyingi, mlango ukafunguliwa na kijana mmoja.
Bi Anna akakaribishwa, akaingia ndani. Akakaa kwenye kiti. Mwili ulikuwa ukimtetemeka kwa hofu, machozi yalikuwa yakimtoka huku akilia. Picha ya mumewe alivyokuwa akishambuliwa na vijana wa Kijiji cha Chibe ilionekana kichwani mwake.
Moyo wake ulimuuma, alijiona kuwa katika wakati mgumu kuliko nyakati zote alizopitia katika maisha yake. Kijana yule akabaki akimwangalia huku koroboi ikiwasaidia kuonana mahali hapo.
“Karibu! Mbona unalia?” aliuliza kijana yule.
Hata kabla hajajibu chochote kile, mlango mmoja wa chumba kimoja ukafunguliwa na mzee moja kutoka. Anna akamwangalia mzee yule, hakuwa akimfahamu na wala hakuwahi kumuona katika maisha yake. Bi Anna akaaanza kulia tena, machozi yakaanza tena kutiririka mashavuni mwake.
“Kuna nini tena? Mbona huyu mwanamke yupo hapa ndani akilia?” aliuliza mzee huyo huku akimwangalia mwanamke huyo aliyeendelea kulia.
“Nimemkaribisha akiwa katika hali hii. Nimejaribu kumuuliza lakini bado analia, nafikiri tumpe dakika kadhaa,” alijibu kijana yule.
Bi Anna aliendelea kulia zaidi na zaidi huku mzee Jumanne akimbembeleza kwa kumtaka kumwambia ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea katika maisha yake. Zilimchukua dakika tano, akanyamaza na kuanza kuelezea kila kitu kilichotokea.
“Pole sana. Inasikitisha mno,” mzee Jumanne alimwambia Anna.
“Naomba mnisaidie...naomba mnisaidie,” Bi Anna aliwaambia.
“Kama tukisema ukae hapa, bado unaweza kuonekana. Si unajua kutoka hapa mpaka kijijini Chibe siyo mbali sana. Wanaweza wakaja na kukukamata,” alisema mzee Jumanne.
“Kwani hapa ni wapi?”
“Hiki ni Kijiji cha Usule,” mzee Jumanne alimwambia Bi Anna na kuendelea:
“Tutakusaidia kwa kukupeleka kwa mdogo wangu katika Kijiji cha Itilima, utaishi huko na kuangalia maisha yako ya mbele,” alisema mzee Jumanne.
“Nashukuru sana....asanteni kwa msaada wenu,” Bi Anna aliwashukuru.
“Na vipi kuhusu kijana wako? Naye walimuua pia?” aliuliza mzee Jumanne.
“Najua watakuwa wamemuua. Alikuwa amechelewa sana kurudi nyumbani, kwa vyovyote vile watakuwa wamemuua. Inaniuma sana kubaki peke yangu katika familia yangu. Nimekuwa mpweke, sijui kama nitapata furaha katika maisha yangu yaliyobakia,” alisema Bi Anna.
Bi Anna akalala ndani ya nyumba ile katika usiku huo. Usingizi kwake haukuwa wa amani, ulikuwa wa mang’amung’mu. Kila wakati alikuwa akishtuka, bado wasiwasi wa vijana wale kumfuata hadi kule ulikuwa umemtawala moyoni.
Asubuhi ilipofika, Omari akamchukua katika baiskeli yake na kuanza kumpeleka katika Kijiji cha Itilima. Njia hazikuwa nzuri sana, wakati mwingine alikuwa akishuka kutoka katika baiskeli na kisha Omari kuibeba. Walipita katika milima na mabonde, Kijiji cha Itilima kilikuwa mbali tofauti na alivyofikiria kabla.
Walichukua saa nne, wakaingia katika kijiji hicho na moja kwa moja kuelekea katika nyumba ya mzee Ubuge. Omari akamuelezea mzee huyo kila kitu kuhusu Bi Anna. Mzee Ubuge akaonekana kusikitika kupita kiasi, habari ile aliyopewa ilimuogopesha sana.
Hakuwa na jinsi, akamkaribisha Bi Anna ndani ya nyumba yake hiyo aliyokuwa akiishi na mkewe. Akapewa chumba kimoja na maisha yake kuanza mahali hapo. Kila wakati alikuwa akimshukuru Mungu kwa kumuwezesha kufika mahali hapo ambapo alipaona kuwa na usalama.
*****
Hakukuwa na mwanakijiji katika kijiji cha Wami ambaye hakuwa akimfahamu mzee Samson Carlos, alikuwa mmoja wa watu waliokuwa maarufu na waliopenda dini sana katika kijiji hicho.
Mzee huyu alikuwa miongoni mwa watu wakarimu, waliopenda Mungu na kupenda dini kuliko kitu chochote kile. Alikuwa na watoto watatu, wavulana wawili, Samuel na Richard na pia alikuwa na binti ambaye ndiye alikuwa huyo Victoria.
Aliwalea watoto wake katika mazingira ya dini, kila siku alihakikisha anakaa nao ndani ya nyumba yake na kufanya ibada, hakukuwa na kitu kilichoonekana kuwa muhimu katika maisha yake na maisha ya watoto wake kama kumtumikia Mungu.
Alijua ni jinsi gani wasichana walikuwa na maisha magumu na yaliyojaa majaribu mengi kijijini hapo. Alichokifanya ni kumuwekea msimamo wake wa kuipenda dini binti yake, Victoria kitu ambacho kilifanikiwa kwa asilimia mia moja.
Miaka yote hiyo Victoria alionekana kuwa msichana mwenye heshima, asiyependa wanaume wala kusikia kitu chochote kutoka kwao. Wanaume hawakuweza kumuacha, kwa sababu alikuwa msichana mrembo, mwenye kuvutia walijaribu bahati zao lakini wote hawakuambulia kitu chochote kile, lile penzi walilokusudia kulipata, hawakulipata.
Siku ziliendelea kukatika mpaka Patrick alipoingia ndani ya kijiji hicho. Huyo ndiye mtu pekee aliyeyabadilisha maisha ya Victoria kiasi kwamba hata wanakijiji wakaonekana kumshangaa. Kila kitu kilichokuwa kikiendelea, kaka zake walikifuatilia, hawakuwa kimya, walimwambia dhahiri baba yao kwamba uhusiano kati ya Victoria na Patrick ulikuwa wenye mashaka tele kiasi kwamba mzee huyo akamuita Victoria kuzungumza naye.
“Kuna nini kinaendelea?” aliuliza mzee huyo.
“Hakuna kitu baba!”
“Una uhakika Vick?”
“Ndiyo! Ni rafiki yangu tu!”
Hayo ndiyo maneno aliyosema kila alipokuwa akiulizwa. Kaka zake hawakuaha kumuatilia, kila siku walihakikisha wanamfuatiliakwa karibu zaidi kwani walihisi kwamba wangeweza kupata kitu chochote kile na kuwa na ushahidi ulioshiba.
Katika kufuatilia kwao, ndiyo siku ya tukio ilipofika, wakawaona wawili hao wakisimama na kuanza kwenda porini. Wakajua kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, walichokifanya ni kuchukua tochi na kuanza kuwafuatilia huko mpaka walipowaona wakiwa wamesimama katika kichaka baada ya kufanya mapenzi na hivyo kuanza kuwakimbiza.
Patrick na Victoria walikuwa wakikimbia kwa kasi. Kila mmoja aliiona hatari iliyokuwa mbele yao. Bado tochi ziliwamulika hali iliyowafanya kuongeza kasi zaidi. Walikimbia kwa umbali mrefu, hawakujua ni watu gani waliokuwa wakiwakimbiza muda huo.
Baada ya kukimbia kwa umbali mrefu, wakaingia kichakani na kujificha. Samuel na Richard wakapita kwa kasi huku wakimulika tochi zao huku na kule. Patrick na Victoria hawakuonekana mahali walipokuwa wamejificha.
“Victoria, hawa watakuwa watu wa kijijini kwenu,” alisema Patrick na kuendelea:
“Siwezi kurudi kijijini kwenu tena, ni lazima niondoke. Huu si mwisho wa safari yangu, nitaendelea mbele. Najua hapa siyo mwisho wa maisha yangu Victoria,” alisema Patrick.
“Usiondoke Patrick...usiniache peke yangu,” alisema Victoria huku akilia.
“Haina jinsi Victoria, ni lazima niondoke na kuendelea na safari yangu,” alisema Patrick.
“Inamaana hutorudi tena? Ina maana huu ndiyo mwisho wa mimi na wewe kuonana?” aliuliza Victoria.
“Huu si mwisho. Tutaendelea kuonana Victoria. Nitarudi kijijini kwenu. Nitarudi kwa ajili ya kukuoa tu. Kama kuna mtu atakuja na kutaka kukuoa....kataa, nitarudi kwa ajili yako,” alisema Patrick huku akimwangalia Victoria usoni.
“Nimekuelewa. Kamwe sitoolewa na mwanaume mwingine zaidi yako. Nitakusubiri mpaka utakaporudi,” Victoria alimwambia Patrick.
“Ni lazima nitarudi Victoria. Maisha yangu si kitu bila wewe. Yaani SI KITU BILA PENZI LAKO. Ni lazima nitakurudia” Patrick alimwambia Victoria kisha kumbusu mdomoni na kuondoka huku akimuacha Victoria akilia na kusimama njiani akiwasubiria watu waliokuwa wakiwakimbiza.

JE, nini kitaendelea?

No comments

Powered by Blogger.