MAKONDA NA MADAWA YA KULEVYA, VITA INAYOHAMIA KWENYE UOGA NA USHABIKI
Na Saleh Ally
JUNI
18, 1971 Rais wa Marekani wakati huo, Richard Nixon alitangaza rasmi
kuwa madawa ya kulevya ndiyo adui namba moja wa taifa hilo. Akisisitiza
vita imeanza na adui huyo ni lazima apigwe na kuangushwa.
Nixon alitangaza hilo mbele ya waandishi wa habari baada ya kuwa amezungumza na viongozi wa nchi.
Vita
hiyo haijawahi kusimama na sasa imefikia Marekani inatumia hadi dola
bilioni 51 (Sh trilioni 112) kwa mwaka kwa ajili ya vita ya madawa ya
kulevya.
Hapa
nyumbani, mkuu wa mkoa wa jiji kubwa zaidi nchini, Dar es Salaam, Paul
Makonda, ameanzisha vita ya kupambana na madawa ya kulevya na tayari
watuhumiwa wamekuwa wakitajwa na kufika kwenye Kituo Kikuu cha Polisi
cha Dar es Salaam maarufu kama sentro kuhojiwa na wengine wamefikishwa
mahakamani.
Vita
ya Makonda dhidi ya madawa ya kulevya si yake kwa kuwa anawapigania
Watanzania na nguvu kazi ya taifa letu ambayo inaonekana kuingia kwenye
“fasheni” ya matumizi ya madawa hayo inayoanzisha mambo mengi mabaya kwa
ajili ya taifa.
Kitu kibaya zaidi, madawa hayana faida zaidi ya wachache wanaoingiza fedha huku nguvu kazi ya nchi yetu ikiteketea.
Hasara
za madawa ya kulevya au unga kama ilivyo maarufu ni kuua nguvu kazi ya
taifa kwa njia nyingi kama vijana kushindwa tena kufikiri kiushindani,
kutokuwa wabunifu, kusambazwa kwa kasi kwa virusi vya Ukimwi na hata
kusambazwa kwa tabia za kishoga.
Kama
itatotea mtu akampinga katika vita hiyo, nitasema akapimwe kwa kuwa
athari zinapozidi kuwa juu basi kila mmoja zitamkuta. Ndiyo maana nchi
kama Marekani imeamua kutumia mabilioni ya dola kuhakikisha inaikomesha,
lakini ajabu kabisa, haijawahi kukoma.
Ukitaka
kujua vita ya madawa si ya leo, Marekani walianzisha sheria mwaka 1931
kupambana nayo. Sasa wanapeleka hadi dola milioni 500 nchini Colombia
pekee kuhakikisha wanaidhibiti kwa kuwa huko ndiyo matatizo makubwa. Na inaelezwa imefikia hadi watu 50,000 hupoteza maisha katika vita dhidi ya madawa.
Hii
ni vita ya dunia nzima, lakini Marekani wamekuwa waathirika wakubwa kwa
kuwa soko kuu liko nchini humo ndiyo maana nilianza kutolea mfano.
Vita
inayoendeshwa na Makonda ni ya sisi sote lakini binafsi nimekuwa
nikiona haiendi katika njia sahihi inayoweza kutoa picha kwamba kweli
imelenga hasa kuwakamata wauzaji au wasambazaji sahihi.
Tumeona
wasanii mbalimbali kama akina Wema Sepetu, Khaleed Mohammed ‘TID’,
Hamidu Chambuso ‘Dogo Hamidu au Nyandu Toz’, Anna Kimario, ‘Tunda’,
Winifrida Josephat ‘Recho’ na wengine wakiitwa sentro na kufikishwa
mahakamani na baadaye wakaachiwa kwa dhamana kwamba watakuwa chini ya
uangalizi kwa mmoja na miwili.
Tumeona
watu wengine maarufu zaidi kama Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf
Manji na mfanyabiashara mkubwa pia kiongozi wa dini, Askofu Josephat
Gwajima, pia wakiitwa kama sehemu ya watuhumiwa.
Mbunge
wa zamani wa Kinondoni (CCM), Iddi Azzan na mwenyekiti wa chama namba
moja cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe akiitwa pia, hata hivyo aligoma kwenda.
Wengi
wameitwa kwa tuhuma au lengo la kusaidia. Kwa maelezo kwamba
wanatuhumiwa kutumia au kusambaza lakini lengo ni kuisaidia polisi. Hii
imezua mazungumzo mengi pembeni wengi wakiamini si sahihi.
Mimi
naungana na wale wanaoamini kuna makosa mengi katika njia ya upambanaji
huu. Hasa unapoona watu wanatangazwa siku mbili kabla, baada ya hapo
wanafika kituoni wakiingia na kupigwa picha, baada ya hapo wanachukuliwa
kwenda kupekuliwa nyumbani kwao na ofisini.
Ninaanza
kuwaza tofauti kama kweli hii ni vita sahihi ya madawa ya kulevya au
ina nia nyingine? Kama haina, basi ninaamini wahusika wanaikosea na
huenda wamekosa angalau wa kuwapa ushauri tu wa wazi kwa nia njema.
Mbaya
zaidi, walioanzisha mjadala pembeni wamekuwa waoga kwa kuwa inaonekana
ukimwambia Makonda umekosea basi utakuwa matatizoni. Hili ni jambo baya
kabisa kwa nchi kama yetu, watu kuwa na hofu hata ya kusema ukweli kwa
lengo la kujenga kwamba “utashughulikiwa”, siamini hilo.
Hata
vyombo vya habari navyo vimeshindwa kuwa huru na kusema kweli kwa nia
ya kujenga. Waandishi nao wana hofu ya “kushughulikiwa?” Acha mimi niwe
wa kwanza.
Wanaoshindwa
kusema, wanazidi kuivuruga hii vita, badala ya kulenga kuwaokoa ndugu
zetu na kuwakomesha wanaofaidika nayo kwa kuliumiza taifa letu, wapo
walioigeuza kuwa ya ushabiki wa Yanga na Simba au kama ile ya zile timu
za mtandaoni, “Team Diamond”, “Team Kiba”. Hii si sahihi hata kidogo.
Hatuwezi
kuwa na taifa la watu waoga, wasioweza kusema au kuchangia jambo kwa
nia nzuri eti unaogopa kushughulikiwa au kukamatwa. Tanzania ni yetu
sote, si ya Makonda pekee na kwa kuwa vita aliyoianzisha ina nia njema
kama alivyoeleza basi tuichangie na kuingiza mawazo chanya ili kuisaidia
ifanikiwe.
Lakini
bado ninaona, katika vita hiyo kuna haja ya kuheshimu na kuthamini utu
wa watu na kuepusha kuifanya ionekane ni ya kisiasa au ya visasi. Tuhuma
kwenda hadharani bila ya uhakika hata kidogo, si sahihi. Tukumbuke
wahusika wana biashara zao, familia zao, watu wanaoawaamini. Lazima
ubinadamu wao uthaminiwe.
Jeshi
letu la polisi lina wataalamu wengi wenye ujuzi wa juu kabisa. Huenda
linaweza likafanya mambo yake kwa uhakika zaidi kuliko mfumo unaotumika
wa watu kwenda polisi kama wanakwenda kwenye mkutano wa kampeni.
Kama
Marekani wanapambana na vita hiyo miaka nenda rudi tena kwa njia rundo
za kitaalamu na hadi leo mtandao wa madawa unaendelea kuwasumbua, basi
lazima tujue hii haiwezi kuwa vita ya shoo na ikafanikiwa.
Tangu
mwaka 1971, Rais Nixon alipotangaza rasmi madawa ya kulevya ni adui
namba moja wa Marekani, zimeshaandikwa ripoti zaidi ya 50 zikionyesha
namna walivyofeli katika kupambana na madawa ya kulevya na zimetumika
kuboresha njia za vita hiyo inayoonekana kutokuwa na mwisho.
Kumekuwa
na kila aina ya njia za kupambana kwa kuwa wauza unga ni kama kinyonga,
wanabadilika kulingana na mazingira, mtandao wao mkubwa pia ni watu
wenye nguvu kubwa. Siamini kwa mwendo huu wa kutaja majina kwa
matangazo, watu wakaenda na kupokelewa na vyombo vya habari ndiyo vita
sahihi pekee.
Mwaka
2000, Marekani walifikia bajeti ya dola bilioni 18.4 kupambana na
madawa huku Jiji la New York likitumia 17% ya bajeti yake katika suala
la madawa pekee. Kiasi hicho kilitumika katika masuala la tiba,
ushawishi wa kuepuka madawa hayo haramu lakini pia uchunguzi wa kina
yaani research, nini cha kufanya, wapi sehemu zilizoathirika, nini
kifanyike na wapi pa kushikilia.
Sisi
hatujafanya research ya kutosha, hakuwezi kuwa na research ya wiki au
mwezi kuhusiana na suala hili halafu tukasema imeanza kufanyiwa kazi.
Tutakuwa tumekurupuka, lazima kuwe na utulivu na wataalamu washirikishwe
hasa huku wakipewa nafasi.
Tumeona
wanaokamatwa asilimia 85 ni watu maarufu. Nani anataka kunithibitishia
hakuna wasio maarufu wameathirika? Hakuna maarufu wanaotumia au kuuza?
Sasa kwa nini wale maarufu tu? Vipi hatujaona hata mmoja ambaye
hatukumtarajia?
Nani
anaamini wanaotumia ni wasanii wa Bongo Movie na Bongo Fleva pekee?
Ndiyo maana nasisitiza, kuna shida katika mwenendo wa vita aliyoianzisha
Makonda na huu ndiyo mchango wangu kwamba vizuri ikaenda kuwa vita
iliyolenga kweli kulimaliza tatizo hili ambalo si dogo na si rahisi
kulimaliza kama tunavyoona.
Kuhofia
kumueleza Makonda ni kuendelea kuifanya vita hiyo kuwa ngumu zaidi na
kuendelea kupoteza muda wote kwa mashabiki wa Simba kuwabeza wa Yanga
kwa kuwa kiongozi wao katajwa, huku Yanga nao wakisema hata wao kiongozi
wao katajwa pia.
Lengo si kuonyesha kina nani wamekosea au kina nani si wasafi. Lengo ni kupambana na madawa ya kulevya kuokoa nguvu kazi.
Wabunge
walipoibuka na kupinga mambo kadhaa ya kampeni hiyo ya Makonda walikuwa
sawa kukosoa. Huenda naye hakufurahishwa akatoa kauli ambayo pia
haikuwa sahihi.
Kweli
Bunge ni mhimili unaojitegemea, ndiyo unaotunga sheria za nchi na una
haki ya kuzisimamia. Naamini bila ya kukosea hakuna aliye juu ya sheria.
Huenda ‘approach’ ya uzungumzaji ya wabunge ilimkera Makonda, lakini
huwezi kulizuia bunge kusema.
Unaona
sasa, mjadala umegeuka, umekuwa ni Makonda kuhojiwa na kamati ya bunge.
Hii naona ni sehemu nyingine itakayopunguza vita hiyo ya madawa ya
kulevya na kusababisha ndani ya vita hiyo kuwa na vita nyingine ya
Makonda na wabunge na mwisho itawapa ahueni wasambazaji, wauzaji na hata
watumiaji kuendelea na mambo yao kama kawaida.
Mwenendo
sahihi ndiyo utafanya vita hii iwe sahihi. La sivyo, itakuwa ni vita ya
muda mfupi na baada ya hapo mambo yataendelea kama kawaida, huku wako
wakiwa wamechafuliwa kimakosa au kuonewa kwa kuwa hawakuwa na nguvu ya
kujitetea.
Katika
ripoti ya mwaka 2012 ya Umoja wa Mataifa (UN) ya madawa ya kulevya,
imeeleza takribani watu 200,000 kila mwaka hupoteza maisha kutokana na
madawa hayo haramu kwa maana ya afya pekee.
Dunia hutumia hadi dola bilioni 250 (zaidi ya Sh trilioni 547) kwa mwaka ili kuwasaidia waathirika kwa njia sahihi.
Ripoti
hiyo imeeleza watu milioni 230 au asilimia 5 ya watu duniani kote
wameathirika na madawa hayo haramu na wanawake wanaonekana kuwa
waathirika wakubwa zaidi.
Hii
si vita ndogo wala fupi. Tumuunge mkono Makonda na Rais John Pombe
Magufuli ambaye ameeleza nia yake ya kupambana. Watu wawe huru na
kuchangia kwa maoni chanya ya kujenga ikiwezekana kulisaidia Jeshi la
Polisi kwa kulionyesha njia za wahusika.
Isiwe
kutajana kwa visasi na wivu unaolenga kukomoana, pia Makonda awe tayari
kupokea maoni kwa kuwa hawezi kuwa sahihi katika kila kitu.
Nisisitize
hatuwezi kuwa taifa la hofu tupu tukafanikiwa, lakini hatuwezi kuwa
sahihi kwa kutaka kukosoa kwa kuharibu au kukatisha tamaa.
Mimi
nawaasa, tusiifanye vita hii ni ya siasa au Usimba na Yanga au Udiamond
na Ualikiba. Watu muwe huru, tuendelee kuifanya Tanzania kuwa Free
Land, Land of Democracy na tuichangie vita hii tukiamini inatuokoa sisi,
familia zetu na vizazi vyetu vijavyo.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
Post a Comment