ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI-24

 
NYEMO CHILONGANI
“Dokta...dokta...” aliita msichana mmoja, alikuwa nesi aliyekuwa akikimbia kuelekea katika ofisi ya dokta mkuu, watu wote waliomsikia, walimshangaa, alikuwa akikimbia huku akionekana kuwa na haraka sana, kama alikuwa na jambo fulani alilotaka kumwambia daktari aliyekuwa akimfuata, alipoufikia mlango, akaufungua na kuingia ndani.
Dokta Sam aliyekuwa ndani ya ofisi hiyo akamwangalia nesi huyo huku amimshangaa, alitaka kusikia kile alichokuwa amemfuata ndani ya ofisi yake. Nesi huyo akamwambia kwamba mgonjwa aliyekuwa ameletwa ndani ya hospitali hiyo na kupoteza fahamu kwa wiki mbili, hatimaye aliyafumbua macho yake pale kitandani alipokuwa.
“Unasemaje?”
“Godson amefumbua macho,” alisema nesi huyo.
Dk. Sam hakutaka kubaki ofisini kwake, naye akachomoka na kuelekea kule kulipokuwa na chumba alicholazwa Godson, alipofika, akamwangalia kitandani pale, kweli, baada ya kulala kitandani kwa wiki mbili mfululizo huku akiwa hajitambui, hatimaye mgonjwa huyo aliyafumbua macho yake na kuangalia huku na kule.
Godson hakukumbuka kitu, hakujua mahali alipokuwa palikuwa wapi. Aliangalia huku na kule kwa mshangao mkubwa, alipoiona dripu iliyokuwa ikining’inia juu yake ndipo akagundua kwamba mahali hapo palikuwa ni hospitalini.
“Nimefikaje?” alijiuliza.
Hapo ndipo akajaribu kukumbuka tukio la mwisho kabisa alilokuwa amelifanya. Alimbuka kwamba alikuwa ndani ya gari, alipofika Sinza Makaburini kwenye kona ya kuelekea Barabara ya Sam Nujoma, kuna gari lilikuja mbele yake na kuligonga gari alilokuwepo, baada ya hapo, hakukumbuka kitu gani kiliendelea.
“Nilipata ajali?” alijiuliza kitandani pale.
Muda wote huo Dk. Sam alisimama pembeni na kumwangalia mwanaume huyo, kwake, kile kilichokuwa kikionekana kilikuwa muujiza mkubwa, hakuamini alichokuwa akikiona mahali hapo.
Ni kweli walikuwa wakipokea wagonjwa kila siku lakini kwa jinsi Godson alivyokuwa ameumia na kupoteza fahamu, moyo wake ulimwambia wazi kwamba mwanaume huyo asingerudiwa na fahamu na ni lazima angekufa palepale kitandani.
“Dok..ta...mp..en..zi wan..gu..yup..o wap..i..?” aliuliza Godson kwa tabu kabisa huku akisikia maumivu makali.
“Subiri! Pata muda wa kupumzika kwanza,” alisema Dk Sam huku akimuweka vizuri kitandani pale.
Alishindwa kuwataarifu wazazi wake kutokana na muda kwenda sana. Ilikuwa ni saa nane usiku, hakuona kama lingekuwa jambo muhimu kuwapigia simu na wakati asubuhi inayofuata tu watu hao wangekuwa hospitalini hapo.
Godson hakuacha kumuulizia mpenzi wake, alikuwa hoi lakini hakuona kama hiyo ilikuwa sababu ya kutokuwa na mpenzi wake mahali hapo. Muda ulizidi kusogea huku Godson akitamani kumuona mpenzi wake, Melania.
Ilipofika saa 1:30 asubuhi, akapewa taarifa kwamba mpenzi wake na wazazi wake walikuwa hospitalini hapo kwa ajili ya kumuona. Akatamani kuonana nao na hivyo muda wa kuona wagonjwa ulipofika, watu hao wakaingia humo ndani.
Kitendo cha Melania kumuona mpenzi wake akiwa amefumbua macho, akamsogelea, alipomfikia, akamkumbatia huku akitiririkwa na machozi mashavuni mwake. Kilipita kipindi kirefu, alikata tamaa, aliona kama Mungu asingeweza kumrudishia fahamu mpenzi wake, kila alipokuwa akimwangalia, alikuwa akilia tu lakini siku hiyo, machozi yake ya majonzi yakabadilika na kuwa machozi yenye furaha.
“Umerudiwa na fahamu mpenzi...umerudiwa na fahamu mpenzi...” alisema Melania huku akimwangalia mpenzi wake ambaye kila alipokuwa akijibu, mwili wake ulikuwa ukiuma.
Furaha ikarudi moyoni mwake, Melania hakutaka kuondoka hospitalini hapo, muda wa kuona wagonjwa ulipokwisha, alitoka ndani na kukaa kwenye mabenchi yaliyokuwepo mahali hapo. Huyo ndiye alikuwa mtu muhimu katika maisha yake, moyo wake ulikosa tumaini, alikataliwa na William, mtu pekee ambaye aliamini kwamba angempa furaha katika maisha yake yaliyobaki alikuwa Godson tu.
“Mungu! Naomba umponye kabisa mpenzi wangu! Sina furaha, sina amani moyoni. Mungu, unajua kwamba nimeumia sana, naomba unifariji, naomba umponye mpenzi wangu,” alisema Melania huku akiyafuta machozi yake pale kwenye benchi alipokaa.
****
“Inakuwaje washikaji? Niliwaambia mkamuue yule mbweha, mbona hamjakamilisha kazi yangu?” aliuliza Nicholaus huku akiwa ameshika simu.
“Kazi ipi?”
“Ya yule mshikaji!”
“Yule aliyepata ajali Sinza?”
“Ndiyo!”
“Mbona alikufa kitambo tu! Nahisi hata kuzika washazika!”
“Acheni masihara! Huyo mtu hakufa!”
“Hakufa? Kivipi? Kaka uliuona ule mzinga wenyewe lakini?” aliuliza jamaa aliyekuwa upande wa pili ambaye alikuwa akizungumza na Nicholaus.
Nicholaus akawaambia kwamba mtu huyo hakufa bali alikuwa hoi hospitalini. Katika kila hatua ambayo Godson alikuwa akipitia, Nicholaus alifuatilia. Kila siku ilikuwa ni lazima kwenda hospitalini na kufuatilia. Alipoambiwa kwamba Godson alikuwa akipata nafuu, moyo wake ulimuuma sana.
Siku zikakatika na ndipo alipoamua kuwaambia watu hao ukweli kwamba mtu aliyewaambia wamuue alikuwa mzima wa afya na mbaya zaidi hali yake iliendelea kutengemaa mpaka kurudiwa na fahamu.
Vijana hao wakamwambia kwamba wangekamilisha kazi hiyo haraka iwezekanavyo. Hawakutaka kukaa makao makuu tu bali walichokifanya ni kupanga mikakati ya kumuua Godson palepale kitandani alipokuwa.
“Huyu tutamuua! Tutajifanya madaktari,” alisema jamaa mmoja.
“Basi haina shida! Tufanyeni juu chini mpaka tufanikiwe,” alisema kijana mwingine.
****
Mzee yule mwindaji, Caspean Hill aliendelea kupita kwenye bomba lile kubwa kuelekea upande wa pili. Alikuwa akitambaa kwa kasi sana kwa kuamini kwamba wale watu waliokuwa nyuma yake ambao aliwaacha kwenye handaki lile wangeweza kumfuata kule alipokuwa na kumuua.
Hakutaka kukubali, hakutaka kuona akiuawa kizembe namna ile, aliendelea kwenda mbele mpaka alipofika mwisho wa bomba lile ambapo kwa chini kulikuwa na mto ulioonekana kuganda na barafu kutanda juu yake, alichokifanya ni kupanda kwa juu na kuelekea njia ileile aliyoelekea William.
Alipiga hatua huku bunduki ikiwa mikononi mwake, tayari alijua kwamba William alikuwa mtu muhimu sana, mwanaume huyo alikuwa fedha, alikuwa utajiri wake ambao piga ua ilikuwa ni lazima ampate na kuwakabidhi CIA ambao walikumtafuta kwa udi na uvumba.
Alipiga hatua mpaka alipofika katika baada ile aliyokuwa William. Hakuhisi kama mtu huyo alikuwa mahali hapo kwani kwa jinsi alivyoonekana, ilikuwa ni lazima kutoka nje kabisa ya eneo hilo, hivyo akapuuza.
Alipopiga hatua kadhaa, ghafla akasikia mlio mkubwa wa risasi kutoka ndani ya baa ile. Machale yakamcheza, kitu kilichokuja akilini mwake ni jina la William tu, hivyo kwa haraka sana akaanza kuelekea kule kulipokuwa na baa ile, tena kwa mwendo wa kasi.
Alipofika kwenye kidirisha kidogo cha kioo, akachungulia ndani, macho yake yakatua kwa watu watano waliomzunguka mtu mmoja mahali hapo. Akapeleka macho yake kwa mtu aliyezungukwa na kugundua kwamba alikuwa William, tena mwanaume mmoja alimnyooshea bastola na kutaka kumpiga risasi nyingine.
Mzee Caspean hakutaka kuchelewa, hapohapo akanyoonesha bastola yake kwa watu wale na kuachia risasi mbili, moja ikapiga bega la jamaa aliyetaka kumuua William na nyingine ikampata jamaa mwingine maeneo ya ubavuni akaanguka chini na damu kuanza kuwatoka.
Wale wengine walipoona hivyo, wakaanza kukimbia kwa kupitia mlango wa nyuma. Walichanganyikiwa, walishambuliwa na mtu ambaye hawakujua alikuwa wapi. Si wao tu bali hata wauzaji na wahudumu ndani ya baa ile wote wakakimbia kuelekea nje kwa kupitia mlango wa nyuma.
Mzee yule akachomoka dirishani na kuelekea kule alipokuwa William, alipomfikia, akamuinamia na kumuweka juu ya kiti na kumtaka kutulia kwani alikuwa kwenye mikono salama, akaanza kumpa huduma ya kwanza.
“Wewe ni nani?” aliuliza Mzee Caspean, alijifanya hajui, alitaka kumsikia mwenyewe akilitaja jina lake.
“William,” alijibu William kwa sauti ndogo.
“Unafanya nini huku? Na kwa nini unatafutwa?”
“Nilitekwa!”
“Ulitekwa? Na nani? Warusi huwa hawatekwi kirahisi!” alisema mzee huyo.
“Mimi siyo Mrusi!”
“Siyo Mrusi! Ni nani sasa?”
“Mwafrika!”
“Mwafrika? Kivipi?”
William akaanza kumwambia kila kitu kilichotokea, Mzee Caspean hakuamini, alimwangalia vizuri mtu huyo, ilikuwa vigumu kugundua kama alikuwa Mwafrika. Akamnyanyua na kumpeleka bafuni, huko, akachukua maji ya moto kidogo na kumwagia na kuanza kumtoa sura ambayo aliambiwa kwamba alikuwa nayo.
Kweli, alipoanza kumtoa sura ile ya bandia ndipo akaamini kwamba mtu huyo alikuwa Mwafrika kama alivyosema. Hakuishia hapo, mwili mzima alikuwa amebandikwa vitu vilivyoonyesha kwamba alikuwa Mrusi hivyo kutolewa vyote na kubaki kama alivyozaliwa.
Mzee Caspean alishangaa, hakuamini kile alichokiona. Mwanaume aliyesimama mbele yake alikuwa mbaya mno, alifanana na sokwe, yeye mwenye alitamani kukimbia kwani alihisi kwamba mtu huyo hakuwa binadamu, bali alikuwa mfano wa sokwe mtu.
“Nahitaji laptop,” alisema William huku akionekana kuwa na maumivu makali.
“Laptop tu au kompyuta yoyote?” aliuliza mzee huyo.
“Yoyote ile.”
“Sidhani kama tunaweza kuipata. Hebu tutoke hapa.”
Wakatoka na kuelekea nje huku Mzee Caspean akiwa amemshika kwa kuupitisha mkono wa William begani mwake, huko, wakaanza kuangalia huku na kule, kwa bahati nzuri kwao wakafanikiwa kuziona nyumba kadhaa na hivyo kuifuata nyumba moja ambayo nje kulikuwa na theluji kila kona, tena nyingine zikiendelea kudondoka.
Walipoifikia, wakagonga mlango ambapo baada ya sekunde kadhaa, ukafunguliwa na msichana mmoja aliyeonekana kuwa mrembo wa sura. Alipomuona William, ilikuwa bado kidogo aufunge mlango kwani alimuogopa mno, hakuamini kama huyo alikuwa binadamu, alihisi Mzee Caspean alikwenda hapo na sokwe.
“Tunahitaji msaada wako!” alisema Mzee Caspean, wakati akiyazungumza maneno hayo, alikuwa akiusukuma mlango na kuingia ndani.
“Msaada gani?”
“Kompyuta!”
Kwanza msichana huyo aliogopa, hakujua watu hao walikuwa wakina nani na kwa nini walihitaji kompyuta. Walimwambia kwamba walikuwa watu wazuri ambao hawakuwa na tatizo lolote lile, msichana huyo hakuridhika, William akamwambia kwamba yeye ndiye alikuwa William, mwanaume aliyeanzisha Mtandao wa MeChat.
“Wewe ndiye William wa MeChat?” aliuliza msichana huyo huku akionekana kushtuka.
“Ndiyo!”
Kitu cha kwanza alichokifanya msichana huyo ni kuchukua boksi kubwa la chumba lililoandikwa Fist Aid Kit ambalo lilikuwa na dawa kadhaa kisha kuanza kumuhudumia William aliyeonekana kuwa kwenye maumivu makali.
Baada ya msichana huyo kumaliza kumuhudumia William, akasimama na kuelekea ndani, baada ya sekunde kadhaa akarudi huku akiwa ameongozana na kaka yake ambaye sura yake ilionyesha tabasamu pana, hakuamini kama siku hiyo William alikuwa ndani ya nyumba yao.
Mtandao wake ulikuwa umekimbiliwa kwa kasi, watu walikuwa wakiutumia, ndani ya muda mchache ulikuwa na watu wengi kupita kawaida. Kaka wa msichana huyo alipomuona William, hakuamini, alimfahamu kwa kuwa mara ya kwanza alimuona kwenye televisheni.
Alichokifanya ni kupiga naye picha kwa staili ya selfie huku akionekana kuwa na furaha kupita kawaida. Alipomaliza, akamgawia laptop kama alivyoomba, William akaifungua na kuanza kubadilisha baadhi ya vitu katika mtandao wake.
“Unaweka nini?”
“Subiri. Utaona,” alisema William huku akiendelea kuchezea kompyuta yake, alichokifanya kaka wa msichana yule ni kuzichukue zile picha alizopiga na William kisha kuzituma kwenye akaunti yake kama lengo la kuwaambia marafiki zake kwamba alikuwa mtu wa kwanza kupiga picha na mwanzilishi wa mtandao huo.
“I make them feel jealous on me,” (nataka wasikie wivu juu yangu) alisema kijana huyo huku akitabasamu.
****
Maofisa wa CIA na FBI walichanganyikiwa, waliwasiliana na wenzao waliokuwa nchini Canada na kuwauliza kuhusu William lakini watu hao waliwaambia kwamba hawakufanikiwa kumpata William. Hawakujua tatizo lilikuwa nini kwani Mzee Caspean aliwapigia simu na kuwaambia kwamba alikuwa na William nyumbani kwake, sasa kwa nini wasimpate?
Waliwauliza kama walikutana na huyo mzee, maofisa hao wakawaambia kwamba walikutana na ugumu kwani dalili zinaonyesha kwamba simu zao walizitraki, kwani walipofika hapo, tayari Warusi walikuwa mahali hapo na walimchukua mzee huyo na kwenda naye huko.
“Mmh! Warusi? Inakuwaje?”
Maofisa hawakuishia hapo, waliwaambia kila kitu kwamba hata baada ya kwenda kwa mzee huyo, walikuta Warusi wale wakiwa wameuawa kwa risasi na moja kwa moja kumuhusisha mzee huyo ambaye aliwakimbia kwa kupitia kwenye bomba ambalo hawakujua lilipokuwa likiishia.
“Kwa hiyo William hamkumkuta?”
“Ndiyo mkuu!”
“Ooh!”
Kilikuwa ni kitendo kidogo cha kumfuata William nchini Canada na kumchukua lakini ilionekana kuwa na ugumu sana. Maofisa hao wakachanganyikiwa, hawakuelewa sababu zilizozifanya harakati zao za kumpata William kuwa ngumu kiasi hicho.
Wakati wakiendelea kutafakari ni kitu gani walitakiwa kufanya, msichana mmoja akaingia humo huku akionekana kuwa na haraka sana, alipofika, akachukua simu yake na kuwaonyeshea kitu maofisa hao.
Ilikuwa ni picha ya William ambapo alikuwa amepiga na jamaa fulani ambaye kwenye Mtandao wa MeChat alikuwa akitumia jina la O’Brein Cook. Waliiangalia picha ile, William alionekana kuwa kwenye maumivu makali, kwa begani alikuwa akitokwa na damu, japokuwa alifungwa bandeji lakini damu hazikuzuilika kumtoka.
“Track the location,” (Lichunguzeni eneo husika) alisema mkuu wa CIA.
Hilo ndilo lilofanyika, wakaichukua picha ile na kuiingiza kwenye kompyuta zao na kuangalia mahali ilipokuwa imepigwa. Hiyo haikuwa kazi kubwa, ndani ya dakika tano tu majibu yakasoma kwamba picha ile ilikuwa imepigwa nchini Canada katika eneo lililoitwa Winnipeg nchini Canada.
“It’s not far away from where they are,” (si mbali kutoka pale walipo)
“Yeah!”
Hapohapo wakawapigia simu wenzao na kuwaambia mahali William alipokuwa, ilikuwa ni lazima kwenda huko tena haraka iwezekanavyo kwani dalili zilionyesha kwamba kama wangeshindwa kumpata basi Warusi wangeweza kufanya lolote liwezekanalo kumpata.
“Si mbali sana na hapa! Tunakwenda!” alisema jamaa aliyekuwa Canada na hivyo kuanza kwenda huko.
****
“Kwanza ilikuwaje?”
“Nilikuwa nikiishi na baba yangu! Alikuwa akinipenda sana. Maisha yalikuwa mazuri mno, mpaka kufikia kipindi hicho sikuwa nimemfahamu mama yangu. Baada ya kufikisha miaka kumi na nane, baba akanionyeshea mama yangu! Alikuwa mwanamke mzuri sana, alipendeza mno, sura yake ilifanana na sura yangu, aninivutia mpaka mimi mwenyewe.
“Kilio changu siku zote kilikuwa ni kuuwataka warudiane, sikuwa na furaha kuwaona wakiishi mbali mbali hivyo ili kunifanya binti yao nifurahi, wakakubali kuishi pamoja. Maisha yalikuwa mazuri, nilijiona mtu mwenye furaha kuliko watu wote duniani. Baada ya mwaka mmoja, baba yangu akafariki kwenye ajali ya gari iliyotokea Manhattan hivyo kuishi na mama yangu ambaye baadaye aliolewa na mwanaume katili, aliyenitesa na kunipa msongo wa mawazo,” alisema msichana mmoja aliyeitwa Cassey Mike.
Kwa kumwangalia, alikuwa msichana mrembo, alivutia, sauti yake nyororo aliyokuwa akiitumia kuongelea iliwapagawisha wanaume wengi. Alikuwa katika kipindi cha Jerry Springer, alikuwa akiyahadithia maisha yake aliyopitia kipindi cha nyuma.
Japokuwa ilikuwa ni historia tu lakini kila mtu aliyekuwa akiisikiliza aliumia moyoni mwake. Alikuwa msichana mdogo, mwenye utajiri mkubwa lakini hakukuwa na aliyeamini kama kweli alipitia maisha hayo yenye kumsisimua kila mtu aliyekuwa akimsiliza.
“Ikawaje?” aliuliza Jerry, watu wote waliokuwa wakikifuatilia kipindi hicho walikuwa kimya, Casey ndiye aliyeutawala ukumbi huo huku kituo cha televesheni cha CNN kikionyesha moja kwa moja kilichokuwa kikiendelea huku kila mtu akitaka kusikia kwa kifupi maisha aliyopitia msichana huyo bilionea na mwanamitindo maarufu duniani.

Je, nini kitaendelea?
Natumaini hadithi ndefu na mmeifurahia.

No comments

Powered by Blogger.