ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI-25


·NYEMO CHILONGANI
Msichana Cassey aliendelea kusimulia historia ya maisha yake, kila mtu aliyekuwa akimsikiliza aliumia moyoni mwake, matukio aliyokuwa amepitia, jinsi baba wa kambo alivyomtesa, wanawake waliomsikiliza walikuwa wakitiririkwa na machozi tu.
Hiyo ilikuwa historia ya maisha yake. Iliisha, ilipita na katika kipindi hicho alikuwa na maisha mengine kabisa, maisha ya kuogelea katika ulimwengu wa pesa. Alikuwa na kiasi kikubwa cha pesa, alimiliki kampuni, magari ya kifahari na nyumba za bei mbaya zilizokuwa Las Vegas. Calfornia na sehemu nyingine nyingi nchini humo.
Kila alipokuwa, watu walimuheshimu Cassey, japokuwa alikuwa binti mdogo lakini alipendwa mpaka na mabilionea wengi ambao kila siku walitamani hata kulala naye kitandani.
Cassey hakuwa mwepesi, aliwachukia wanaume kwa ajili ya baba wa kambo. Mambo aliyofanyiwa katika maisha yake, kwake, kila mwanaume aliyekuwa akikutana naye alionekana kama shetani. Hakuwa mwepesi, hakujirahisisha hata kidogo, kwake, ilikuwa ni bora kufanya mapenzi na midoli ya kiume kuliko mwanaume.
“Na vipi kuhusu wanaume?” aliuliza Jerry Springer.
“Ninawachukia wanaume, sipendi hata kuwaona,” alisema Cassey huku akimwangalia Jerry.
“Kwa hiyo hata mimi unanichukia?”
“Hahah! Jerry bhana! Kwani wewe unanitaka?” aliuliza Cassey na kuanza kucheka.
Alichokizungumza ndiyo ukweli wenyewe. Kulikuwa na wanaume wengi waliomfuata na kumwambia walimpenda lakini aliwakatalia. Walikwenda mabilionea, wacheza filamu, tenisi, waendesha magari ya Formula One, wachezaji wa kikapu na baseball lakini wote hao aliwakatalia kwa kuwaambia kwamba aliwachukia wanaume mno.
Tangu alipokuwa akibakwa na baba wa kambo, hakutaka tena kuwa na mpenzi, kwa kuwa aliwachukia wanaume, alichokifanya ni kununua mdoli wa kiume nchini China na kuupeleka nyumbani kwake, California, na ndiyo mdoli ambao ulimaliza shida zake kitandani.
Hayo yalikuwa maisha yake, hakutaka kuficha, aliwaambia watu wengi kwamba alishiriki mapenzi na mdoli uliokuwa nyumbani kwake. Wengi walimshangaa, walimuona mtu wa ajabu lakini hakutaka kujali, bado msisitizo wake ulikuwa uleule kwamba aliwachukia wanaume.
Baada ya kuzungumza sana, akamwambia Jerry kwamba alitaka kutengeneza kitabu cha maisha yake, alitaka kuwaandikia wale waliokuwa wakilelewa maisha ya hovyo kwamba bado walikuwa na nafasi ya kupata mafanikio, haikujalisha walipitia matatizo gani, kama Mungu alitaka kuwanyooshea katika maisha yao basi wangefanikiwa na kuwa matajiri wakubwa huko mbele.
Alipoondoka katika ukumbi huo alipokuwa akifanyiwa mahojiano, akaelekea nyumbani kwake. Kichwani mwake alikuwa na mawazo tele, alitaka kuandika kitabu cha historia ya maisha yake, alitaka kuyaweka maisha hayo kwenye kitabu, akutane na mwandishi wa vitabu na kumuandikia lakini hakujua ni nani alistahili kukiandika kitabu hicho.
“Labda Chilongani,” alijisemea ndani ya gari.
Monye Chilongani Mtanzania aliyekuwa akiishi Philadelphia nchini Marekani, alikuwa mmoja wa waandishi wakubwa duniani. Alikuwa miongoni mwa waandishi walioandika vitabu vya watu wengi akiwemo Barack Obama, Celine Dion, Tiger Woods na wengine wengine. Kwake, mwandishi huyo alionkana kuwa bora hivyo alichokifanya ni kutafuta mawasiliano naye na kumpigia simu.
“I can’t do that right now,” (siwezi kufanya hivyo kwa sasa?) alisema mwandishi huyo alipopigiwa simu.
“Why?” (kwa nini?)
“I got something to do Cassey, but thank you,” (nina kitu cha kufanya, ila nashukuru)
“What is it?” (kitu gani?)
“I do write Trump’s book, so I’ve to travel here and there. Maybe, let’s do it next year,” (ninaandika kitabu cha maisha ya Trump kwa hiyo natakiwa kusafikiri huku na kule. Labda tufanye mwaka ujao) alisema Monye kwenye simu.
“Next year? I can’t wait.” (mwaka ujao? Siwezi kusubiri)
Hakuwa na jinsi, alitamani sana kitabu chake kiandikwe na mwandishi huyo lakini iliposhindikana, akaamua kuwatafuta waandishi wengine na kufanikiwa kumpata mwandishi wa Kifaransa aliyeitwa Babi D’e Consious ambaye ndiye alitakiwa kukiandika kitabu hicho.
“Hakuna shida. Dola milioni 1.5,” alisema Babi.
“Hakuna tatizo!”
Hilo likamalizika na kilichokuwa kimebaki ni kuendelea kuwasiliana na mwandishi huyo ambaye alifika nchini Marekani na kuanza kukiandika kitabu hicho. Muda mwingi aliokuwa akisimulia matukio yaliyokuwa yakitokea, Cassey alikuwa akilia, hakuamini kama kulikuwa na binadamu ambaye aliwahi kupitia maisha kama aliyokuwa amepitia kipindi cha nyuma.
Siku zikakatika, baada ya kukatika miezi miwili, kitabu kikakamilika, kikachapishwa na kitu kilichokuwa kimebaki ni kukitangaza kwa ajili ya kuingia sokoni. Akawatafuta watu wengi ambao walimsaidia kumfanyia matangazo mbalimbali, alipomaliza, kuna sehemu moja tu ambayo alitakiwa kufanya matangazo hayo, sehemu yenye nguvu ambayo aliamini kwamba ingemsaidia kuuza.
“Ni lazima nikitangaze kwenye Mtandao wa MeChat kwa ajili ya kuwafikia watu wengi zaidi,” alisema msichana huyo, alichotakiwa kufanya ni kuwasiliana na William, mmiliki wa mtandao huo kwa ajili ya kumfanyia kazi yake.
****
Linda hakuwa na furaha, moyo wake ulikuwa na mawazo mno. Muda mwingi alikuwa akilia akimtaka Mungu amrudishe mpenzi wake salama nyumbani. Hakuacha kuwasiliana na maofisa wa FBI na CIA ambao pia walitumia muda wao mwingi kuwaweka walinzi wao alipokuwa akiishi kwa kuamini kwamba Warusi wangeweza kumteka ili William awafanyie kazi yao.
Tangu mpenzi wake atekwe, zilipita siku mbili hakuwa amelala, kitanda kilionekana kuwa na miba kila sehemu, asingeweza kulala na wakati mpaka muda huo hakujua mahali alipokuwa mpenzi wake.
Maofisa wa FBI walimpa moyo kwamba mpenzi wake angeweza kupatikana, hakutaka kuliamini hilo kwa asilimia mia moja, alitaka kuona likifanyika na kuletewa nyumbani kwake, hapo ndipo angeamini kwamba kazi ilifanyika na kuwa na amani moyoni mwake.
Siku ya tatu ilipoingia, akapigiwa simu na kuambiwa kwamba William alipatikana nchini Canada katika Mji wa Winnipeg. Hakuamini, akataka kumuona au kuwasiliana naye. Hilo halikuwezekana kwani kwa kipindi hicho William alikuwa kwenye hali mbaya kutokana na risasi alizokuwa amepigwa.
“Ila ninataka kuzungumza naye!”
“Utazungumza naye akifika. Kwa sasa yupo kwenye hali mbaya,” alisikika mwanaume kwenye simu.
“Atakufa?” aliuliza huku akilia.
“Hapana! Hawezi kufa,” alijibu mwanaume huyo na kukata simu. Japokuwa aliambiwa kwamba mpenzi wake asingekufa, moyo wake ulikuwa na hofu kupita kawaida.
****
Maofisa wa CIA hawakuchelewa, kwa haraka wakafika mahali ambapo waliambiwa kwamba William alikuwepo. Walipofika hapo, wakaizunguka nyumba na kuingia ndani huku wakipiga kelele kwamba wao walikuwa CIA.
Mzee Caspean baada ya kusikia hivyo, akatupa bastola yake chini, wanaume wanne wakaingia na kumuweka chini ya ulinzi na kumbeba William aliyekuwa kwenye kochi huku akiwa hoi. Hawakuzungumza kitu, yeye na mzee huyo wakapakiwa kwenye gari na kuondoka mahali hapo.
William alikuwa akilia kwa maumivu makali. Alipoteza kiasi kikubwa cha damu na kadiri dakika zilivyokuwa zikisonga mbele zilionyesha kwamba angeweza kufariki akiwa njiani. Wakafika salama mjini Winnipeg ambapo akapelekwa katika Hospitali ya St. Carthbert ambapo akalazwa kitandani huku akiwa hoi.
Madaktari wakaanza kuifanya kazi yao, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutoa risasi zilizokuwa mwilini mwake. Kila mmoja alishangaa, kwa jinsi alivyokuwa amejeruhiwa ilikuwa vigumu sana kwa mtu kukaa kwa kipindi kirefu huku akiwa hai kwani alikuwa na majeraha makubwa katika sehemu zile alizokuwa amepigwa risasi.
Simu zikapigwa mpaka nchini Marekani, wakawaambia kwamba William alipatikana akiwa hoi na katika kipindi hicho alikuwa akitibiwa hospitalini. Kila mmoja akaonekana kuwa na furaha tele, hawakuamini kama maofisa wa CIA wangefanya kazi hiyo kwa haraka sana mara baada ya kupewa taarifa juu ya mahali alipokuwa mtu huyo.
Baada ya kukaa kwa saa moja na kutibiwa huku akiandaliwa kwa ajili ya safari, William na Mzee Caspean ambaye kichwa chake kiliendelea kufikiria pesa, wakachukuliwa na kupelekwa ndani ya ndege kwa ajili ya kupelekwa nchini Marekani.
Kutoka Winnipeg mpaka Marekani haikuwa mbali, walichukua dakika arobaini na tano tu, ndege ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK jijini New York ambapo hapo kulikuwa na magari zaidi ya kumi yakiwasubiri watu hao.
“How is he?” (anaendeleaje?) aliuliza jamaa mmoja.
“He is just fine,” (anaendelea vizuri tu)
Wote wakachukuliwa na kupakizwa ndani ya gari ambalo lilianza safari ya kuelekea katika Hospitali ya Main View Medical Center iliyokuwa hapohapo New York. Msafara wake ulikuwa mkubwa, zaidi ya magari kumi yalikuwa yakiongoza huku kila mtu aliyekuwepo katika msafara huo akiwa na silaha nzito kwani mtu waliyekuwa wakimlinda alikuwa na heshima kubwa, mtu ambaye alionekana kuwa na thamani kuliko hata waziri mkuu wa nchi hiyo.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika hospitalini hapo ambapo William akaanza kupatiwa matibabu huku chumba alichokuwepo kikilindwa kwa ulinzi mkali kwa kuepuka kutekwa tena na Warusi, ulinzi huo haukuwa ndani tu, hata nje ya jengo hilo bado kulikuwa na watu waliokuwa na silaha, kwa muonekano tu, ilionyesha kama rais wa nchi hiyo alikuwa humo kupata matibabu.
Siku hiyohiyo baada ya Linda kupigiwa simu, akaondoka jijini Massachuesetts na kuelekea New York huku akiwa kwenye hali ya ujazito aliyokuwa nayo. Ndani ya ndege, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria mpenzi wake, alimuomba Mungu kwa hali aliyokuwa nayo, hakutaka kumuona mwanaume huyo akiondoka mikononi mwake kwani ndiye mtu pekee ambaye aliamini kwamba angeweza kumfariji katika maisha yake.
Alipofika, akapokelewa na kupelekwa huko hospitali. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuelekea hospitalini huku maofisa wa CIA wakiwa wanamlinda kila hatua kwa kuepuka utekaji, akachukuliwa mpaka hospitalini huko.
Kitendo cha kumuona mpenzi wake kitandani, akatabasamu, naye William akarudisha tabasamu pana. Akamsogelea pale alipokuwa na kumjulia hali. William akafurahi mno, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kulishika tumbo la Linda.
“Anaendeleaje?” alimuuliza Linda.
“Ni mzima! Anaendelea vizuri na amekukumbuka pia,” alisema Linda huku akiachia tabasamu pana.
Rais akapigiwa simu na kuambiwa kwamba William alipatikana na walikuwa naye mikononi mwao. Japokuwa kulikuwa na ulinzi mkubwa lakini rais huyo akaagiza ulinzi uongezeke kwani mtu waliyekuwa naye alikuwa muhimu kuliko katiba ya nchi hiyo kipindi hicho.
Hilo likafanyika, polisi wakawekwa, ndani ya hospitali hiyo, wakawekwa maofisa wengine wa CIA waliojifanya kuwa madaktari kumbe nyuma ya pazia bado waliendelea kuhakikisha ulinzi unafanyika vya kutosha humo ndani.
Watu walipotangaziwa kwamba William amepatikana, kila mmoja akashusha pumzi, wakafurahi kwani wengi wakaona kwamba huo ndiyo ulikuwa muda wa kuutumia Mtandao wa MeCat uliokuwa ukijiendesha wenyewe, tena kwa kasi kubwa huku mamilioni ya watu wakiendelea kujiunga kila siku.
Mzee Caspean hakutaka kuondoka, moyo wake ulikuwa na furaha, hakuamini kama kweli William yule aliyekuwa amemsikia kwa kipindi kifupi, genius aliyekuwa ametikisa dunia ndiye yule ambaye alimsaidia, moyoni mwake akajiona mkombozi ambaye alitakiwa kuheshimiwa na kila mtu kwani bila yeye, mtu huyo angeweza kuuawa kitambo tu.
William alikaa hospitalini kwa muda wa mwezi mzima ndipo aliporudi nyumbani kwake. Akaendelea kuingiza fedha kupitia mtandao wake ambao ulionekana kuwa bora kuliko mitandao yote duniani.
Makampuni hayakuacha kujiunga na kujitangaza huko, kila siku ilikuwa ni lazima kampuni mpya kujiunga na kumpa kiasi kikubwa William. Akaanza kuwa bilionea, kwake, hakuangalia pesa, hakuangalia heshima, kitu pekee alichokiangalia ni kuwapa watu kile walichokuwa wakikihitaji.
Hakutaka kumuacha Mzee Caspean, aliyaokoa maisha yake, aliuthamini mchango wake hivyo baada ya kulipwa dola milioni moja, William akamuongezea nyingine na kumnunulia jumba kubwa la kifahari pembezoni mwa Jiji la Ottawa nchini Canada, karibu na bahari.
“Hii ni yangu?” aliuliza Mzee Caspean mara baada ya kutumiwa picha ya jumba alilonunuliwa.
“Ndiyo! Hiyo ni nyumba yako!”
“Siamini!”
“Ishi katika imani! Hii ni nyumba yako!” alisema William huku akiachia tabasamu pana.
Siku ziliendelea kukatika, baada ya mwezi mwingine kuingia, akapokea ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwa msichana mrembo, Cassey aliyetaka kuonana naye kwa kuwa alikuwa na kazi kubwa aliyotaka kufanya naye.
Alishangaa, alizoea kumsoma msichana huyo kwenye majarida, umaarufu wake, utajiri wake ulitisha sana na hakuamini kama kipindi hicho msichana huyo alitaka kuonana naye. Hilo halikuwa tatizo, akawasiliana naye na kumwambia amfuate ofisini kwake, ndani ya saa mbili, msichana huyo alikuwa amekwishafika.
“Ninataka kumuona William,” alisema Cassey.
Dada wa mapokezi aliambiwa kuhusu yeye, hakukuwa na tatizo, akamchukua na kumpeleka katika ofisi ya bosi wake. Alipofika, wakasalimiana na msichana huyo kukaa kwenye kochi, akakunja nne, upaja wake mweupe, ulionona, uliofunikwa na sketi yake fupi ukaonekana, William akaukodolea macho kama vile aliona kitu kigeni.
“Unashangaa nini?” aliuliza Cassey huku akiachia tabasamu, na kwa mbali alijiweka vizuri ili upaja uendelee kumtoa udenda mwanaume huyo.
“Jinsi Mungu anavyojua kuumba. Mungu fundi sana aisee,” alisema William huku akimwangalia Cassey kwa jicho lililomaanisha kitu cha tofauti kabisa.
Japokuwa msichana huyo alicheka kwa kuhisi kwamba ni masihara, lakini kwa William, kile alichokizungumza alimaanisha, alitokea kuvutiwa na msichana huyo lakini kabla hajasema kitu chochote juu ya uzuri aliokuwa nao Cassey, picha ya Linda akiwa kitandani ikamjia kichwani mwake. Akachanganyikiwa.

Je, nini kitaendelea?

No comments

Powered by Blogger.