ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI-23

 
NYEMO CHILONGANI
Saa kadhaa zilikatika, William alikuwa kwenye hali mbaya, muda wote alikuwa kimya, alionekana kama tayari alikuwa mfu. Pale alipokuwa, hakuweza kusogeza kiungo chake chochote kile na hata kuufumbua mdomo wake alishindwa kabisa.
Ilipofika saa 7:26 usiku, hali yake ikaanza kurudi kama ilivyokuwa, akaanza kupata nafuu na kitu cha kwanza kabisa alichokihisi ni kuona vidole vyake vikianza kusogea huku na kule. Akajitahidi kuinuka pale alipokuwa, akashindwa kabisa lakini kidogo viungo vyake vilianza kupata nafuu.
Hakusimama pale alipotoka, alitulia na kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele na ndivyo alivyokuwa akipata nafuu. Ilipofika asubuhi, mwili ukawa na nguvu tena lakini hakutaka kujionyesha, hakutaka kumuonyeshea mzee yule kwamba alikuwa amerudi katika hali ya kawaida.
Mwindaji yule hakujua kama William alirudi kwenye hali yake ya kawaida, akamnywesha uji kama kawaida na alipoona mwanaume huyo akitangazwa kwenye televisheni kwa kutumia sura ile ya bandia aliyokuwa nayo, akaondoka kwa ajili ya kuwasiliana na CIA.
Huku nyuma William hakutaka kukaa, akasimama, akajaribu kutoka ndani ya handaki lile kwani mpaka hapo alipofikia, hakutakiwa kumwamini mtu yeyote yule.
Akasimama na kujaribu kwenda nje, kulikuwa na baridi kali mno, hakutaka kwenda huko, alichokifanya ni kurudi ndani, akaangalia huku na kule ndipo akakutana na bomba kubwa likiwa limeelekea upande mwingine kabisa.
Hakutaka kusubiri, alijua kwa namna moja au nyingine ilikuwa ni lazima bomba hilo lielekee sehemu ambayo aliamini ingekuwa salama kwa maisha yake. Akaingia ndani ya bomba lile na kuanza kutambaa kuelekea upande wa pili kabisa ambao hakujua ni upande gani.
Japokuwa mule kulitakiwa kuwa na joto lakini kwa kipindi cha baridi kali kama kipindi hicho, hakukuwa na joto lolote lile, kulikuwa na baridi kali na muda wote meno yake yalikuwa yakigonganagongana tu.
Alitambaa kwa dakika kumi na tano ndipo akafika mwisho wa bomba lile ambalo lilionyesha kwamba kila kitu kilichokuwa kikipitishwa mule, kilikwenda katika mto mkubwa ambao nao kipindi hicho maji yake yote yaliganda na kuwa barafu.
“Mungu wangu! Nifanye nini?” alijiuliza.
Kwa kuwa aliamini kwamba alikimbia hatari, hakutaka kusubiri mahali hapo, akajitokeza kuanzia kichwani mpaka kifuani kwa staili ya kulala chali, akalishikilia bomba lile na kupanda juu yake.
Ilikuwa kazi kubwa kwa mtu kama yeye ambaye mwili wake haukuwa na nguvu za kutosha lakini hakuwa na jinsi, alipopanda, kilichofuata ni kuondoka mahali hapo. Alishindwa kujua sehemu alipokuwa akielekea, kulikuwa ni porini, pori ambalo miti yake yote ilikuwa imetawaliwa na theluji nyingi, hakutaka kusimama sehemu, aliendelea kusonga mbele huku akisikia baridi kali japokuwa mwilini mwake alikuwa na sweta zito lililokuwa na skafu shingoni mwake.
Safari yake hiyo ikaishia sehemu ambayo kulikuwa na mgahawa huku kukiwa na magari manne ambayo yalikuwa yakitumika kusafishia njia kwa ajili ya wakazi wa eneo hilo kupitisha magari yao, akaelekea kule kulipokuwa na magari yale, kwa bahati nzuri kwake akakutana na msichana mmoja mrembo ambaye kwa kumkadiria tu hakuwa na miaka zaidi ya kumi na tano.
“Do you speak English?” (unazungumza Kiingereza?) alimuuliza.
“Yes! I do! What can I help you si?” (ndiyo! Ninazungumza! Nikusaidie nini bwana mkubwa?) aliuliza msichana huyo aliyekuwa na mbwa wake pembeni.
“Where am I?” (nipo wapi?)
“What do you mean?” (unamaanisha nini?)
“I mean where am I right now?” (namaanisha nipo wapi sasa hivi?)
“Winkler...”
“What the hell is Winkler?” (ndiyo wapi huko)
“Southern Winnipeg, Canada,” Kusini mwa Winnipeg, nchini Canada) alijibu msichana yule.
“Is there any phone booth around?” (kuna kibanda cha simu karibu?) aliuliza William.
“Yeah!”
Akaonyeshewa sehemu kulipokuwa na kibanda cha simu, hakikuwa mbali sana na mahali alipokuwa. Akaanza kuelekea huko, hakuacha kutetemeka, japokuwa mwilini mwake kulikuwa na sweta, jaketi kubwa lakini alihisi baridi ikiingia mpaka kwenye mifupa yake.
Akafika katika kibanda hicho, akajipekua mfukoni na kutoa senti hamsini aliyokuwa nayo na kuiweka kwenye simu kisha kumpigia mpenzi wake Linda. Simu iliita, iliita na kuita lakini haikuwa ikikpokelewa na mwisho wa siku kuambiwa kuacha ujumbe mfupi.
“Linda! Naomba unisaidie, nipo Canada sehemu inayoitwa Winkler. Nipo hai, sikufa, naomba uwaambie FBI kwamba nipo hai ila wakichelewa watakuta nimekufa,” alisema William na kisha kukata simu.
Alitamani kubaki kibandani kwa kuamini kwamba Linda atakapowaambia FBI basi ingekuwa rahisi kwao kumfuata mahali pale ila tatizo lilikuwa ni baridi lililokuwa likipiga.
Hakuvumilia kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea sehemu iliyokuwa na baa na kuingia ndani ambapo kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakilewa pombe kali.
Kila mtu aliyemuona William akiingia, alibaki akimshangaa, ilikuwa vigumu sana kwa kumuona Mrusi akiingia ndani ya baa zilizokuwa zikimilikiwa na Canada kutokana na ugomvi uliokuwepo baina yao.
Walimshangaa, hawakujua mwanaume huyo alijiamini nini na wakati wao walikuwa wengi ndani ya baa hiyo. Muziki uliokuwa ukipigwa kwa sauti ya chini, ukazimwa kabisa, wale waliokuwa na silaha pembeni, wakazishikilia kisiri kwani ilikuwa ni lazima kumpiga mwanaume huyo ambaye aliingia kwenye anga zao kwa kuwa hata Wacanada waliokuwa wakielekea nchini Urusi, nao walikuwa wakipigwa sana na wengine kuuawa.
William hakujua kitu chochote kile, hakujua kwamba ile sura ya bandia aliyokuwa amevishwa ndiyo iliyokuwa ikimuharibia. Hakuzungumza na kitu, alikwenda katika meza moja na kutulia chini.
“Nikusaidie nini?” aliuliza mhudumu mmoja, japokuwa uso wake ulikuwa kwenye tabasamu lakini William aligundua kwamba tabasamu hilo halikutoka moyoni.
“John Walker!”
Mhudumu huyo akaondoka, hata kabla hajarudi, wanaume wawili wakasimama na kuanza kumfuata kule alipokuwa. Walipofika katika meza ile, nao wakachukua viti na kukalia katika meza ile.
William alibaki akishangaa, hakujua sababu iliyowafanya watu hao watoke kule walipokuwa mpaka katika meza yake, akagundua kwamba kulikuwa na kitu. Hakuwasalimia, alinyamaza, mwanaume mmoja akaegemea kiti makusudi na kuifanya bastola yake kuonekana kiunoni.
“Umekuja kufanya nini humu Mrusi?” aliuliza jamaa mmoja, sura yake ilionyesha dhahiri kwamba kuua halikuwa jambo gumu kwake.
“Nani? Mimi? Mimi siyo Mrusi.”
“Sikiliza, kaka yangu aliuawa nchini Urusi mwaka jana, baba yangu aliuawa hukohuko pia kwa vitu visivyoeleweka kwamba ni chuki binafsi. Kila unayemuona humu ndani, ndugu yake aliuawa nchini Urusi. Tulijiapiza kulipiza kisasi, wakati tukiwa na hasira sana juu yenu, hatimaye umeingia kwenye kumi na nane zetu,” alisema jamaa mwingine, wale waliokuwa pembeni wakaanza kusogea kule walipokuwa.
“Francis...” aliita jamaa mmoja aliyekuwa mbali.
“Unasemaje!”
“Unamchelewesha, unamuhoji kwani wewe mwandishi wa habari?” alisema jamaa mmoja aliyekuwa kaunta, alichokifanya ni kusogea kule walipokuwa, alipofika kwenye meza ile, akachomoa bastola yake, akampiga risasi mbili William, moja ikaenda kwenye bega la kushoto na nyingine kuzama kwenye mbavu zake, hapohapo akaanguka chini, damu nyingi zikaanza kumtoka.
“Mmalizie kabisa,” alisema jamaa mwingine, jamaa yule akaichukua bastola yake, akamnyooshea tena William, alidhamiria kuua, mlio wa risasi ukasikika, damu zilizokuwa zikimtoka William, zikaongezeka pale sakafuni alipokuwa amelala.
“Aagghh...” alipiga kelele William sakafuni pale huku akiwa kwenye maumivu makali, akaona kabisa mtoa roho alimkaribia na alitaka kuitoa roho yake

Je, nini kitaendelea?
William amekufa?

No comments

Powered by Blogger.