FUTA MACHOZI MPENZI -18
NYEMO CHILONGANI
Linda alikuwa chumbani, moyo wake ulikuwa na hofu tele, hakujua ni kitu gani kiliufanya moyo wake kuwa namna hiyo, alikosa furaha, amani ikapotea kabisa. Akasimama kutoka kitandani na kuanza kutembea huku na kule, aliogopa kwani kwa kawaida anapokuwa katika hali hiyo basi ilikuwa ni lazima kuwe na jambo baya mbele yake.
Hakujua ni jambo gani. Kitu cha kwanza kabisa kilichokuja kichwani mwake kilikuwa ni mpenzi wake, William. Akaichukua simu yake na kuanza kumpigia, simu ilikuwa ikiita, iliita na kuita lakini haikupokelewa.
Akashikwa na hofu zaidi kuona kwamba inawezekana kulikuwa na jambo baya hivyo akamwandikia ujumbe kwamba kama angeuona basi ampigie kwa kuhisi inawezekana alikuwa sehemu yenye kelele ambapo hakuweza kuisikia simu yake ikiita.
Hakupata usingizi, alijaribu kulala lakini usingizi haikumjia kabisa. Mawazo yelimuendesha, muda ulizidi kwenda mbele lakini mpenzi wake hakupiga simu, hivyo akampigia Borya.
Kama ilivyokuwa kwa William, hata naye hakupokea simu ile, akashikwa na hofu kwamba inawezekana walipata ajali wakati wakirudi kwani haikuwa kawaida kwa wote wawili kutokupokea simu.
Usiku huo ukawa wa mateso tele, mpaka asubuhi inaingia William hakuwa amerudi chumbani kitu kilichomfanya kuwasiliana na uongozi wa chuo. Hakukuwa na aliyeamini kile walichoambiwa, haikuwa rahisi kwa William kwenda sehemu na kulala hukohuko. Taarifa za kupotea kwake zikasambazwa chuoni hapo mpaka kuwafikia maofisa wa FBI ambao walipewa jukumu la kumlinda chuoni hapo.
“What? This is impossible!” (nini? Haiwezekani!) alisikika mwanaume kwenye simu.
“He got lost,” (amepotea)
“How?” (kivipi?)
Maofisa wa FBI walichanganyikiwa, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumtafuta Linda ambaye aliwaambia kwamba usiku uliopita aliondoka na rafiki yake, Borya kwenda kwenye sherehe ya kuzaliwa ya msichana mmoja aitwaye Catherine na baada ya kuondoka, hawakurudi tena.
“Did you try to reach him?” (ulijaribu kumpigia?)
“Yes! I did it several times,” (ndiyo! Nilifanya hivyo mara kadhaa!)
Maofisa hao hawakutaka kukubali, walichokifanya ni kumpigia simu, kama ilivyokuwa kwa Linda, hata kwao simu haikuwa ikipokelewa. Hawakuwa na jinsi, walichokifanya ni kutraki simu yake ili kujua ilikuwa mahali gani. Hilo likafanyika na ndani ya nusu saa, tayari walijua kwamba simu hiyo ilikuwa katika Mtaa wa Livingstone katika ukumbi mmoja ulioitwa Cassanova.
Maofisa hao wakaelekea huko, walipofika, wakaingia ndani, hakukuwa na mtu, waliangalia huku na kule lakini hawakubahatika kumuona mtu yeyote japokuwa bado GPS yao ilionyesha kwamba simu ya William ilikuwa humo ndani.
Wakapiga tena, wakasikia simu ikianza kuita chooni, wakaondoka na kuelekea huko, walipofika, waliikuta simu ikiwa chini lakini William hakuwepo mahali hapo, haikuwa simu yake tu bali hata simu ya Borya ilikuwa pembeni yake hivyo wakazichukua na kuondoka nazo.
Walichanganyikiwa, walijilaumu kwa kutokuwa makini kuhakikisha kwamba William anakuwa kwenye mikono iliyo salama. Waliondoka mpaka katika kituo chao kidogo ambapo kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuchukua simu ya Borya na kuangalia namba alizokuwa amepiga na kupiga.
Katika uwanja wa namba zilizoingia na kutoka, hakukuwa na namba yoyote ile lakini hilo halikuwatisha kwani waliamini kwamba walikuwa na uwezo wa kugundua namba zozote zile hivyo wakaituma namba yake makao makuu na kuomba kutajiwa namba zilizoingia na kutoka na kama iliwezekana basi wachukue mawasiliano yao yaliyofanyika kwa njia ya sauti.
“Tupe dakika ishirini!”
Baada ya dakika ishirini, wakapigiwa simu na kupewa namba zote zilizokuwa zimeingia na kutoka. Hapo ndipo walipopata jibu kwamba mtu aliyekuwa na William alikuwa Mrusi na hata namba ambazo alikuwa akiwasiliana nazo zilitoka katika makao makuu ya Shirika la Ujasusi la KGB nchini humo.
“Tumekwisha! Kumbe yule kijana alikuwa jasusi!” alisema ofisa mmoja wa FBI, kiongozi aliyeitwa Hugh Jackman.
“Unasemaje?”
“Hakikisheni upekuzi unafanyika kila kona. Bado tunahitaji kumfahamu mtu aliyekuwa akiitumia simu hii kwa undani, kama atakuwa nchini ame ameondoka,” alisema Jackman.
Hilo ndilo lililofanyika, ilikuwa ni lazima FBI wahakikishe kwamba mwanaume huyo anapatikana haraka iwezekanavyo. Wakarudi chuoni ambapo huko wakachukua picha ya Borya, wakaangalia picha yake na kuanza kuitafuta katika kompyuta zao.
Nyaraka zake zote zilionekana wazi, ilionyesha ni siku gani aliingia nchini Marekani, alipopitia mpaka kufika katika chuo hicho. Walijilaumu sana, walihisi kwamba Borya alikuwa mtu hatari lakini cha kushangaza hawakuchukua hatua yoyote ile.
“Hebu alama za vidole zake,” alisema Jackman.
“Ngoja tuziskani tuone!”
Wakaichukua simu ile na kuanza kuskani, walitaka kuona alama zake za vidole ili wazitume uwanja wa ndege ambapo hapo wangeangalia kama kwa simu hiyo mtu aliyekuwa na alama hizo za vidole kama aliondoka.
Hilo halikuwa zoezi la muda mrefu, ndani ya dakika tano, wakapewa alama za vidole ambazo zilitumwa hadi uwanja wa ndege sehemu ya kuingilia abiria ambapo baada ya kuangalia, zilionyesha kwamba mtu huyo alipita muda muda mchache uliopita na kuingia kwenye ndege uya Fly Emirates.
“Tunakuja!”
Kila kitu kilichofanyika kwa wakati huo kilifanyika haraka sana. Maofisa hao wakaelekea mpaka uwanja wa ndege, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuangalia picha za kamera kwa siku hiyo. Walipelekwa katika chumba maalumu kilichokuwa na kompyuta nyingi na televisheni na kisha kuonyeshewa picha zote zilizopigwa siku hiyo.
“Hapohapo! SI alipitia geti hili?”
“Ndiyo!”
“Huyu hapa! Yupo na wenzake! Madaktari! Inakuwaje? Nani anaumwa?” aliuliza Jackman.
“Kwa maelezo yaliyotolewa mwanaume mgonjwa anaitwa Vladimir Kulich. Amepooza mwili mzima,” alisema dada yule ambaye ndiye aliyekagua vitambulisho vyao.
“Sasa ilikuwaje apite na wenzake? William alikuwa wapi?”
“Hatujui! Hakukuwa na mtu mweusi waliyepita naye zaidi ya huyu mgonjwa,” alisema dada huyo.
Jackman akachoka, akashusha pumzi ndefu na kutulia kitini. Kila mmoja alikuwa kimya, alimwangalia mwanaume huyo aliyeonekana kuwa na hasira kupita kawaida. Akaanza kuzungukazunguka ndani ya chumba kile huku akionekana kuwa na mawazo tele.
Kila mmoja alikuwa akimsikilizia yeye, walitaka kufahamu ni kitu gani kilitakiwa kufanyika kipindi hicho. Baada ya kukaa katika hali hiyo kwa dakika tano, hapohapo akawarudia.
“Umesema wale waliokuja ni madaktari?” aliuliza.
“Ndiyo!”
“Na mgonjwa alitoka wapi?”
“St. Pius Medical Centre.”
“Hebu wapigieni simu kuwaulizia kuhusu huyu mgonjwa,” alisema Jackman.
Hapohapo alichokisema ndicho kilichofanyika. Namba zikatafutwa na kupigwa kwa ajili ya kumuulizia mgonjwa aliyeitwa Vladimir Kulich. Simu ilipopokelewa na kuuliza swali hilo, mtu aliyekuwa huko hospitalini akaangalia majina ya wagonjwa wote waliokuwepo na hata walioruhusiwa, hakukuwa na mgonjwa mweye jina hilo.
“Hakuna mgonjwa mwenye jina hilo,” alisikika dada wa hospitalini.
“Huyu mgonjwa ni William!” alisema maneno yaliyomfanya kila mtu kushtuka.
“Unasemaje?”
“Huyu mgonjwa ndiye William!” alirudia maneno yake.
Kila mmoja alimshangaa, hawakuamini kama angesema maneno kama hayo. Walimwangalia mgonjwa yule kwenye televisheni ile, alikuwa Mzungu wa Urusi, muonekano wake haukuonekana kama alikuwa William hata mara moja.
“Inawezekana vipi?”
“Kwani huyu mgonjwa alizungumza lolote?”
“Hapana!”
“Ndiyo maana nimewaambi kwamba mgonjwa huyu ni Willia,’ alisema Jackman huku akimwangalia mmoja baada ya mwingine aliyekua ndani ya ndege hiyo.
Kitu alichokitaka ni kujua mahali ndege hiyo ilipofikia, waliamini kwamba safari ya watu hao ilikua ni kwenda nchini Urusi hivyo ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba hata kabla ya ndege hiyo kuwasili nchini humo basi waweze kuishusha ndege hiyo na kumchukua mtu wao.
Wakawasiliana na watu wa mamlaka ya anga uwanjani hapo na kupewa taarifa kwamba bado ndege ilikuwa safarini kuelekea Ottawa nchini Canada hata kabla ya kuelekea nchini Urusi.
“Ilikwishaingia nchini Canada?”
“Bado! Ndiyo inakaribia!”
“Ni lazima ishushwe haraka iwezekanavyo,” alisema Jackman.
Wakati wakiwa wanawasiliana na watu hao, baadaye wakaambiwa kwamba mawasiliano yalikatika na hawakuwa wakiifikia ndege hiyo. Hawakujua watu hao walikuwa wapi, hawakujua kama ndege hiyo ilikuwa safarini au ilipokea hitilafu.
Wakaendelea kuwasiliana nao, wakaifuatilia kwenye rada na kitu kilichowashangaza wote, ndege hiyo haikuweza kuonekana kwenye rada.
Hapo ndiupo maofisa wa FBI wakachanganyikiwa zaidi, kikao cha dharura kikaitishwa katika chumba kidogo makao makuu kwa ajili ya kujadili kitu kilichokuwa kikiendelea. Kila mmoja ndani ya chumba hicho alionekana kuwa na hofu tele, walikuwa radhi kupoteza kitu chochote kile lakini si kumpoteza William ambaye alionekana kuwa mkombozi wao mkubwa katika masuala ya teknolojia. Wakati wakiwa kwenye kikao hicho, mara mlango ukafunguliwa na msichana fulani mrembo kuingia huku akiwa na karatasi mkononi mwake, kila mmoja akamshangaa.
“What is going on?” (nini kinaendelea?) aliuliza jamaa mmoja.
“A plane carrying William has crashed in the Columbia Mountains,” (ndege iliyomchukua William imepata ajali katika milima ya Columbia).
Kila mtu aliyesikia maneno hayo akashtuka, hakuamini kama kweli kile kilichozungumzwa kilikuwa kweli au la. Alichokifanya msichana yule ni kuchukua rimoti iliyokuwa ndani ya chumba kile na kuwasha televisheni, kila kituo cha habari kilikuwa kikionyesha tukio hilo.
Wote kwa pamoja wakajikuta wakishika vichwa kwa huzuni tele, ndege ileile waliyoambiwa kwamba ndiyo iliyombeba William huku akionekana mgonjwa ndiyo iliyopata ajali kwa kuanguka katika milima ya Columbia ambayo asilimia kubwa ilikuwa ni ya mawe iliyokuwa na barafu kubwa.
“At least one fifty people died,” (watu mia moja na hamsini walikuwa wamepoteza maisha,” yalisomeka maneno makubwa yaliyokuwa yakipita yaliyowafanya watu wote kulengwa na machozi kwani idadi hiyo ya watu ndiyo iliyokuwa ndani ya ndege hiyo kubwa ya Fly Emirates.
Je, nini kitaendelea?
Je, William, Warusi na Waarabu wamekufa?
Je, Waarabu waliilipua ndege kama walivyotaka?
Je, William atafikishwa Urusi?
Tukutane Alhamisi mahali hapa.
UKISHARE nitafurahi sana.
Post a Comment