ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI-17

 
NYEMO CHILONGANI
Baada ya kupita saa kadhaa, Melania akarudiwa na fahamu pale kitandani alipokuwa. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kulitaja jina la Godson. Aliangalia huku na kule, alitaka kufahamu mahali alipokuwa, aliona akiwa juu ya kitanda huku kukiwa na dripu iliyokuwa ikining’inia.
Kwa jinsi muonekano ulivyokuwa ndani ya chumba kile, akagundua kwamba alikuwa hospitalini. Alifikaje? Hakujua, na kama aliletwa mahali hapo, alikuwa akiumwa nini na kwa nini mpenzi wake hakuwepo? Hakupata jibu.
Baada ya kukituliza kichwa chake kwa dakika kadhaa ndipo kumbukumbu zikaanza kumrudia. Akakumbuka namna alivyopigiwa simu na kupewa taarifa kwamba mpenzi wake alikuwa amekufa.
Hapohapo alipokuwa, akaanza kulia huku akiliita jina la mpenzi wake, Godson. Moyo wake uliumia mno, hakuamini kama alikuwa akipita katika kipindi kigumu kama hicho. Huku akiwa analia, nesi mmoja akaufungua mlango wa chumba hicho na kumfuata Melania aliyekuwa hapo kitandani.
“Godson yupo wapi? Mpenzi wangu yupo wapi?” aliuliza Melania huku akimwangalia nesi huyo ambaye alikuwa akimtuliza anyamaze kwani hapo alipokuwa palikuwa hospitalini.
Alihisi maumivu makali moyoni mwake, moyo wake ulimwambia kwamba mpenzi wake alikuwa amekufa na ndiyo maana alipigiwa simu na kupewa taarifa. Alitaka kuondoka hospitalini hapo, hakutaka kuendelea kubaki na wakati hakujua hali ya mpenzi wake ilikuwaje.
Kuondoka halikuwua jambo jepesi, akaambiwa atulie mpaka pale atakaporuhusiwa kwani hali yake haikuwa nzuri kama ilivyotakiwa kuwa. Alikaa hospitalini kwa saa kadhaa ndipo mama yake aliporudi kumjulia hali.
Alipomuona tu, akaanza kulia, alimwambia mama yake jinsi moyo wake ulivyokuwa kwenye maumivu makali baada ya kusikia taarifa za kifo cha mpenzi wake, Godson. Hapo ndipo mama yake, Bi Pamela akaanza kumbembeleza na kumtaka anyamaze kwani Godson hakufa kama alivyosikia bali alikuwa hospitali akipatiwa matibabu.
“Mama! Niambie ukweli!”
“Godson hajafa mpenzi! Ni mzima ila madaktari wanaendelea kumpatia matibabu!” alisema Bi Pamela.
Hakukuwa na kitu alichokihitaji Melania kama kumuona mpenzi wake. Hakukaa sana hospitalini, alipotolewa, kitu cha kwanza kilikuwa ni kwenda hospitalini huko kwa ajili ya kumuona Godson.
Walipofika, wakaambiwa wasubiri, wakaungana na wazazi wa mwanaume huyo na kuambiwa wasubiri. Muda wote Melania hakuonekana kuwa na furaha, alionekana kuumia mno moyoni mwake.
Walisubiri kwa siku nzima, wakaambiwa kwamba siku hiyo wasingeweza kumuona hivyo walitakiwa kurudi siku nyingine. Wakaondoka huku wakiwa wamenyong’onyea, nyumbani, Melania alikuwa na hali mbaya, hakula, hakulala, hakufanya kitu chochote kile zaidi ya kukaa na kumfikiria mpenzi wake.
Ilipofika saa sita usiku, akashindwa kuendelea kukaa nyumbani, akaelekea hospitalini, alitaka kufuatilia kila hatua ambayo mpenzi wake alikuwa akipitia. Hakuruhusiwa kumuona, akarudi kwenye benchi na kutulia hapo.
Usiku ulikuwa ni wa mateso sana, alilia mno, alipigwa na baridi lakini hakuwa tayari kuondoka mahali hapo. Moyoni mwake hakuhisi kabisa kwamba ajali ile ilikuwa imepangwa, hakuhisi kabisa kama Nicholaus alihusika katika ajali hiyo, kwake aliichukulia kama ajali ya kawaida ambayo ingeweza kumtokea mtu yeyote yule.
Asubuhi ilipofika, wazazi wa Godson wakafika hospitalini hapo. Walishangaa kumuona Melania akiwa hapo, wakamfuata na kumkumbatia huku wote wakilia. Madaktari hawakutoa tamko juu ya hali aliyokuwa nayo Godson mule ndani, walikuwa watu wa kuwapita huku kila mmoja akionekana kuwa na jambo zito la kuwaambia lakini walishindwa kufanya hivyo.
Baba yake Godson akaonekana kugundua kitu, jinsi madaktari walivyokuwa wakipitia kutoka ndani ya kile chumba na kuwaangalia, walionekana kuwa na kitu mioyoni mwao, kitu kibaya ambacho hawakutaka watu wengine wakifahamu.
“Kuna nini?” aliuliza baba yake Godson huku akiwa amemsimamisha daktari mmoja.
“Hakuna kitu!”
“Mtoto wangu anaendeleaje?”
“Anaendelea vizuri,” alijibu daktari huyo huku akionekana kutokuwa na uhakika na kile alichokuwa akikizungumza.
“Una uhakika?”Daktari hakujibu kitu chochote kile, akaondoka mahali hapo kwenda kuendelea na shughuli zake.
Kitendo hicho kikawatia hofu, mioyo yao ikapata majibu kwamba Godson alikuwa amekufa chumbani mule hivyo ilikuwa ni lazima madaktari wasite kuwaambia ukweli. Wakachanganyikiwa, Melania akazidi kulia kwa sauti mpaka madaktari wengine walipofika na kuuliza nini kilikuwa kimetokea mpaka Melania alie, wakajibiwa kwamba kulikuwa na dalili zote kwamba mgonjwa wao alikuwa amefariki ndani ya chumba alichokuwa amelazwa.
****
Ilikuwa ni vita ya kumgombea William, kila mmoja alijua kwamba endapo serikali ya Marekani ingekuwa na mtu kama William basi kungekuwa na mambo mengi ambayo yasingekwenda kama yalivyotakiwa kwenda kwani nchi hiyo ingekuwa juu kiteknolojia kitu ambacho kingeifanya dunia kuwa na hofu kubwa juu ya taifa hilo kubwa.
Mbali na Urusi ambayo kila siku walikuwa wakipambana kuhakikisha kwamba William anapatikana mikononi mwao pia kulikuwa na kundi jingine ambalo usiku na mchana lilikuwa likimuhitaji William, kundi hili lilikuwa ni Al Qaeda, kundi la kigaidi lililokuwa na makazi yao nchini Afghanistan katika Milima ya Tora Bora.
Kundi hilo lililokuwa likiongozwa na jamaa mwenye roho mbaya, Idriss Al Ghabush lilichanganyikiwa mara baada ya kusikia taarifa juu ya William ambaye alionekana kuwa mtu hatari katika masuala ya kompyuta.
Ilikuwa ni lazima kupambana na Marekani kwa kutumia kompyuta. Watu wengi wa kundi hilo waliuawa kwa sababu ya masuala ya kompyuta. Wengi walikuwa wakikamatwa kila walipokuwa wakizungumza kwa njia ya simu ambazo zilidukuliwa na wataalamu hao wa IT.
Marekani ilikuwa na wataalamu wengi wa kutumia kompyuta kitu kilichowapa ugumu kupambana nao. Mara baada ya kuona kwamba wanashindwa na taifa hilo kutokana na nguvu kubwa ya teknolojia, hapo ndipo walipoamua kumtafuta Muhindi aliyeitwa Cashmir Ajay ambaye alilifanya kundi hilo kuwa juu zaidi kiteknolojia kiasi kwamba Marekani ikaanza kupata kazi upya.
Baada ya kusumbuliwa sana, ndipo ujio wa William ukagundulika. Walijua kwamba huyo alikuwa mtu hatari kutokana na yale aliyokuwa akiyafanya hivyo kuwatuma watu nchini Marekani kwa ajili ya kumfuatilia mtu huyo.
“Ila kuna taarifa zinasema kwamba hata Warusi wanamfuatilia,” alisema jamaa mmoja.
“Umejuaje?”
“Kuna yule mpelelezi wetu kitengo cha KGB ndiye aliyenipa taarifa hizo.”
“Kwa hiyo nao wapo Marekani?”
“Ndiyo mkuu!”
“Hakikisheni mnakwenda huko! Chochote kitakachotokea, fanyani mnalolijua ili mambo yawe sawa,” alisema Ghabush.
Harakaharaka mawasiliano kati ya Waarabu waliokuwa Afghanistan na Marekani yakafanyika haraka sana. Vijana wengine watatu wakatumwa kuelekea huko kwa ajili ya kukamilisha kile kilichotakiwa kufanywa kipindi hicho.
Kuingia nchini Marekani hakukuwa na tatizo lolote lile, walijifanya kuwa wanachuo waliokuwa wakienda huko kusoma huku wengine wakijifanya kuwa wafanyabiashara wakubwa.
Hilo halikuwa tatizo, wakaruhusiwa kuingia ambapo moja kwa moja wakaonana na wenzao na kuwaambia kilichokuwa kikiendelea. Walichokifanya ni kufuatilia, walipofika chuoni wakagundua kwamba kulikuwa na Mrusi mmoja aliyekuwa karibu sana na William.
Wakaingiwa na shaka kwamba huyo Mrusi hakuwa mtu wa kawaida, alikuwa karibu na William kwa maslahi fulani, hivyo wakaanza kufuatilia kwa ukaribu. Siku ambayo Borya na William walikuwa wakienda kwenye sherehe ya kuzaliwa ya msichana Catherine, wakawatuma vijana wawili ambao walifika mpaka ukumbini na kutaka kuingia ndani lakini hawakuruhusiwa.
Hilo halikuwa tatizo, walijua fika kwamba huo wote ulikuwa ni mchezo uliopangwa, ili kuwadanganya, wakajifanya wakiondoka lakini wakaliegesha gari lao sehemu na kuteremka kisha kuanza kufuatilia.
Ilipofika usiku mkubwa, Warusi wanne wakatoka ndani ya ukumbu ule huku mmoja akiwa amembeba mtu begani, walikuwa na uhakika kwamba huyo alikuwa William, akapandishwa ndani ya gari na kuondoka mahali hapo.
“Tuwafuatilie,” alisema Mwarabu mmoja, huyo aliitwa Kadesh Saleh.
Wakaingia ndani ya gari na kuanza kuwafuatilia. Ilikuwa ni safari ndefu kidogo ambayo iliishia ndani ya jumba moja la kifahari lililokuwa likimilikiwa na Mrusi mmoja, mfanyabiashara mkubwa aliyeitwa Petrov Tasha.
Humo ndani, mara baada ya William kuingizwa, mtu aliyeonekana kuwa daktari akahitaji William apelekwe katika chumba maalumu kwa ajili ya kuvishwa sura ya bandia.
Hilo halikuwa tatizo, huku akiwa amepoteza fahamu, akapelekwa katika chumba hicho na kuwekwa juu ya meza kubwa. Hapo, ikachukuliwa sura ya bandia ya mtu aliyeonekana kuwa Mrusi kisha kuvarishwa, ngozi yake nyeusi ikaanza kupakwa vipodozi mbalimbali na kubadilika, akaonekana kama Mzungu.
“Ni lazima achomwe sindano yenye Mitrophynpil,” alisema daktari huyo.
“Haina shida! Dawa ziandaliwe!”
“Hiyo si dawa, ni sumu ambayo itavifanya viungo vyake vyote kutokufanya kazi kwa saa sabini na mbili,” alisema daktari huyo.
“Sawa. Ngoja itafutwe.”
Kulikuwa na ugumu mkubwa kuipata sumu ya Mitrophynpil lakini ndani ya saa moja, wakafanikiwa na hivyo kumpelekea daktari huyo ambaye bila hofu, akamchoma William sindano yenye sumu hiyo ambayo ingevifanya viungo vyake vyote kutulia, kutokufanya kazi kabisa zaidi ya kichwa.
“Sasa yupo huru kusafirishwa!”
Hicho ndicho kilichofanyika, siku iliyofuata, hata kabla suala la William halijaanza kuwa gumzo, wakafanya mipango ya kumsafirisha William kuelekea nchini Urusi, hawakupata tabu kupata tiketi, walipopewa na vibali vyote vya safari, wakaelekea uwanja wa ndege.
Wakawatafuta watu wengine watatu, hao walitakiwa kujifanya ndugu wa William na walikuwa wakimpeleka ndugu yao nchini Urusi kwa ajili ya matibabu. Ilikuwa vigumu kwa watu kugundua kwamba mtu huyo hakuwa yule waliyekuwa wakimwangalia.
Sura ilikuwa nyingine, aliyafumbua macho yake lakini alishindwa kuongea kitu chochote kile. Hakuonekana kuwa mtu mweusi, sura pamoja na vipodozi alivyokuwa amepakwa vilionyesha kabisa kwamba William alikuwa Mrusi.
We have to take him to Russia, he is going to die,” (tunatakiwa tumpeleke Urusi, anakufa) alisema mwanamke mmoja ambaye naye alikuwa Mrusi.
“Ooh! Very sorry! Can I see his ID, please” (Ooh! Poleni sana! Naweza kukiona kitambulisho chake, tafadhali?) alisema msichana aliyekuwa katika sehemu ya kukagua pasipoti na vibali vingine.
“This one madam,” (hii hapa mama)
Mwanamke yule akakichukua na kuanza kukiangalia, ni kweli alionekana kuwa Mrusi aliyeitwa Vladimir Kulich ambaye alionekana kuwa na siku chache za kuishi duniani kutokana na magonjwa mawili yaliyokuwa yakimsumbua, kupooza mwili na kansa ya damu. Baada ya kukiangalia kwa sekunde kadhaa, akawaruhusu wapite huku Wiliam akiwa amewekwa kwenye kiti cha matairi.
Alikuwa akiona kila kitu kilichokuwa kikiendelea, alitamani kuzungumza na kumwambia mwanamke yule kwamba hao hawakuwa ndugu zake lakini alishindwa kabisa kufanya hivyo.
Hakutingishika pale alipokuwa, bado sumu aliyokuwa amechomwa iliendelea kuvidhoofisha viungo vyake. Moyoni mwake aliumia mno, hakujiona kuwa tayari kuelekea nchini Urusi ila kwa sababu ya watu hao kumuhitaji, akajikuta akipelekwa huko pasipo kupenda.
Wakati wao wakipita na kuingia ndani, ya jengo la uwanja huo. Waliofuata walikuwa Waarabu wa kundi la Al Qaeda. Hao walitumwa kwa ajili ya kumsafirisha William kuelekea nchini Afghanistan.
Walifuatilia kwa karibu kila kitu kilichokuwa kimetokea, tangu usiku uliopita mpaka siku hiyo. Walijua kwamba kama ndege hiyo ingefika Urusi ingekuwa ngumu sana kwao kufanikiwa kumteka William hivyo waliona kulikuwa na umuhimu mkubwa wa kumalizia kila kitu ndani ya ndege.
Hakukuwa na mtu aliyejua kama asubuhi sana ya siku hiyo baada ya kugundua ndege aliyokuwa akisafirishiwa William, Waarabu hao walionana na wahusika kinyemela na kuwalipa dola laki moja kwa ajili ya kuweka mzigo wao wa silaha na mabomu ndani ya ndege hiyo.
Kilichobaki kilikuwa ni kuiteka ndege hiyo, kuwaua abiria wote na kumtorosha William.

Je, nini kitaendelea?
Je, Waarabu watafanikiwa kumteka William?
Je, Wamarekani watafanya nini wakisikia mtu wao ametekwa?
Je, WIlliam atafika Urusi?

No comments

Powered by Blogger.