FUTA MACHOZI MPENZI-13
NYEMO CHILONGANI
“Получили ли вы что-нибудь?” (umepata chochote?)
“Да сэр! Он здесь, имы должны сделать что,” (ndiyo mkuu! Yupo hapa na tunatakiwa tufanye jambo).
“Можем ли мы взять его?” (tunaweza kumpata?)
“Конечно,” (Bila shaka).
Hayo yalikuwa mawasiliano kwa njia ya simu baina ya Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi nchini Urusi, KGB (Komitet gosudarstvennoy bezopasnost), Petel Komukov aliyekuwa nchini Urusi na kijana wao waliyekuwa wamemtuma kwa kazi maalumu nchini Marekani, Samotic Kasemitov.
Shirika hilo la kijasusi lilikuwa limepata taarifa za ujio wa William ndani ya Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani. Sifa zake nyingi alizokuwa amemwagiwa kutokana na ujuzi wake mkubwa, akili aliyokuwa nayo kuhusu matumizi ya intaneti yaliwachanganya mno.
Walipanga kumchukua, kitendo cha nchini kama Marekani kuwa na mtu kama huyo tayari waliliona tatizo kubwa mbele yao. Walijua kwamba nchi kama Marekani ambayo walikuwa majirani zao na maadui zao wakubwa wangetumia kila hila kuhakikisha wanaingia katika kompyuta zao na kuangalia vitu vilivyokuwa vikiendelea humo.
Walikuwa na hofu, walimtaka William kwa nguvu zote, ilikuwa ni lazima kumteka kwani hakuwa Mmarekani, alikuwa Mtanzania ambaye nchi yake haikumjali na wala haikutaka kusikia chochote kuhusu mtu kama yeye, mwenye akili nyingi ambaye angeweza kufanya kitu chochote kwa usalama wa nchi.
Warusi hawakutaka kukubalia, walipewa taarifa za awali kwamba kijana huyo alikuwa ameingia ndani ya chuo hicho lakini pia aliwekewa ulinzi mkubwa ambao hakuujua kabisa. Aliishi kikawaida sana chuoni hapo huku akizoeana na watu wengi, kutokana na uchangamfu wake, kila mmoja alitaka kuwa rafiki yake.
Maofisa wa FBI ambao walitumwa kwa ajili ya kumlinda William walikuwa na hofu kubwa, kazi kubwa ilikuwa mbele yao, hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya kwani hawakutaka kumuona kijana huyo akizoeana na watu wengi lakini kwa hali iliyokuwa imetokea, hasa uchagamfu wake uliwafanya kuwa na wakati mgumu sana wa kumlinda.
Walichokifanya Warusi mara baada ya kugundua kwamba bado chuo hicho kilikuwa kikipokea wanachuo wapya kipindi hicho, wakamtuma kijana wao ambaye alitakiwa kujifanya kama anajiunga katika chuo hicho na kusoma huku akiweka ukaribu wake na William, mtu huyu aliitwa Borya Dima.
Kijana huyo akaingia chuoni hapo kama mtu aliyetaka kusomea mambo ya kompyuta, hakukuwa na ofisa yeyote wa FBI ambaye aligundua kwamba kijana huyo alikuwa ametumwa kutoka nchini Urusi.
Alikuwa mtaalamu wa kompyuta na katika wiki ya kwanza kufika chuoni hapo akaanza kuutafuta ukaribu na William. Haikuwa kazi kubwa kuupata ukaribu huo, William hakuwa mtu wa kunyamaza, kila mtu aliyesimama mbele yake, alizungumza naye.
Borya akawa na furaha, katika kila hatua aliyokuwa akipiga, usiku aliwapigia simu maofisa wa KGB na kuwaambia pale alipoishia. Safari yake ya kutaka kumteka William haikuonekana kuwa kubwa hata kidogo, kwake, ilionekana kama kumsukuma mlevi.
“Ninajua kompyuta zaidi yako,” alisema Borya huku akimwangalia William.
“Una uhakika?”
“Ndiyo! Unafahamu kitu gani ambacho mimi sikifahamu?” aliuliza Borya huku akimwangalia William, yote hayo ilikuwa ni kutafuta mazoea na kijana huyo.
“Nahisi vingi!”
“Kama?”
“Kujua huwa unawasiliana na nani nyakati za usiku,” alisema William huku akiachia tabasamu pana.
Borya akashtuka, kile kilichokuwa kikiendelea usiku alihisi kwamba William alikujua, kwanza akanyamaza, akaingia kwenye dimbwi la mawazo na kugundua kwamba kila kitu kilichokuwa kikiendelea kwenye simu usiku William alikuwa akifahamu.
Hakujua kama William alisema hivyo kama kumtisha, kumfanya amuone mtu hatari na hakuwa akifuatilia mawasiliano yake hata kidogo. Alipopewa jibu hilo, Borya akajibaraguza na kuelekea chumbani kwake, siku hiyo hakutaka kusubiri mpaka usiku, alichokifanya ni kuwapigia simu watu waliomtuma.
“Nahisi picha imeungua!” alisema Borya huku akionekana kuwa na hofu.
“Kwa nini?”
“Huyu jamaa anajua kwamba nawasiliana na nyie kila siku usiku,” alisema Borya.
“Amejuaje?”
“Ameniambia!”
“Una uhakika?”
“Siwezi kudanganya katika hili,” alisema Borya.
Wao wakampa mbinu mpya, hawakutaka kuendelea kuongea usiku kwa kuhofia kwamba William angeendelea kuyakamata mawasiliano yao kitu ambacho haikuwa kweli hata kidogo. Ubishi wake, ushindani wake na William ukamfanya kuwa karibu na kijana huyo.
Wakawa wawili, marafiki wakubwa, wakifanya mambo mengi pamoja na hata siku nyingine kutoka pamoja na kwenda klabu ambapo huko walikuwa wakicheza muziki na kufanya vitu vingi.
FBI hawakujua kama Borya alikuwa mtu aliyetumwa kutoka Urusi, walimwamini na kumuona mtu wa kawaida, mwanachuo ambaye alitamani sana kuwa na William. Siku zikakatika, kila walipokuwa wakienda klabu, Borya alikuwa akimtaka William anywe pombe lakini kijana huyo hakuwa akikubali.
“Borya! Huwa sinywi pombe,” alisema William.
“Najua lakini wakati mwingine jifunze. Mdogomdogo utaweza kuhimili,” alisema Borya huku akiachia tabasamu.
“Hapana!”
Urafiki ukaendelea, wakati wakiendelea kuwa pamoja, kukatokea msichana mmoja, mrembo, mrefu na mwenye mchanganyiko wa rangi, huyu aliitwa Linda. Alikuwa msichana mrembo ambaye naye alikuwa miongoni mwa wanawake waliotokea kupendwa chuoni hapo.
Japokuwa William alikuwa na sura mbaya lakini alitokea kupendwa mno na msichana huyo. Kila alipokuwa akimwangalia, moyo wake ulitamani sana kuwa naye. Alijitahidi sana kuwa karibu naye, mara kwa mara alikuwa akimpigia simu na kuzungumza.
Watu walimshangaa Linda, hawakuamini kama kungekuwa na msichana ambaye angetamani kujenga ukaribu na mwanaume huyo ambaye wengi waliupenda uwezo wake lakini si kumpenda yeye kwa jinsi sura yake ilivyokuwa mbaya.
Linda hakujali, moyo wake ulimwambia kwamba William ndiye alikuwa mwanaume pekee ambaye angeishi naye kipindi chote. Kila siku ilikuwa ni lazima kukutana na William na kumwambia ukweli kwamba alikuwa akimpenda, hakukuwa na mwanaume yeyote chini ya jua aliyekuwa akimpenda kama yeye.
Hilo likamfariji William lakini ugumu ulikuja kila alipomkumbuka msichana Melania, alikumbuka kwamba msichana huyo alimwambia kuwa anampenda na alitaka kuwa naye japokuwa yeye mwenyewe hakutaka kuwa naye kwa kuwa aliona kutokustahili kuwa na msichana mrembo kama alivyokuwa.
Kwa Linda, jinsi alivyomuona, aliona kwamba alistahili lakini kumkubalia lilikuwa jambo gumu sana. Alimwambia ukweli msichana huyo kwamba alimpenda lakini hakutaka kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi.
“Kwa nini?”
“Hakuna sababu! Ni maamuzi tu!” alijibu William.
“Ni maamuzi yanayoniumiza William! Naomba uwe wangu,” alisema msichana huyo, uzuri wa sura yake ulionekana kama kuwa kosa kubwa kwa William kumkatalia.
“Haiwezekani,” alisema William.
Alikataa katakata, si mara moja, mara nyingi alimkatalia msichana huyo. Hakutaka kuwa naye, kwake, alimchukulia kama rafiki wa kawaida tu. Ukaribu na msichana huyo ukaongezeka maradufu mpaka kufikia kipindi wakawa wanalala pamoja chumbani, japokuwa hawakuwa wakigusana lakini mwili wa William ulikuwa kwenye presha kubwa.
“Linda! Unafanya nini?” aliuliza William, wakati anauliza swali hilo, mkono wa msichana huyo ulikuwa kwenye mapaja yake ukifuata eneo la zipu.
“Nimeshindwa kuvumilia mpenzi,” alisema Linda kwa sauti nyororo, muda huo ulikuwa ni saa nane usiku.
“Linda...”
“Hapana William! Ninakupenda, ninakupenda mpenzi,” alisema Linda huku mkono ukizidi kupanda juu.
Katika maisha yake yote hakuwa kukutana kimwili na msichana yeyote yule. Mwili wake ulimsisimka mno, mguso aliopewa na msichana huyo ulimpagawisha. Alikataa na kukataa lakini mwisho wa siku akajikuta akijiweka vizuri na ndani ya dakika kumi tu kitanda kikaanza kulia kama mtu aliyekuwa akienda juu na chini.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa uhusiano wao wa kimapenzi. Moyo wa Linda ulifurahi, hakuamini kama kweli alifanikiwa kuwa na mwanaume huyo. Kila alipomuona, alimpenda maradufu na hata ubaya wa sura yake kwake haukuonekana.
William aliifurahia mapenzi, kila siku alipokuwa akizungumza na Borya, alimwambia ukweli juu ya maisha yake kwamba alimpenda msichana huyo kuliko kitu chochote kile katika maisha yake. Uhusiano huo ukaibua gumzo kubwa chuoni hapo, hakukuwa na aliyeamini kwamba Linda angekuwa mwepesi sana kwa William.
Wakati yote yakiendelea, maofisa wa FBI waliendelea kumlinda William, walikuwa tayari kila wakati, walijitahidi kuhakikisha kwamba mtu huyo hatekwi wala hafanyiwi jambo lolote baya, walipoona kwamba wao kama wao hawakuweza zaidi, wakaamua kuwaweka wanachuo wengine, walijifanya kama wasomi lakini kila siku walikuwa wakifuatilia kilichokuwa kikiendelea.
“Borya! Kuna kitu nataka nifanye!” alisema William.
“Kitu gani?”
“Nataka niandae mtandao wa kijamii! Ufanane na Facebook, watu wawasiliane, watumiane picha na mambo mengine,” alisema William.
“Unahisi utapata mashabiki wengi?”
“Ndiyo! Kitu cha kwanza kabisa nitakachokifanya ni kuudhoofisha Mtandao wa Facebook,” alisema William huku akimwangalia Borya usoni.
“Kivipi?”
“Utaona! Kwanza ngoja niutengeneze mtandao wenyewe,” alisema William.
Hicho ndicho alichotaka kukifanya. Siku iliyofuata akamuita mpenzi wake, Linda na kumwambia wazo hilo alilokuwa nalo. Hilo halikuwa tatizo, Linda alimuunga mkono kwa kila kitu hivyo baada ya wiki moja akaanza kufanya kazi aliyotaka kuifanya.
Akajifungia chumbani, hakutaka kutoka ndani, alikuwa peke yake huku akiwa bize. Hakuingia darasani, alitaka kubaki ndani, peke yake huku akiendelea kufanya kazi hiyo aliyokuwa akiifanya.
Alitumia kipindi cha wiki moja kutengeneza muonekano wake na baadaye kuingizia vitu muhimu, kama sehemu za meseji, ukuta wa mwenye akaunti na vitu vingi na mwisho wa siku kuupa mtandao huo jina la MeChat.
“Nimemaliza,” alisema William huku akimwangalia Linda.
“Kweli?”
Ndiyo! Utazame,” alisema William, hakutaka kumpa mtu yeyote taarifa zaidi ya msichana huyo tu.
Linda akautazama, aliangalia kila kitu kilichokuwa humo. Moyo wake ukaridhika, ulikuwa mtandao wenye muonekano mzuri ambao alihakikisha anaingiza vitu vingi ambavyo vijana walikuwa wakivitaka.
Kabla hajauruhusu ufanye kazi aliamini kwamba ungekuwa na nguvu, Linda kamshauri kuongeza baadhi ya vitu na yeye kufanya hivyo. Alifanikiwa kwa asilimia mia moja na hivyo kumpigia simu rafiki yake mkubwa, Borya kwa ajili ya kuuona.
“Ninakuja!” alisema Borya kwenye simu.
Wakati hayo yakiendelea, macho ya Linda yalikuwa usoni mwa William, kila alipomwangalia, alimpenda, alihisi mapenzi mazito moyoni mwake. William akashindwa kuvumilia, akaamini kwamba kulikuwa na kitu mpaka msichana huyo kumwangalia namna hiyo.
“Kuna nini?” aliuliza William.
“Umegundua nini?” aliuliza Linda huku akiligusa tumbo lake.
“Unanitania...unanitania Linda...” alisema William huku akionekana kuwa na furaha tele.
“Nina mimba yako! Ina wiki mbili sasa,” alisema Linda huku akionekana kuwa na furaha mno. William akapiga magoti kisha kulibusu tumbo la mpenzi wake, akatarajiwa kuitwa baba! Muda wote huo, macho yake yalilowanishwa na machozi ya furaha yaliyoanza kumtiririka mashavuni mwake.
Je, nini kitaendelea?
Je, Warusi watafanikiwa kumteka William?
Je, nini kitatokea endapo watafanikiwa?
Je, vipi kuhusu Melania?
Tukutane hapahapa.
Post a Comment