Serikali yatangaza ‘Diploma’ ndiyo kigezo cha chini cha elimu kwa waandishi wa habari
Serikali
imetangaza kuwa kiwango cha chini cha taaluma anayopaswa kuwa nayo
mwandishi wa habri kuwa ni 'Diploma ya Uandishi wa Habari' kwa mujibu wa
kanuni za sheria mpya ya hunda za habari zilizokamilika utungaji wake
hivi karibuni.
Akizungumza
na wana habari leo mjini Dodoma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo , Nape Nnauye amesema kuwa kanuni zimeshaundwa na zimechapishwa
kwenye gazeti la serikali tangu Februari 3 mwaka huu baada ya kupokea
maoni ya wadau mbalimbali.
"Tumesoma,
tumechambua maoni ya wengi, wapo waliotaka iwe cheti, wengine diploma,
wengine digrii, wapo waliotaka PhD na wapo waliotaka iwe mtu yeyote
nayejua tu kusoma na kuandika. Serikali imesimama katikati ya maoni
hayo. Sifa ya chini kabisa kwa kuanzia itakuwa ni diploma ya uandishi wa
habari” Amesema Nape
Waziri
Nape amesema pia kuwa sheria hiyo imeshaanza kutumika tangu Desemba 31
mwaka 2016, ambapo yeye kama Waziri mwenye dhamana alishatoa tangazo
katika gazeti la serikali.
Aidha
kuhusu wasio na sifa hiyo, Waziri Nape amesema kuwa serikali imetoa
kipindi cha mpito cha miaka mitano ili waandishi wasiokuwa na sifa hiyo,
waliopo sasa na watakaoingia kwenye taaluma hiyo, wakasome ili wawe
wamepata sifa hiyo.
Amesema
katika utekelezaji wa sheria hiyo, kuna taasisi ambazo tayari zipo,
zitaongezewa majukumu au kazi zake kuhuishwa, pia kuna vyombo vipya
vitaanzishwa na kuna taratibu mpya za kiutendaji zitaandaliwa.
Kuhusu
manufaa ya sheria hiyo, Nape amesema kuanza kutumika kwa sheria hiyo ni
jambo muhimu kwa tasnia hiyo kwa kuwa ni ruhusa ya kuanza kwa mchakato
wa kuifanya taaluma ya habari kuwa taaluma kamili yenye sifa mahsusi na
maadili yaliyokamilika pamoja na kuwa na vyombo vya kusaidia
utekelezaji wake.
Sheria
hiyo ilisainiwa na Rais Magufuli Novemba 16 mwaka 2016, na siku mbili
baadaye ilichapishwa kwenye gazeti la serikali baada ya muswada wake
kupitishwa na Mkutano wa 5 wa bunge mwezi Novemba 2016.
Post a Comment