ad

ad

FUTA MACHOZI MPENZI - 12

 
NYEMO CHILONGANI
William aliona kazi kubwa mbele yake, aliambiwa kwamba ilikuwa ni lazima aelekee nchini Marekani kwa ajili ya kuonyesha ugenius wake lakini alitaka kuwaonyeshea huku akiwa nyumbani amekaa.
Ilikuwa ni lazima azime huduma ya intaneti iliyokuwa ikipatikana chuoni hapo. Ilikuwa kazi kubwa kuzitafuta kompyuta za chuo hicho, jasho lilimtoka, siku hiyo hakutaka kufanya kitu chochote kile zaidi ya kuchezea kompyuta na kuzitafuta kompyuta za chuo hicho.
Chuo hicho kilikuwa vigumu kupatikana, alipambana lakini matokeo yake alikuwa akipata kompyuta za vyuo vingine ambavyo wala hakuwa akivitaka, yeye alikitaka Chuo Kikuu cha Harvard kilichokuwa nchini Marekani.
Usiku mzima alikesha akipekua huku na kule, alihangaika mno, alishindwa kuzipata kompyuta za chuo hicho hivyo alichokifanya ni kutafuta kompyuta za Chuo Kikuu cha Oxford cha nchini Uingereza kwa kuamini kwamba kulikuwa na mawasiliano baina ya vyuo hivyo viwili kwani vyote vilikuwa vikubwa duniani.
Akazipata kompyuta za chuo cha Oxford, kwa sababu walikuwa na barua pepe yake, akaanza kuingiza codes kwa ajili ya kuihack barua pepe ya kompyuta hizo. Hilo wala halikuwa tatizo, alifanikiwa kwa asilimia mia moja, akaingia kwenye barua pepe hizo, akaanza kuangalia zile barua pepe zilizotumwa kwenda kwenye chuo hicho na ndipo akafanikiwa kuona barua zote ambazo zilitumwa, alichokifanya ni kuchukua ‘links’ za zile barua na kuziingiza kwenye codes zake na kuanza kuhack upya.
Codes zikaanza kusoma taratibu huku zikifungua mafaili, ilikuwa kazi kubwa kwani kulikuwa na mafaili makubwa ambayo mengine yalichukua mpaka GB 100 na hivyo codes hizo kwenda taratibu sana.
Alisubiri kwa saa mbili, zikamaliza na hatimaye akafanikiwa kuziona kompyuta za chuo hizo ambazo zilikuwa zikitumia intaneti chuoni humo, alichokifanya ni kuiba IP Adress zote zilizokuwa zikiunganishwa na modem kubwa iliyokuwemo humo chuoni na kisha kuanza kuzichanganya kwenye codes zake, zilipomalizika, yeye ndiye alikuwa na uwezo wa kuzima na kuwasha intaneti ya chuo hicho.
“Hatimaye nimeweza,” alisema William huku akishusha pumzi.
Kabla ya kuendelea, akaingiza virusi vipya alivyovitengeneza vya Winirus kisha kuficha codes na IP Adress za huduma ya intaneti katika chuo hicho na kuweka zake kisha kuizima huduma hiyo.
Hilo ndilo alilotaka kuliona, moyo wake ukafurahi, akafarijika kwa kuona kwamba alifanikiwa kile alichokuwa amekitaka kwa kipindi kirefu. Hakuhuzunika wanachuo kukosa huduma ya intaneti bali alichokuwa amekifurahia ni kwamba alitaka kuwaonyesha kwamba yeye ni genius kwa kutumia vitendo.
Siku hiyo ilikatika, kazi yake ilikuwa ni kufuatilia kwenye kompyuta yake kuona kama walikuwa wamefanikiwa au la. Siku ya kwanza ikapita, hakukuwa na mafanikio yoyote yale, siku ya pili ikapita na kuingia ya tatu bado hakuona kama walikuwa wamefanikiwa.
Taarifa za kuzima kwa intaneti chuo hapo ikaanza kutangazwa katika vyombo vya habari hasa CNN na BBC. Wataalamu walikuwa wakihangaika kuhakikisha kwamba intaneti inapatikana chuoni hapo lakini hawakufanikiwa kabisa.
Alikenua, aliona kwamba aliweza kuwakomoa kwa kile walichokuwa wamemjibu kwani aliona lilikuwa suala la kukubaliwa kujiunga na si mpaka kuitwa ili aonekane kama kweli alikuwa na genius.
Siku ya nne ilipoingia, saa nne usiku ndipo akaona codes zake zikianza kuvurugwa na IP Adress alizokuwa ameziweka zikianza kufutwa moja baada ya nyingine. Alishtuka, hakuamini kama kungekuwa na mtu aliyekuwa na uwezo wa kushindana naye.
Hakutaka kuchelewa, hapohapo akaivuta laptop yake na kuanza kuichezea. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kutaka kujua kompyuta ambayo ilikuwa ikitumika kwa ajili ya kuingiza IP Adress mpya, hilo halikuwa tatizo, alifanikiwa na mwisho wa siku kompyuta hiyo kuonekana.
“Kumbe ni hii! Subiri,” alisema na kisha kuvituma virusi vya Winirus katika kompyuta hiyo huku akiambatanisha na vitu viwili, picha na ujumbe kwa mtu mwenye kompyuta hiyo.
Akatoa zile codes mpya zilizokuwa zimewekwa na kuweka zake yeye na kuruhusu ujumbe na picha ile uonekane, ujumbe mfupi uliosomeka ‘I GET YOU BACK TTO WORK’ (NAKURUDISHA TENA KAZINI)
***
Profesa Mcleash hakuamini alichokuwa akikiangalia, picha ya kijana yule iliyotokea kwenye kompyuta ya Vint aliifahamu sana, aliiona wakati alipotumiwa barua pepe ya kuomba kujiunga na chuo hicho, ilikuwa picha ya William, sura mbaya ambayo hakuwahi kuiona kabla.
“Who is this ghost?” (huu ni mzimu gani?) aliuliza Profesa Turnbull huku akimwangalia Macleash.
Profesa huyo ndipo akaanza kuwaambia kuhusu Wiliam kwamba ndiye alikuwa yule kijana aliyeomba kujiunga na chuo chao lakini maprofesa hao walimuwekea ngumu. Walishangaa, hawakuamini kwamba mambo hayo yote ya kukatika kwa intaneti yalifanywa na kijana huyo, tena kilichowachanganya zaidi ni kwamba alikuwa nchini Tanzania.
Waliangalia picha ya kijana huyo, alikuwa mbaya wa sura, alitisha lakini ndiye alikuwa genius wa kufanya mambo hayo yote. Vint akawaangalia maprofesa hao huku akiwashangaa, hakukuwa na profesa yeyote duniani ambaye hakutaka kuonana na mtu mwenye kipaji, sasa ilikuwaje mpaka wakatae kuonana na kijana huyo ambaye alimtoa jasho na hata intaneti ilipokatika tena, hakujua angeirudisha vipi?
“Huyu yupo wapi?” aliuliza Vint, hakuamini kama mtu huyo ndiye aliyemtoa jasho namna hiyo.
“Yupo Afrika, nchi moja inaitwa Tanzania!” alijibu Macleash.
“Ninahitaji nimuone, ninahitaji nifanye naye kazi,” alisema Vint.
“Hapana! Anakuja kujiunga na chuo hiki! Utamchukua atakapomaliza masomo ya chuoni hapa,” alisema Turnbull, yeye ndiye aliyemkataa William siku chache zilizopita lakini leo, alitaka kumng’ang’ania asome chuo hicho kwa kuamini kwamba chuo chao kingetengazika sana kupitia yeye.
“Nishawasiliana naye na kumtumia tiketi!”
“Naomba ufuatilie, hata kesho au keshokutwa awe amekwishafika,” alisema Turnbull.
****
Moyo wa William ulikuwa na furaha kubwa, hakuamini kama alikuwa amefanikiwa kufanya kile alichokifanya. Kila alipokaa, alihisi kurukaruka kwa furaha, alidharaulika kwa kuonekana kwamba hakuwa na kipaji lakini baada ya kuwadhihirishia kwa matendo, kila mmoja akakubali kwamba alikuwa na kipaji kikubwa na hivyo kumtaka aende akasome katika chuo hicho.
Akamwambia mama yake, mara ya kwanza alitaka kuhack akaunti zao benki ili ikiwezekana aonekane amefanya malipo ya ada, ilikuwa kazi nyepesi lakini kabla ya kufanya kitu hicho, akahitajika huko chuoni kuanza masomo.
Akamwambia mama yake, Bi Sophia kwamba alitakiwa kusafiri kwenda nchini Marekani kusoma, alipoulizwa, alimjibu kwamba hakutakiwa kulipia ada kwani kwa kile alichokuwa amewafanyia, wote walitamani kumuona akiwa pamoja naye chuoni hapo.
“Hongera sana! Kwa hiyo unaondoka lini?” aliuliza mama yake.
“Kesho! Imekuwa ghafla sana mama!”
“Sawa. Tutamuomba Mungu aweze kukupigania katika safari yako yote,” alisema mama yake huku akionekana kuwa na furaha tele.
Hakutaka kuishia hapo, mtu mwingine ambaye kwake alionekana kuwa muhimu alikuwa msichana Melania, akampigia simu na kumwambia kilichokuuwa kimetokea, msichana huyo hakutaka kukubali, akamwambia kwamba alitaka kuonana naye na kuzungumza naye zaidi.
Baada ya saa mbili, wakaonana katika mgahawa mmoja uliokuwa Kinondoni. Kila mtu aliyekuwa ndani ya mgahawa huo alibaki akimwangalia William, ubaya wa sura yake uliwashangaza wote, hawakuwahi kumuona na wala hawakujua alikuwa akijishughulisha na vitu gani.
Alikuwa na sura mbaya lakini aliteremka kutoka kwenye gari la thamani kubwa na alikaa kiti kimoja na msichana mrembo ambaye alijulikana sehemu kubwa jijini Dar, huyu alikuwa Meliania ambaye muda wote alionekana kuwa na furaha, kukutana tena na William kwake ilikuwa shangwe.
“Mbona ghafla sana?” aliuliza Melania.
“Yeah! Kuna mambo yalitokea, ilibidi niondoke mapema sana,” alisema William.
Walikaa na kuzungumza mambo mengi, japokuwa siku za kwanza Melania alimuona William kuwa na sura mbaya lakini kutokana na ukaribu wao mkubwa, akajikuta akianza kumuona mtu wa kawaida na mbaya zaidi chembechembe za mapenzi juu ya mwanaume huyo zilichipukia lakini hakuonekana kukubaliana naye, hakutaka kuwa naye kabisa.
Siku hiyo, Melania hakutaka kunyamaza, kama alivyomwambia kipindi cha nyuma, akamwambia tena na tena kwamba alikuwa akimpenda lakini mwanaume huyo hakuwa na habari, alimwambia wazi msichana huyo kwamba lingekuwa jambo jema kama wangekuwa marafiki na si wapenzi kama alivyotaka iwe.
Moyo wake ulimuuma, hakuamini kama na uzuri wake wote huo mvulana huyo angekataa kuwa naye na wakati kulikuwa na wanaume wengi waliomsimamisha na kumwambia kwamba walikuwa wakimpenda.
Baada ya kuzungumza kwa saa moja, wakaagana kwa kukumbatiana na kuondoka mahali hapo ambapo siku iliyofuata William akapanda ndege na kuanza kuelekea nchini Marekani huku akiwa na furaha tele.
Ndani ya ndege kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, alikuwa akiyafikiria maisha yake mapya ambayo alikuwa akienda kuyaanza nchini Marekani, alikuwa na furaha tele na muda wote alikuwa akitoa tabasamu pana.
Ndani ya ndege ile kila mtu aliyekuwa akimwangalia alishtuka, ni kweli walikuwa wamewaona watu wengi waliokuwa na sura mbaya lakini kwa William ilikuwa ni zaidi ya mbaya.
Alitisha, watoto waliomuona walihisi kwamba walikuwa wakikiangalia kinyago na hivyo kuanza kulia. Hakuumia moyoni mwake, aliyazoea maisha hayo kwani hayakuanza ghafla, yalikuwa maisha aliyozoea kuishi tangu alipokuwa mdogo.
Mbali na kuyawaza maisha anayokwenda kuyaanza Marekani lakini hakuacha kumfikiria msichana Melania. Alikuwa msichana mrembo mno, alitamani kuwa naye kimapenzi lakini hakuona kama moyo wake ulikuwa tayari kuwa na msichana huyo.
Kila wakati alipokuwa akimfikiria, tabasamu pana lilikuwa likionekana usoni mwake. Alijiona kunyimwa kila kitu lakini alimshukuru Mungu kwa kuwa akili nyingi alizokuwa nazo ndizo zilizokuwa zikiyabadilisha maisha yake kila siku.
Ndege ikachukua saa ishirini na mbili, ikatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK uliokuwa jijini New York ambapo baada ya kupumzika kwa saa moja, wakaunganisha safari ya kuelekea Massachuesetts hapohapo nchini Marekani.
Walipoingia ndani ya ndege hiyo na kuanza safari hiyo, moyo wake ulikuwa na furaha tele, hakuamini kama kweli alikuwa ameingia nchini Marekani ambapo kila siku alikuwa akipaota tu.
Ndege ilichukua saa moja, ikaanza kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Boston Logan ambapo baada ya abiria kuteremka, naye akateremka mpaka sehemu ya kuchunguzia mizigo, alipoonekana hana tatizo, akaelekea nje ambapo akakutana na mwanaume mmoja aliyeshika ubao ulioandikwa jina lake huku pembeni akiwa na wanachuo wanne.
“There he is,” (yule pale) alisema mwanaume huyo na kuanza kumfuata.
Hakuwapotea, hakukuwa na mtu aliyejiuliza kama ndiye yeye au la, sura yake tu kwa jinsi ilivyokuwa mbaya kila mmoja aligundua kwamba ni yeye. Walikuwa wakimshangaa lakini pia walikuwa wakifurahi kuwa na mtu kama huyo.
Wakaanza kuzungumza naye hata kabla ya kuingia ndani ya gari, kila mmoja alifurahi kukutana naye. Watu wengine walikuwa wakimshangaa tu William, wengi walihisi kwamba alipata ajali na uso wake kupasuliwa kwa jinsi alivyokuwa na sura mbaya.
Akachukuliwa na kuingizwa ndani ya basi moja kubwa lililoandikwa Harvard University ubavuni na kuanza kuelekea chuoni. Alipofika huko, kila mwanafunzi alikuwa akimwangalia kwa mshangao, walisikia habari zake kwamba ndiye aliyezima intaneti ya chuo hicho na mpaka muda huo haikuwa imerudi alipoizima kwa mara ya pili.
Kila mmoja alimuona kuwa mtu mwenye uwezo wa ajabu sana. Akachukuliwa na kupelekwa katika ofisi ya profesa Turnbul, alipofika huko, akakaribishwa na kupewa jukumu la kuirudisha huduma ya intaneti chuoni hapo, kazi ambayo aliifanya kwa dakika tano tu, intaneti ikawa imerudi.
Hapo ndipo alipotakiwa kuishi, hakutakiwa kwenda sehemu yoyote ile, maprofesa walijua kwamba William alikuwa na uwezo mkubwa hivyo kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwasiliana na ikulu ya Marekani na kuwaambia kuhusu mtu huyo.
Kitu kilichofanya ikulu hiyo ni kuwataka maafisa wa FBI (Federal Bureau of Investigation) wamlinde William kisiri ili asitokee mtu yeyote yule akamchukua mtu huyo ambaye waliamini kwamba angeweza kuwa muhimu kwa nchi yao hasa katika kipindi hicho ambacho teknolojia ilikuwa juu, walihitaji kupambana na maadui zao kama Urusi, China kwa kutumia teknolojia tu. Hivyo mtu huyo alitakiwa kulindwa sana.
Je, nini kitaendelea?
Je, FBI wataweza kumlinda William siku zote?
Je, William ataweza kuwa na Melania?
Nini kitatokea katika maisha ya William?
Nani aliambiwa afute machozi yake?
Tukutane Ijumaa hapahapa.

Ukishare, nitafutahi zaidi.

No comments

Powered by Blogger.