Wizara zote zatakiwa Kuhamia Dodoma kabla ya Feb. 28

Serikali
imezipa msisitizo wizara mbalimbali kuhakikisha zinahamishia makazi
yake Makao Makuu ya nchi mkoani Dodoma kabla ya Februari 28, mwaka huu,
kama ilivyotangazwa na Rais John Magufuli mwaka jana.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema agizo la
serikali lazima liwe limetekelezwa ifikapo Februari 28, mwaka huu.
“Kama
agizo lilivyotolewa na Rais Magufuli kuhusu wizara na watumishi wake
kuhamia Makao Makuu Dodoma, ndivyo wanavyotakiwa manaibu makatibu wakuu,
makatibu, manaibu mawaziri na mawaziri kutakiwa kuwapo Dodoma mwishoni
mwa Februari,” alisema Mhagama.
Waziri
Mhagama alisema ofisi yake imeweza kukagua miundombinu na ujenzi wa
majengo mbalimbali ya serikali yanayoendelea kujengwa na mengine yakiwa
yamekamilika kwa ajili ya matumizi ya wizara hizo.
“Hakuna
tatizo la ofisi za watumishi wa wizara zote, kwani majengo yamekamilika
na yapo katika hali nzuri tayari kwa ajili ya kuanza kutumiwa, hivyo
wakuu husika wakiwamo mawaziri wahakikishe wanatakiwa kuhamia Dodoma,”
alisema.
Post a Comment