KIFO CHA MTU ASIYE NA HATIA - 01 (HADITHI MPYA HII)
Nimeamua kuitunga simulizi hii mpya ili kuwaonyesha jinsi maisha yanavyoweza kuwa magumu lakini bado binadamu akafanikiwa! Na pia jinsi binadamu anavyoweza kumpenda binadamu mwenzake na hata kutoa vyote alivyonavyo kwa ajili yake!
Nina hakika hii ni simulizi nzuri na ya kuvutia pengine kuliko simulizi zote zilizotangulia, haina uhusiano na mtu yeyote na bado nasisitiza kuwa ni ya kubuni na nimeitunga mwenyewe haijatafsiriwa kutoka mahala popote kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakisema, ila kama kuna mtu ana ushahidi wa kuniaibisha basi aulete au atumie chombo kingine chochote cha habari kuthibitisha madai yake.
Simulizi hii naitoa maalum kama zawadi kwa dada yangu Upendo John mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Jangwani anayeteseka kwa uvimbe mgongoni uliomfanya apooze na kushindwa kuendelea na masomo yake! MUNGU AKUBARIKI UPENDO NA NINASEMA WAZI KUWA NINAKUPENDA SANA NA KWA MOYO WANGU WOTE.
Sehemu ya mwisho ya simulizi ya ‘SEE YOU IN HEAVEN DAD! (tutaonana mbinguni baba) itamalizika wiki ijayo! Samahani kwa usumbufu.
Eric J. Shigongo.
ILIKUWA ni siku ya Desemba 23, tena siku mbili tu kabla ya Christmas, dunia nzima ilijawa na shamrashamra za Sikukuu hiyo ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, maduka mengi jijini Dar yalijaa watu wakinunua nguo na vitu mbalimbali kwa ajili ya sikukuu.
Magari mengi yalisongamana barabarani na kufanya usafiri wa magari kuwa mgumu, sehemu ya kuendesha kwa dakika moja yalikwenda kwa dakika thelathini! Madereva wengi waliyaacha magari yao na kutembea kwa miguu.
“Mary’s boy child Jesus Christ was born on Christmas day, up now here the Angel sing the king was born to day, a man will live forever more because of Christmas day!....” Nyimbo za Chrismas zilitawala kila kona ya jiji la Dar es Salaam.
Siku hiyo Belinda alikuwa ndani ya daladala la kuelekea Segerea akiwa na mtoto wake wa miaka mitano, Alicia! Alikuwa mtoto mzuri mno na mwenye sura ya kumvutia kila aliyemwangalia, wengi walisema alichukua sura ya baba yake! Kila mtu ndani ya basi hilo alitamani kumbeba Alicia lakini Alicia mwenyewe alikataa na kubaki mikononi mwa Belinda mama yake.
Pamoja na uzuri wote huo wa mtoto Alicia alikuwa na kasoro katika mwili wake, hakupitisha hata wiki mbili bila kuugua! Homa na kikohozi hazikumpa nafasi katika maisha yake, Belinda alishatafuta tiba sehemu mbalimbali lakini hakufanikiwa kupata tiba kamili ya mtoto wake.
“Mom what are we going to do for Christmas? Are you going to buy me new clothes? My friends are going shopping with their parents? Mom are you going to take me shopping too? (Mama sisi tutafanya nini Christmas? Je, utaninunulia nguo mpya? Rafiki zangu wanakwenda madukani kununua nguo mpya na wazazi wao, utanipeleka na mimi kununua nguo?) Alicia alimuuliza mama yake huku akimpigapiga mgongoni.
Belinda alijifanya kutosikia maswali ya mwanae hii ni kwa sababu hakuwa na pesa wala jibu la kumpa mtoto wake ambaye kwa umri wake alikuwa hajaambiwa na mtu yeyote juu ya kilichoendelea katika maisha yao! Kwake kila kitu kilikuwa sawa.
“Mummy! Please answer my question!” (mama tafadhali jibu swali langu!)
“What have you said my dear daughter, I didn’t hear you! (Umesemaje kweli binti yangu mpendwa? Sikukusikia).
“Are you going to buy me new clothes this Christmas?” (utaninunulia nguo mpya Chrismas hii?”) Alicia aliuliza tena lakini bado mama yake aliendelea kukaa kimya, ni kweli hakuwa na jibu la swali hilo, hakuwa na pesa za kumnunulia mtoto wake nguo mpya! Si nguo tu bali hata pesa ya chakula cha siku ya Christmas hakuwa nayo!
Siku hiyo asubuhi walikuwa ndani ya daladala wakielekea kwenye gereza la Segerea kupitia Tabata, ilikuwa ni siku ya mwisho kwenda kuonana na mumewe Prosper aliyekuwa amekaa gerezani kwa muda wa miaka minane baada ya kuhukumiwa kifo kwa kosa la kumuua baba yake mzazi kwa kumpiga na mchi usoni.
Kwa kutumia mawakili Belinda alijitahidi kwa kila alichokuwa nacho kuhakikisha mume wake anatoka gerezani au kufungwa kifungo cha maisha lakini haikuwezekana, Prosper alikaa gerezani muda wote wa miaka minane akisubiri siku ya kunyongwa.
Ni siku iliyofuata ndiyo Prosper alitegemea kufa kwa kupigwa sindano ya sumu aina ya Digoxmait ili kumwondoa kabisa duniani, Prosper hakuwahi kuua kabla lakini kwa kosa hilo moja alihukumiwa kifo! Ni siku hiyo ya Desemba 23 ndiyo Belinda alitegemea kupewa nafasi ya mwisho kuongea na mumewe kabla ya kifo chake! Ilikuwa ni siku ya huzuni kubwa mno katika maisha yake na kila alipomfikiria mume wake roho ilimuuma sana na kufanya aanze kulia!
Hakuna mtu aliyewahi kumwambia Alicia kuwa baba yake asingerudi tena nyumbani na angenyongwa na kufa! Kila siku walipomtembelea gerezani, ili kumuondolea huzuni Alicia aliyeonekana kumpenda mno baba yake, Prosper alimwambia mwanaye Alicia kuwa angetoka gerezani siku si nyingi, jibu hilo ndilo mtoto aliliweka kichwani, hakuwahi kufahamu kabisa kuwa baba yake tayari alishahukumiwa kifo na alikuwa akisubiri siku yake.
“Mum! Mummy! Dad told me he is going to be with us during Christmas dont you remember? (Mama! Mama! Baba aliniambia atakuja nyumbani Christmas hii? Haukumbuki?) alipaza sauti Alicia mpaka watu ndani ya gari wakageuza shingo zao kumwangalia.
Belinda alishindwa kumjibu kitu chochote badala yake machozi yalianza kumtoka! Maneno ya mwanae yalimuumiza sana moyo alielewa wazi mtoto wake alikuwa haelewi chochote na asingeweza kumwambia ukweli kuwa baba yake alikuwa anakufa siku iliyofuata na walikuwa safarini kwenda gerezani kuagana naye kwa mara ya mwisho! Belinda aliendelea kulia kichinichini.
“Haya Segerea gerezani hapa, wa kushuka sogeeni mlangoni upesi msilete urembo wenu hapa” Alisema kondakta wa daladala na Belinda alisimama na kumshika Alicia mkono wakaanza kusogea mlangoni.
“Shusha hapo gerezani!” kondakta alipiga kelele na dereva akakanyaga breki na Belinda na mtoto wake wakateremka na kuanza kutembea kuelekea gereza la Segerea lililokuwa umbali wa kama mita mia tatu kutoka kituo cha basi.
Walipofika gerezani walionyeshwa chumba maalumu kilichoandaliwa kwa ajili yao kuongea na Prosper, Belinda aliketi chumbani humo akiwa amembeba mtoto wake miguuni, muda wote machozi yaliendelea kumbubujika na kufanya azilowanishe nguo zake.
“Mom stop crying, what are we doing here? Let’s go and see dady!”(Mama acha kulia, tunafanya nini hapa twende tukamwone baba!) Alicia aliendelea kumwambia mama yake.
Kabla Belinda hajatoa neno lolote mara mlango uliokuwa pembeni yao ulifunguliwa akajitokeza askari jela mmoja akiwa na bunduki mkononi mwake na baadaye aliingia mtu akiwa amevaa nguo nyeupe juu hadi chini na akiwa amefungwa kitambaa cheusi usoni, Belinda alipomwangalia mtu huyo alimtambua alikuwa ni mume wake Prosper. Alinyanyuka kitini na kuanza kumfuata.
“We mama hebu kaa chini usubiri utaratibu wa gereza kwanza, usituletee mambo ya uraiani, hapa ni gerezani kuna sheria zake vinginevyo na wewe utajikuta unanyea ndoo!” Askari alimfokea Belinda.
Bila ubishi Belinda alirudi kinyumenyume na kuketi kitini kwake akatulia akisubiri taratibu zote za gereza zimalizike. Prosper alikalishwa chini na kufunguliwa kitambaa usoni, alipowaona mke wake na mwanae alitokwa na machozi, huruma ilimshika kwani alijua kuwa hiyo ndiyo ilikuwa siku yake ya mwisho kuonana na familia yake.
“Mama una saa moja tu na nusu ya kuongea sisi tunaondoka tukirudi tutamchukua mumewe, utumieni vizuri muda mliopewa na mpange mambo vizuri! Hii ni nafasi ya mwisho kuonana na mumeo duniani!” Alisema askari mmoja na baadaye kutoka nje na kufunga mlango nyuma yake.
“Belinda umekuja mama mtoto wangu?”
“Ndiyo Prosper!”
“Hebu kabla ya yote na tupige magoti tumwombe Mungu kwani hii ni siku yetu ya mwisho katika dunia hii kuwa pamoja!” Prosper alimwambia mkewe na wote watatu walipiga magoti chini, Prosper akiwa na pingu zake mikononi na miguuni.
“Father in the name of Jesus and the mighty power of holly spirit, I thank you for every thing that happened in my life! Father you know how innocent I’m in this case, you know I didn’t kill anybody! But the entire world knows I’m a killer, tomorrow I’m dying leaving my wonderful wife and daughter behind me, protect them Lord, make me meet them in heaven! Father you know how much I Love my wife and how much I love my daughter Alicia too. It haunts me badly inside to learn that this is my last moment with them! I’m dying and leaving my Alicia and Belinda alone, but I know with you they will never be alone..... (Baba katika jina la Yesu na uwezo wa Roho Mtakatifu ninakushukuru kwa kila kitu kilichotokea katika maisha yangu, baba ninajua ni kiasi gani unaelewa sina hatia katika suala hili, unajua wazi sikuua lakini dunia nzima inanijua mimi ni muuaji. Kesho ninakufa nakuwaacha mke wangu mzuri na mwanangu nyuma yangu, baba uwalinde, nifanye nikutane nao Mbinguni, baba unajua ni kiasi gani ninampenda mke wangu na ni kiasi gani ninampenda binti yangu Alicia. Inaniumiza vibaya kujua kuwa huu ni wakati wangu wa mwisho kuwa nao, ninajua ninakufa na kuwaacha Belinda na Alicia peke yao lakini ninafahamu wakiwa na wewe hawatakuwa wapweke milele.....) Alipofika hapo Prosper alishindwa kuendelea na kuanza kulia.
“Daddy what’s going to kill you? But you said you will be home this Christmas!” (Baba nini kitakuua, lakini si ulisema utakuwa nyumbani Christmas hii!”) Alicia aliuliza kwa mshangao ilikuwa ni mara ya kwanza kwake kusikia kuwa baba yake angekufa.
“My daughter Alicia let me reveal the truth to you today, the truth that even you mother never knew about!”(Mwanangu Alicia acha nikuonyesha ukweli wote leo, ukweli ambao hata mama yako hakuwahi kuufahamu!)
Baada ya kusema hayo huku Belinda na Alicia wakiendelea kulia, Prosper alisimulia kila kitu kilichotokea katika maisha yake na nini kilichopelekea awe gerezani, Belinda alionekana kufungua mdomo wake kwa mshangao wakati Prosper akielezea kilichotokea, siku zote alielewa kitu tofauti kabisa.
“Kwa hiyo hukumuua baba yako!”
“I didn’t kill him but my mom did!) (Sikumuua baba ni mama yangu aliyemuua baba)
“Why are you in Prison then? (Sasa kwanini upo gerezani).
“Nilimpenda sana mama yangu, sikutaka kitu kibaya kimtoe maana nikasema ni mimi ndiye niliyemuua baba ili tu mama yangu aachiwe huru na mimi nikawekwa gerezani, sikuwahi kukueleza hili Belinda lakini leo ni lazima nikuambie ukweli, nakufa sababu ya mama yangu ingawa naye hivi sasa ni marehemu, nitaonana naye ahera kesho! Nakupenda sana Belinda na kuomba umtunze sana mtoto wetu ingawa naye ni mgonjwa mara kwa mara lakini mpeleke hospitali ipo siku atapona!”
Hawakuongea kitu tena zaidi ya kuendelea kulia kwa pamoja muda mrefu mpaka askari walipokuja na kumfunga Prosper kwa kitambaa cheusi tena usoni, Belinda na Alicia walimkumbatia na kumbusu usoni kwa mara ya mwisho akaanza kuvutwa kutolewa chumbani.
“I love you Belinda! I love you Alicia! I will love you forever, see you in Heaven! (Nakupenda Belinda! Nakupenda Alicia, nitawapenda milele, tutaonana mbinguni!) alisema Prosper huku akivutwa na maaskari kutolewa chumbani.
Walipotoka chumbani huku wakilia Belinda na mtoto wake walinyoosha moja kwa moja hadi kituo cha basi, habari aliyoisikia siku hiyo kwa Prosper ilimsikitisha sana Belinda, alikuwa ameamua kwenda kufanya kila lililowezekana kumwona Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kumsimulia juu ya jambo hilo, alipita ofisini kwa wakili wake na kumweleza na wote walinyoosha hadi ofisini kwa Mwanasheria Mkuu!
*********
“Nasikitika leo hamuwezi kumwona ana kazi nyingi sana!” alisema Katibu Muhtasi wake!”
“Hapana dada ni jambo muhimu sana linalohusu kifo, tusipomuona leo kesho mtu ananyongwa na ana uwezo wa kuzuia!” alijibu Belinda huku akilia machozi.
“Hebu subirini nimuulize?” alisema Katibu huyo na kunyanyua simu iliyokuwa mezani kwake, alisikika akiongea na mtu na alipoweka simu chini alimgeukia Belinda.
“Dada nakuhurumia ila sina jinsi ya kukusaidia, Mwanasheria amesema mje kesho saa nne kamili ataonana nanyi!”
“Mume wangu ananyongwa saa 4.30 tu dada!”
“Siwezi kulazimisha awaone kwa kweli huyo ni bosi wangu!”
Belinda na mwanaye waliondoka pale wakilia machozi na kwenda nyumbani kwao ambako Belinda chakula hakikulika wala usingizi haumwijia alikesha usiku mzima akisali kumwomba Mungu afanye miujiza yake.
******
Siku iliyofuata asubuhi na mapema Prosper alianza kuandaliwa kwa ajili ya kifo! Alipewa muda wa masaa mawili kusali na kusoma Biblia ili kutubu dhambi zake, ilipofika saa nne kamili alitolewa chumbani kwake akiwa amefungwa kitambaa cheusi usoni na kupelekwa katika chumba maalum cha kunyongea, kilichoitwa Death room, ambako alilazwa katika kitanda maalum tayari kwa kifo.
Mtaalam wa kuua aliyeitwa bwana Nyonganyonga ambaye kwake kutoa roho za watu ndio ilikuwa kazi yake, alisimama pembeni mwa kitanda cha kifo akimwangalia Prosper kwa huruma ni kwa mara ya kwanza katika kazi yake aliyoifanya kwa miaka 15 alijisikia kumwonea mtu huruma kiasi hicho!
“Kweli uliua?” Alimuuliza Prosper
“Sikuua?”
“Ila?”
“Ni mama yangu aliyeua mimi nilisema nimeua ili kumwokoa mama asife!”
“Kwa hiyo wewe upo tayari kufa kwa ajili ya mama yako?”
“Ni sawa tu!”
“Mama yako hivi sasa yupo wapi?”
“Alifariki kwa Kifua Kikuu muda mfupi baada ya kutoka gerezani!”
“Kwa hiyo upo tayari kufa?”
“Sawa tu!”
Bwana Nyonganyonga alikuwa tayari na sindano yake ya dawa ya Digoxmait Tayari kwa kumchoma Prosper ikitimia saa 4.30 juu ya alama!, sumu hiyo iliua kwa kuusimamisha moyo kusukuma damu.
Wakati huo tayari ilikuwa ni saa 4.20! Prosper alilala pale akisubiri kifo, zilikuwa zimebaki dakika kumi tu achomwe sindano ya sumu, alijaribu kukifikiria kifo na kushindwa kukielewa.
“Hivi inakuwaje mtu akifa, kweli nitawasahau Belinda na Alicia?” alijiuliza Prosper na picha ya mke na mtoto wake ilimwijia kichwani akasikia huzuni kubwa sana moyoni mwake! Alipotupa macho ukutani tayari ilikuwa saa 4.25 zilikuwa zimebaki dakika tano afe!
“Nichome hiyo sindano, nataka kufa unasubiri nini?” Prosper alisema katika hali ya kukata tamaa.
*******
BELINDA SAA 4. KAMILI OFISINI KWA MWANASHERIA
“Karibuni Mwanasheria anawasubiri!” Katibu Muhtasi aliwakaribisha
Belinda, Alicia na wakili Joseph Mziray waliingia ofisini na kwenda moja kwa moja hadi mbele ya meza yake, Mwanasheria alikuwa mzee wa makamo mwenye umri kati ya miaka 50-55, kichwa chake kilijaa mvi nyingi sana na alivuta kiko!
“Shikamoo mzee” Belinda na wakili walimwamkia
“Marahaba!”
“Niwasaidie nini?”
Belinda alianza kusimulia kila kitu kilichotokea huku machozi yakimtoka, Alicia pia alilia machozi akiliita jina la baba yake! Maneno ya Belinda yalimwingia Mwanasheria akajikuta akinyanyua simu na kuanza kubonyeza namba fulanifulani.
“Shikamoo Mheshimiwa Rais!” kuna habari ya kusikitisha sana hapa juu ya yule kijana anayenyongwa leo!”Mwanasheria alisimulia kila kitu katika simu alipokata simu alichukua kalamu na karatasi na kuanza kuandika kitu fulani.
“Rais ameamua kusitisha adhabu ya kifo kwanza mpaka uchunguzi ufanyike!” Alisema mwanasheria mkuu.
“Haleluya!”Belinda aliruka juu na kushangilia.
“Chukueni hii barua muikimbize gerezani haraka iwezekanavyo!”
“Hivi sasa ni saa 4.10 Mheshimiwa tuna dakika ishirini tu, hatuwezi kuwahi lazima tutakuta amenyongwa!”
“Hizo zinatosha! Gari linawasubiri hapo chini!”
Waliteremsha ngazi kwa haraka hadi chini ambako walikuta gari aina ya Ladrover 110 likiwasubiri tayari kwa safari ya kuelekea Segerea, wote waliingia na kwa kasi ya gari lilianza kuondoka wakati wanafika gerezani ilikuwa tayari saa 4:29:30, zilikuwa zimebaki sekunde 30 tu! Belinda aliruka na kuanza kukimbia hadi kwenye lango la kuingilia gerezani ambako alianza kupiga kelele.
“Jamani msimuue mume wangu! Barua hii hapa kutoka kwa Mwanasheria, aliwakabidhi maaskari waliokuwa getini walipoiangalia ilikuwa na muhuri wa Mwanasheria Mkuu na iliandikwa neno ‘URGENT’ ikimaanisha ‘HARAKA’
“Mungu wangu mbona zimebaki sekunde 15 tutawahi kweli?” alisema askari mmoja baada ya kuangalia saa yake na palepale alitoka mbio kwenda ndani kujaribu kuokoa maisha ya Prosper, Belinda, Alicia na wakili walibaki nje wakisubiri jibu! Waliendelea kulia machozi waliomba muujiza utokee!
Jua lilikuwa bado halijaanza kuchomoa vizuri, hivyo hali ilikuwa bado ya ubaridi asubuhi ya siku hiyo, msichana alitembea kandokando ya barabara akielekea shuleni baada ya kuteremshwa na gari la nyumbani kwao, alivaa vizuri na kuufanya uzuri wake uongezeke maradufu!
Katika umri wa miaka 16 tu msichana huyo alikuwa msichana mrembo mno! Kwanza alikuwa mrefu, mwembamba mwenye macho ya kulegea, alikuwa na nywele ndefu, miguu minene iliyomfanya avutie zaidi.
Hapakuwa na msichana mzuri kama yeye katika shule yao ya St. Magreth jambo lililofanya atamaniwe na kila kijana shuleni hapo mpaka walimu wake, mpaka wakati huo alishasababisha walimu wawili kufukuzwa kazi baada ya majaribio ya kumbaka ofisini! Wengi walimwita kwa jina la queen ingawa jina lake halisi lilikuwa Belinda.
Alizaliwa katika familia yenye kila kitu, familia tajiri, baba yake alimiliki majumba mengi ya kifahari jijini Dar es Salaam, meli nyingi za kusafirisha mizigo katika bahari ya Hindi na maduka mengi makubwa karibu kila mkoa nchini Tanzania.
Familia ya msichana huyu ilikuwa ya watoto watatu, ndugu zake wawili David na John wakiwa wa mama mmoja na yeye alizaliwa peke yake kabla baba yake hajafunga ndoa na mama yao David na John, Angelina Kapinga.
Baba yake Thomson Komba alimpenda sana Belinda pengine kuliko hata David na John na alimpa kila kitu, lakini mama yake wa kambo hakumpenda Belinda hata kidogo! Alimfanyia kila aina ya manyanyaso na kuyafanya maisha yake kuwa ya shida na huzuni kubwa .
Mbegu ya chuki ilipandikizwa hadi ndani ya mioyo ya kaka zake David na John! Walimchukia Belinda kupita kiasi, baba yao alijitahidi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha upendo unakuwepo kati ya watoto wake lakini haikuwezekana kwa sababu mbegu ya chuki baina ya watoto ilitoka kwa mama aliyekaa na watoto muda mwingi.
MzeeThomson alikuwa mtu wa safari nyingi kupita kiasi, katika mwezi ni wiki moja tu aliyokaa nyumbani, wiki nyingine tatu zote alizimaliza katika safari zake za kibiashara, ni katika muda huo ndio Belinda alipata mateso makali kutoka kwa mama yake wa kambo, alinyimwa chakula! Alipigwa na kupewa kazi ngumu kila alipotoka shuleni.
Baba yake aliporudi kutoka safari Belinda hakudiriki hata siku moja kufungua mdomo wake kueleza yaliyompata kwa kumwogopa mama yake wa kambo, maisha yake yalijaa huzuni na muda wote alikuwa mnyonge na hata kupungua uzito.
Baba yake aliligundua hilo na ili kumuepushia matatizo zaidi aliamua kumhamishia Belinda katika shule ya St. Magreth iliyokuwa ya bweni ambako aliendelea na masomo yake vizuri na kufaulu mtihani wake wa kidato cha nne akachaguliwa kuendelea na kidato cha tano na sita katika shule hiyo hiyo.
********
“Fungua mlango wee kenge!”
Hiyo ndiyo ilikuwa kauli ya mzee Kabaka kila aliporejea kutoka ulevini saa 8:30 usiku kila siku! Prosper aliyelala chumba cha karibu na mlango wa kuingilia ndani waa kibanda chao kidogo cha vyumba viwili alinyanyuka na kwenda kumfungulia baba yake mlango!
“Weee! Unafungua mlango wewe ndiyo mke wangu?” Ndilo swali ambalo mzee Kabaka alimuuliza Prosper.
“Hapana baba mama amelala!”
“Niniiii? Funga huo mlango upesi kabla sijakuvunja mbavu na kimbia upesi ukamuamshe mama yako aje anifungulie mlango!”
Bila ubishi sababu aliyesema ni baba yake Prosper aliufunga mlango na kwenda chumbani kumwamsha mama yake.
“Mama! Mama! Mama! Baba amekuja amka ukamfungulie!”
“Mfungulie tu wewe mwanangu mimi atanipiga!”
“Amekataa mimi kumfungulia!”
Baada ya jibu hilo mama yake Prosper, Kalunde Katunzi alisikia dirisha la chumbani likipondwa na jiwe kubwa akashtuka na kuchukua shuka alilokuwa amejifunika na kufunga kifuani.
“Wee kenge hivi hutaki kunifungulia? Nikiingia humo ndani hakyanani leo nakutoa roho, nilishakukata sikio moja hujasikia eh?” Alisema mzee Kabaka.
“Nakuja mume wangu!” Alijibu mama yake Prosper huku akitetemeka na kuanza kukimbia kwenda kufungua mlango, alimgonga Prosper aliyekuwa amesimama njiani wakati akikimbia.
Alimuogopa sana mume wake na alijua siku hiyo angepata kipigo kikubwa mno, Prosper mtoto mkubwa wa mama huyo akifuatiwa na wadogo zake Nyamizi na Kasanda, alimfuata mama yake nyuma alijua angepigwa na alitaka kumsaidia.
Alipoingia tu ndani baada ya kufunguliwa mlango baba yake aliyekuwa kipande cha mtu cha miraba minne, mwanajeshi aliyepigana vita vya Kagera lakini aliporudi akaasi jeshi na kuamua kufanya biashara zake, alimdaka mke wake na kumpiga ngumi mdomoni, meno kama matatu hivi yakadondoka chini! Damu nyingi zikatapakaa sakafuni, hakumwachia hapo alimfuata na kumpiga teke tumboni akaanguka chini.
“Prosper! Prosper! Prosper! Mshike baba yako ataniua!” Alisema mama huyo na baadaye kukaa kimya huku akiendelea kutoka damu, hiyo ndiyo ilikuwa kawaida mama huyo aliishi kwa mateso jambo lililomkera sana Prosper na dada zake.
“Baba mwache mama! Kwanini unampiga hivyo si keshakufungulia mlango?”
“Wee unanishika unataka kunichangia na mama yako siyo?”
“Sitaki kukupiga baba lakini naomba usimpige mama kiasi hicho hana kosa!”
Wakati Prosper akiongea maneno hayo tayari Kasanda na Nyamizi walishafika na kumnyanyua mama yao aliyekuwa amelala chini akiwa amepoteza fahamu huku damu nyingi zikimtoka mdomoni, midomo yake ya juu na chini ilikuwa imevimba kwa ngumi aliyopigwa na mume wake, wakambeba na kumpeleka chumbani kwao ambako walimmwagia maji akarejewa na fahamu.
“Mama twende polisi!” Kasanda alimshauri mama yake.
“Hapana watoto wangu tukienda polisi baba yenu atafungwa! isitoshe sisi Wanyamwezi hatutakiwi kabisa kushtaki polisi tunapopigwa na waume zetu”
Watu wote katika kijiji cha Tutuo barabara ya kwenda Sikonge walikoishi Prosper na wazazi wake walitambua ukorofi wa mzee Kabaka na hakuna mtu aliyediriki kumkemea, kila mtu alimuogopa.
Kama ungefanikiwa kukutana na mama Kalunde, sio siri machozi yangekutoka, alikuwa ni mama wa makamo, mrefu mwenye umbile la kitutsi,rangi ya ngozi yake ilikuwa nyeusi lakini iliyojaa makovu mengi, kwa kumwangalia ungegundua kabisa kuwa mama huyo aliwahi kuwa tishio wakati wa ujana wake!
Alikuwa ni mama mwenye mateso, alipigwa karibu kila siku na mume wake,hakuwa na sikio moja tayari lilishakatwa na mumewe! Jicho lake la kulia lilikuwa chongo baada ya kupasuliwa na mume wake wakati wa kupigwa miaka miwili kabla ya siku hiyo! Alikuwa ni mama aliyepata mateso makubwa mno katika maisha yake ya ndoa.
Wakati hayo yote yakitokea Prosper alikuwa na umri wa miaka 17 akimalizia kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Sikonge, pamoja na matatizo aliyokuwa nayo alifanikiwa kuchaguliwa kuendelea na kidato cha tano katika shule ya sekondari ya St.Magreth ilikuwa ni shule ya bweni, na ilikuwa ni lazima aende kuishi bwenini akiwaacha dada zake Kasanda na Nyamizi pamoja na wazazi wake.
“Prosper tutaweza kweli kumhimili baba akimpiga mama?”
“Mungu atawasaidia dada zangu sina budi kwenda shule ili niwasaidie baadaye!” Prosper aliwaeleza dada zake wakati wa kuagana, akaondoka kwenda zake Moshi shuleni.
Alipofika shuleni kwa mara ya kwanza alikuwa amechelewa na kilichomchelewesha zaidi ilikuwa ni ada, mama yake Kalunde alilazimika kufanya vibarua katika mashamba ya watu ili aweze kupata pesa za kumwezesha Prosper kwenda shule! Baba yake hakujali kabisa.
“Prosper mwanangu usifanye michezo shuleni, si unaona maisha yetu yalivyo na unaona nilivyohangaika? Baba yako hana msaada wowote, yeye ni pombe kila siku na kunipiga mimi tu, familia nzima tunakutegemea wewe uje kuwa mkombozi wetu kajitahidi mwanangu!”
“Sitakuangusha mama nakuahidi! “
“Sawa mwanangu!”
Darasa lao lilikuwa na wafunzi hamsini na mbili kati yao wasichana wakiwa kumi na saba! Ni Prosper peke yake aliyeonekana kuwa na uwezo mdogo kifedha na watu wengi walimdharau, alikuwa na nguo zilizochanika na madaftari yake yalikuwa ni ya kurasa shirini na nne ambayo hayakutumiwa na wanafunzi wengi shuleni hapo! Yalidaiwa kuwa ya watoto wa shule za msingi.
Pamoja na umasikini wake Prosper alijitahidi sana na masomo kama alivyomuahidi mama yake na hiyo ni kwa sababu aliifahamu familia yake, alitaka asome ili apate uwezo wa kuwakomboa ndugu zake, barua zilizokuja kutoka nyumbani kwao zilimweleza juu ya kipigo alichopata mama yake na Prosper alilia.
Wanafunzi wengi walimtenga sababu ya umasikini wake isipokuwa msichana mmoja tu aliyeitwa Belinda!Msichana huyo alimsaidia Prosper kwa vitu vingi shuleni ikiwemo Sabuni, mafuta na hata sukari na wakatokea kuwa marafiki wakubwa.
Katika mtihani wa mwisho wa muhula aliwashangaza wengi pale alipoibuka na kushika namba ya kwanza kati ya wafunzi wote! Ni matokeo hayo ndiyo yalianza kumpa heshima na marafiki wengi shuleni.
******
Shule zilipofungwa kwa sababu Prosper hakuwa na nauli ya kumrudisha hadi nyumbani kwao Tabora, ilibidi abaki shuleni peke yake akijisomea! Alimkumbuka sana mama yake na alitaka kwenda nyumbani lakini kwa sababu hakuwa na nauli alilazimika kubaki peke yake shule nzima.
Shule zilipofunguliwa wanafunzi wote walirejea shuleni na yeye na Belinda msichana aliyeonekana kutoka familia tajiri jijini Dar es Salaam, walisoma na kufanya kila kitu pamoja Belinda alikuwa miongoni mwa wasichana wagumu kuelewa masomo yao, lakini Prosper alitumia muda wake mwingi kumfundisha hatimaye akawa miongoni mwa wasichana waliofanya vizuri katika mitihani yao.
Mwisho wa muhula wa pili Prosper alishika tena namba ya kwanza darasani kwake na Belinda aliibuka katika kumi bora! Kila mtu mpaka walimu wake walishangaa,hilo liliukomaza zaidi uhusiano wao.
“Prosper utakwenda Tabora likizo hii?”
“Mimi? Mimi? Hapana sitakwenda!”
“Kwanini?”
“Sina nauli ya kunipeleka nyumbani nendeni tu mtanikuta!”
“Hapana Prosper this time ni lazima uende!”
“Nitakwenda na nini sina nauli Belinda?”
“Nitakupa nauli ya kukupeleka na kukurudisha!” Alisema Belinda.
Prosper hakuamini aligeuka na kumwangalia Belinda usoni, wote wawili walijikuta wakitabasamu na baadaye kukumbatiana na kuanza kupigana mabusu usoni, Belinda alijaribu kuupenyeza ulimi wake kuuingiza mdomoni kwa Prosper lakini Prosper aliuma meno yake kuonyesha hakupenda kitu hicho kitokee!
“Belinda unataka kufanya nini?”
“Nakupenda Prosper tafadhali tunyonyane ndimi!”
“Nitatapika Belinda sijawahi kufanya kitu kama hicho hata siku moja!”
Belinda alishindwa kuendelea lakini alijua ni kwanini Prosper alisema hivyo, alimwachia na wakaendelea na safari yao kuelekea mabwenini kujipumzisha wakisubiri siku inayofuata.
Asubuhi kitu cha kwanza alichofanya Belinda ni kumkabidhi Prosper kiasi cha shilingi 50,000 kwa ajili ya nauli ya kumpeleka Tabora na kumrudisha shuleni.
“Belinda mbona pesa hizi ni nyingi sana!”
“Zitakazobaki utawanunulia wazazi na ndugu zako zawadi!”
“Ahsante Belinda, sikutegemea!”
“Ahsante wewe kwani bila wewe mimi nisingefanikiwa kimasomo? Isitoshe nakupenda Prosper huwezi kupata taabu wakati mimi nina kitu!”
“Belinda mzazi wako ni nani hasa hapa nchini?” Ilibidi Prosper aulize, sababu alishangazwa na msichana mdogo kama Belinda kuwa na kiasi kile chapesa.
Belinda alimweleza kila kitu kilichokuwepo katika maisha yake, alieleza pia juu ya utajiri wa baba yake na jinsi baba yake alivyompenda sababu alikuwa mtoto pekee wa kike! Hakuacha kumweleza juu ya mama yake wa kambo.
“Nina kila kitu nyumbani isipokuwa upendo wa mama, mama yangu wa kambo ananitesa sana, hanipendi amewafanya hata kaka zangu wa kambo pia wanichukie!”
“Unafikiri ni kwanini?”
“Kwa sababu wanajua baba ananipenda na kuna uwezekano wa kupata sehemu kubwa sana ya mali yake akifa, hiyo nafikiri ndiyo sababu kubwa!”
“Pole!”
“Ahsante, lakini nataka uelewe nakupenda na tukirudi kutoka likizo safari hii nataka kila mtu aelewe jambo hapa shuleni ili wavulana waache kunisumbua!”
“Huogopi kuchekwa Belinda!”
“Kwanini?”
“Sababu mimi ni masikini!”
“Nakupenda kwa jinsi ulivyo Prosper!”
Ni kweli Prosper alikuwa na sura ya kumvutia kila mwanamke kilichomsumbua kilikuwa ni umasikini.
******************
Prosper alikata tiketi ya treni na kusafiri hadi Tabora mjini ambako alipanda mabasi ya kumpeleka hadi nyumbani kwao Tutuo, kiasi cha kilometa sabini hivi kutoka Tabora mjini, njia nzima alimfikiria mama yake alitaka sana kumwona! Ulikuwa umepita muda mrefu bila kuonane naye! Mawazo juu ya dada zake na baba yake hayakumuumiza kichwa sana, alimuwazia mama yake zaidi, alimpenda sana na hapakuwa na mtu mwingine kama mama maishani kwake!
Aliposhushwa na basi kituoni kitu cha kwanza alichofanya ni kukimbia dukani na kununua vitenge doti tatu kwa ajili ya mama yake na pia alinunua magauni mawili kwa ajili ya dada zake, Nyamizi na Kasanda! Hakusahau kumnunulia baba yake suruali nzuri! Moyo wake ulijaa furaha, alikuwa na hamu kubwa mno ya kuiona familia yake tena.
Baada ya manunuzi hayo alinyoosha moja kwa moja kwenda nyumbani kwao,njiani akiwa amebeba begi lake alishangaa jinsi ambavyo watu walimwangalia na kuonyesha masikitiko.
Alipofika nyumbani kwao hakuna mtu aliyejitokeza kumpokea, mlango wa nyumba ulikuwa wazi, ilibidi aingie hadi ndani akiliita jina la mama yake, lakini hakuitikiwa, mwisho alianza kuita majina la dada zake lakini bado ilikuwa kimya.
Wakati bado akijiuliza maswali kichwani mwake alitokea rafiki yake mkubwa aliyeitwa Kategile na kusimama mbele yake.
“Pole sana Prosper bahati mbaya umechelewa mazishi!”
“Ya nani?” Aliuliza kwa mshangao Prosper.
“Baba yako!”
“Baba?”
ITAENDELEA KESHO HAPA HAPA

Post a Comment